loader
Ukatili kwa watoto unavyoangamiza taifa kimya kimya-1

Ukatili kwa watoto unavyoangamiza taifa kimya kimya-1

JUMATATU Juni 6, 2022 nilifika katika shule za chekechea na msingi za Minazi Mirefu na Airwing zilizopo eneo la Jeshi la Anga wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam.

Sababu ya kwenda ni baada ya kupata tetesi zinazodai kuwa wanafunzi zaidi ya 10 wamefanyiwa ukatili wa kingono na mzee muuza matunda ambaye alikuwa akifanya biashara nje ya ukuta wa shule hizo kwa zaidi ya miaka 10.

Muuza matunda huyo anadaiwa kuwafanyia vitendo hivyo katika nyumba ambayo nyakati za jioni hutumika kwa ajili ya kufanyia mazoezi, funguo za nyumba hiyo zilikabidhiwa kwa babu huyo kwa ajili ya kuhifadhi vifaa vya biashara yake anapomaliza.

Shule hizo zipo ndani ya uzio mmoja wenye milango miwili inayowahudumia walimu na wanafunzi, geti la upande wa Kusini ni kwa ajili ya Minazi Mirefu na Magharibi ni kwa ajili ya Airwing. 

Katika kila geti alionekana mlinzi ambaye aliruhusu wanafunzi kutoka na kuingia na nilivyoomba ruhusa ya kuingia ndani kupitia geti la Minazi Mirefu aliniruhusu. 

Nilifika katika shule hizo baada ya kuwasiliana na mmoja wa wazazi ambaye mtoto wake alifanyiwa kitendo hicho.

Baada ya kuingia nikiwa na mwalimu (jina linahifadhiwa) nilifanikiwa kuzungumza na mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Minazi Mirefu mwenye umri wa miaka minane akasema kuwa alifanyiwa kitendo hicho mara moja baada ya kupelekwa na rafiki yake.

“Rafiki yangu (jina limehifadhiwa) aliniambia twende kwa babu tukachukue matunda tulivyofika babu akanichukua na kunipeleka kwenye kile chumba na kunifanyia mchezo mbaya, akanipa dawa nikameza na machungwa mawili akaniambia nisimwambie mama wala mwalimu,” anaeleza mwanafunzi huyo.

Awali katika siku tofauti wazazi watatu tofauti walifika katika shule hizo wakiambatana na vyombo vya usalama kutaka kuthibitisha kuwa watoto waliofanyiwa kitendo cha ulawiti ni wanafunzi katika shule hizo jambo ambalo lilithibitika.

Baada ya hatua ya wazazi hao, ilibainika kuwa watoto waliofanyiwa kitendo hicho ni zaidi ya watatu kutokana na watoto hao kutajana kila walipohojiwa. 

“Huwa ninatabia ya kuzungumza na mtoto wangu sasa wakati tukiongea aliniambia anapata maumivu sehemu ya kutolea haja kubwa baada ya kumdadisi akaniambia kitendo alichofanyiwa na huyo babu nilimpeleka Hospitali Amana akapimwa na kweli alikutwa na michubuko,” anabainisha mmoja wa wazazi.

Mzazi mwingine anaeleza: “Sisi tumejitokeza ili tujue na kufuatilia jambo hili ili watoto wetu wapate haki zao lakini naumia ninapoona wazazi wengine hawapo tayari kujihusisha na kesi hii licha ya watoto wao kufanyiwa mchezo mchafu,” alieleza mzazi huyo.

Baada ya maelezo hayo nilimfuata mzazi ambaye hakutaka kuchukua hatua, akasema: “Hivi vitu huwa vina mlolongo mrefu hivyo nitatumia muda mwingi na ni gharama kufuatilia kesi, mimi namwachia Mungu hao waliojitokeza wanatosha.”

Hata hivyo, baada ya mahojiano kwa baadhi ya wazazi, mzazi mwingine aliungana na wenzake watatu kutafuta haki ya watoto wao na kufanya idadi ya wazazi kuwa wanne.

Katika mazungumzo yangu na uongozi wa Shule ya Airwing ilithibitisha kuwepo kwa wanafunzi wanaodaiwa kufanyiwa ukatili huo.

Mwalimu Mkuu Msaidizi, Fatihuba Karata anaeleza kuwa ana taarifa za watoto wawili wanaodaiwa kufanyiwa ukatili.

“Hizo taarifa tumezipata lakini shule haihusiki kwa chochote, walikuja wazazi wawili ambao watoto wao wanasoma darasa la pili na darasa la awali na wazazi ndio walimkamata mtuhumiwi na kumpeleka polisi,” anafafanua.

Kwa upande wa Shule ya Msingi Minazi Mirefu, Mwalimu Mkuu, Brutu Msenga anathibitisha kuwepo kwa mwanafunzi aliyefanyiwa kitendo hicho.

Polisi wamshikilia mtuhumiwa

Wakati wa mahojiano Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema wanamshikilia mtuhumiwa Joshua Simangwe (66) mkazi wa Kipunguni, Ukonga kwa kosa la ubakaji.

Baada ya maelezo hayo HabariLEO ilimuuliza kamanda kwanini mtuhumiwa alifunguliwa shitaka la ubakaji pekee wakati anadaiwa kulawiti pia, alisema matukio yote hayo ni ukatili wa kingono na kumtaka mwandishi aandike ukatili wa kingono.

Malalamiko ya wazazi

Baada ya kukaa kwa muda wa wiki mbili na siku bila kuelewa kinachoendelea wazazi wa wanafunzi hao walilalamika kuzungushwa na polisi.

Mwandishi alipomtafuta Kamanda Muliro, alisema ametoa maelekezo ya kukamilishwa kwa uchunguzi haraka ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani.

Juni 13 mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya kulawiti mtoto mwenye miaka minane huku mafaili mengine yakiwa bado hayajafikishwa mahakamani.

HabariLEO inafuatilia kesi hiyo mpaka pale hukumu itakapotolewa.

Ukatili wa kingono janga kubwa  

Matukio ya ukatili kwa watoto ni kinyume cha Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019 pamoja na sheria ya kanuni ya adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2021.

Katika Kituo cha Mkono kwa Mkono kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Amana wilayani Ilala, Dar es Salaam inaripotiwa kuwa watoto wawili hadi watatu wanafanyiwa vitendo vya kikatili kila siku.

Ripoti ya Polisi inaeleza kuwa Mkoa wa Kipolisi Ilala una matukio ya ukatili kwa watoto 489 ikitajwa kuwa ya tano katika mikoa vinara. 

Kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii wa kituo hicho, Suphiani Mndolwa, ukatili unaoongoza kufanyiwa watoto ni wa kingono ambao ni ubakaji na ulawiti.

Mdolwa anasema ukatili huo mara nyingi unatokea ndani ya jamii ambapo watoto wa kike ndio wanaoathirika zaidi.

Pamoja na hayo Utafiti wa Serikali na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) unaonesha asilimia 60 ya matukio yanatokea nyumbani na asilimia 40 shuleni.

Aidha, takwimu za polisi nchini katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 zinaonesha kuwa matukio ya ukatili kwa watoto 11,499 yaliyoripotiwa ikilinganishwa na matukio 15,870 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Mikoa iliyoongoza kwa vitendo hivyo ni Arusha (808), Tanga (691), Shinyanga (505), Mwanza (500) na Mkoa wa Kipolisi Ilala (489). 

Aidha, makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ni ubakaji (5,899), mimba kwa wanafunzi (1,677) na ulawiti (1,114). 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima anathibitisha kuwa, pamoja na jitihada za kukabiliana na vitendo vya ukatili, bado taarifa za vitendo hivyo hususani kwa watoto zinaendelea kuongezeka ikiwemo ubakaji, ulawiti, utumikishwaji wa watoto katika ajira hatarishi, ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni na ukatili mwingine.

"Wizara kwa kushirikiana na wadau wake tunaratibu kampeni shirikishi ya jamii iitwayo SMAUJATA (Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii, 2022) ili kukomesha ukatili katika jamii,” anaeleza Dk Gwajima.

Itaendelea toleo lijalo

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/575f31be9d5553f52cd214c1abd39d08.jpg

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Aveline Kitomary

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi