loader
Ukatili kwa watoto unavyoangamiza taifa kimya kimya-2

Ukatili kwa watoto unavyoangamiza taifa kimya kimya-2

JUMATATU iliyopita tuliangalia sehemu ya kwanza ya makala haya inayohusu ukatili wa kingono waliofanyiwa watoto zaidi ya 10 katika shule mbili za awali na msingi za Minazi Mirefu na Airwing zilizopo eneo la Jeshi la Anga wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Gazeti hili lilifika katika shule hizo Juni 6, mwaka huu (2022) kufuatilia habari hiyo ya ukatili dhidi ya watoto waliofanyiwa kwa zamu na nyakati tofauti na mtu anayedaiwa ni muuza matunda nje ya shule hizo.

Muuza matunda huyo anayefanya biashara hiyo nje ya shule hizo kwa zaidi ya miaka 10, anadaiwa kuwafanyia vitendo hivyo watoto hao katika nyumba ambayo nyakati za jioni hutumika kwa ajili ya kufanyia mazoezi. Funguo za nyumba hiyo zilikabidhiwa kwa babu huyo kwa ajili ya kuhifadhi vifaa vya biashara yake anapomaliza.

Shule hizo zipo ndani ya uzio mmoja wenye milango miwili inayowahudumia walimu na wanafunzi, geti la upande wa Kusini ni kwa ajili ya Minazi Mirefu na Magharibi ni kwa ajili ya Airwing.

MABADILIKO MTINDO WA MAISHA KUCHANGIA UKATILI

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Kituo cha Mkono kwa Mkono kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Amana wilayani Ilala, Dar es Salaam, Suphiani Mndolwa, anasema matukio hayo ya kikatili yanasababishwa na uangalizi mdogo wa watoto, mmomonyoko wa maadili, kisasi na imani za kishirikina.

Mndolwa anasema kwa kiasi kikubwa ukatili unasababishwa na wazazi kutokuzingatia au kufuatilia malezi, makuzi na maendeleo ya watoto.

Anasema katika kesi walizofuatilia wapo watu ambao utotoni walifanyiwa vitendo vya kikatili kama ulawiti na hivyo mioyo yao inabaki na visasi.

“Na kwa sababu wana visasi wanalipizia kwa watoto, wengine ni miili kuingia tamaa hivyo watu waliopitia ukatili wanahitaji kutibiwa kisaikolojia.

“Kuna watu wakati mwingine wazazi au walezi wanawafanyia ukatili watoto kutokana na imani za kishirikina eti watapata mali kitu ambacho si sahihi,” anasema Mndolwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki Mwenge (MWUCE), Cristian Bway anasema mabadiliko ya mtindo wa maisha yanachangia ukatili kwa watoto.

Anasema wazazi wengine hawana uelewa wa namna ya kushughulika na watoto wa kizazi cha sasa kwani wanaishi kwenye mazingira ambayo wanapata taarifa nyingi na wanajifunza vitu huku wazazi wakiwa hawafuatilii.

Sababu nyingine anayoiainisha ni wazazi au walezi kutokuwa karibu na watoto na kuwajengea kutojiamini hivyo anapokutana na kitu cha kumhatarisha hawawezi kusema.

“Zamani baba akienda kutafuta mama yuko nyumbani na ndio mlezi hivyo uwezekano wa mtoto kukutana na watu wa hatari ulikuwa mdogo sasa wazazi wana mambo mengi baba anatoka na mama anatoka mtoto hana wa kumuangalia hilo linachangia,” anabainisha Bway.

UKATILI HUHARIBU USTAWI WATOTO

Miongoni mwa madhara ya ukatili  kwa watoto yaliyoainishwa ni kuangamiza ustawi wa taifa la kesho.

Mndolwa anasema endapo mtoto wa kiume atafanyiwa ulawiti leo asipopata msaada atashindwa kusimama katika nafasi yake atakapokuwa mtu mzima (baba).

“Hata watoto wa kike wakifanyiwa ukatili wanaweza kushindwa kusimama katika nafasi zao kesho kwani kuna madhara makubwa ya kisaikolojia,” anaeleza.

Msaikolojia Bway anasema ukatili unaweza kusababisha matatizo ya kisaikolojia ambayo yanaweza kuharibu maisha ya mhusika kwa kushindwa kufikiri kuzalisha.

“Wasiposaidiwa kisaikolojia wanaweza kuwa watu wa visasi na hawatakaa sawa katika nafasi zao hata utendaji kazi utasuasua,” anasema Bway.

DINI INAWEZA KUMALIZA UKATILI?

Viongozi wa dini mbalimbali wanasema endapo jamii watazingatia imani njema wanaweza kuachana na vitendo vya ukatili kwa jinsi zote.

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Nuhu Mruma, anasema hofu ya Mungu ina nafasi kubwa katika kuteketeza maovu baina ya watu.

Anasema pia kwa sasa ni muhimu wazazi na walezi kuchukua nafasi zao za malezi kwa vijana na watoto kwa kuwaelekeza mema na mabaya na kuwalea katika maadili ya kidini.

“Sisi kama viongozi wa dini tunakemea vitendo hivyo na wanaofanya vitendo hivyo tunao katika jamii wengine ni watoto wetu, wengine ndugu na waumini wetu kikubwa zaidi ni watu kufuata maadili ya dini hata wale wasio na dini basi wafuate mila na desturi maana hairuhusu mambo hayo,” anaeleza Mruma.

Mruma anasema endapo watoto na vijana watalelewa katika maadili mema wataacha kufanya vitendo vichafu ambavyo ni laana katika jamii na kwa Mungu.

Padri Charles Kitima ni Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), anabainisha kuwa kinachopaswa kuangaliwa katika jamii ni kugeuza dhamira mbaya za watu kwa mafundisho ya dini.

“Watoto kama dini inavyotuambia wanategemea utu wetu na ukaribu wa watu wote katika kuwapa makuzi stahiki kwahiyo ni vizuri watu wote tukumbuke hata mila na desturi zetu, mafundisho ya dini dhidi ya maovu wanayotenda na si suala la kusema tu polisi hawezi kunikamata.

“Sasa hata wazazi wanawafanyia watoto wao ukatili huo hii yote ni kukosa hofu ya Mungu, kuamini ushirikina, jambo hili ni laana kubwa kwa jamii,” anasema Padri Kitima.

WAZAZI WATAKIWA KUFANYA HAYA

Tafiti zinaonesha kwamba watoto wasio na ukaribu na wazazi au walezi wao hukosa uwezo wa kujiamini na hivyo kushindwa kueleza masaibu yao kwa mtu yeyote na mara nyingi huathirika kwa ukatili.

Fatuma Kamramba ni Meneja Huduma ya Simu kwa Watoto C-Sema Zanzibar anaeleza mzazi au mlezi anapaswa kuwa tayari muda wote kumsikiliza mtoto hivyo lazima aanze mapema kujenga ukaribu na mahusiano mazuri yenye upendo.

Kwa mujibu wa Fatuma ni muhimu kuwa na mahusiano yatakayomfanya mtoto kujiamini na kwamba mama au baba awe kimbilio endapo ana jambo linamtatiza na anataka kutoa taarifa.

Anasema katika hali hiyo mzazi au mlezi anapaswa kuanza kumshauri mtoto kwa kuzungumza naye ili kujua kwa undani zaidi na amwambie hatua atakazochukua.

“Kama mzazi au mlezi ataona hawezi kuzungumza na mwanae hasa aliyefanyiwa ukatili wa kingono anaweza kuomba ushauri kwa mtaalamu au kupiga namba 116.

 “Ukimjengea mwanao mazingira rafiki ya kukufikia na kuamini wewe ni msaada kwake atakuwa huru kujieleza kwako hivyo nawashauri wazazi wajenge utaratibu wa kuzungumza na watoto, kuwapa taarifa muhimu za kujitambua, kutambua viashiria vya udhalilishaji na namna ya kujilinda katika umri mdogo,” anashauri.

Bway anasema kuna haja ya kujenga ukaribu kati ya mzazi au mlezi na mtoto ili inapotokea viashiria vya ukatili aweze kutoa taarifa mapema.

Naye Mndolwa anasema wanatoa elimu na kuhimiza wazazi na walezi kuwa makini na taarifa ndogondogo wanazopata kutoka kwa watoto wao.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima anatoa wito kwa wazazi na walezi kuwa karibu na watoto, kuwafundisha kutokubali mtu kugusa mwili wake na kutopokea zawadi zozote.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/51534e8f31d8121fe60a1ae7566eb039.png

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Na Aveline Kitomary

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi