loader
HEET kuneemesha taasisi 17 za elimu nchini

HEET kuneemesha taasisi 17 za elimu nchini

KATIKA kukabiliana na mabadiliko pamoja na changamoto za elimu ya juu za muda mrefu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliandaa na kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Juu (HEDP), ambao uliisha mwaka 2015.

Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa James Mdoe aliyasema hayo katika ufunguzi wa kikao cha kusaini makubaliano ya mkopo wa masharti nafuu wa Mradi wa Mageuzi ya Sekta ya Elimu kwa Ajili ya Kuchochea Uchumi (HEET).

Akinukuliwa katika kikao hicho, Profesa Mdoe anasema mpango huo wa miaka 10 uliisha 2015, ndipo wizara ikajipanga na kutafuta mradi utakaosaidia kukabiliana na changamoto za elimu ya juu nchini ili kuchangia jitihada zinazofanyika kupitia bajeti kuu ya serikali mwaka hadi mwaka.

Mradi huo mpya unaangalia changamoto za uwiano mdogo wa wahitimu wa sekondari wanaojiunga na elimu ya juu ikilinganisha na nchi jirani, kutokuoana kwa ujuzi kwa maana ya kuwa kile kinachofundishwa vyuo vikuu vya Tanzania bado kinatofautiana na kinachotakiwa na soko la ajira.

Licha ya mafanikio yaliyopo ya kuanza bodi ya mikopo na mifumo thabiti ya urejeshaji mikopo ilionekana bado maboresho yanahitajika katika utoaji elimu kwani changamoto za mikopo hazilengi vipaumbele vya taifa.

Kwa maelezo ya Profesa Mdoe, kutokana na changamoto hizo zilizokuwepo baada ya mpango huo kuisha, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Benki ya Dunia (2016-17) ili kupata mkopo wa masharti nafuu. Januari mwaka 2018 hatua ya kwanza ilifanikiwa.

Anaeleza kuwa kutokea hapo hatua mbalimbali za kuandaa mradi huo wa HEET zimefanyika ikiwemo hiyo ya kusaini makubaliano hayo yaliyofanyika kwa taasisi 17.

Kati ya taasisi hizo, 14 ni vyuo vikuu, tatu chini ya wizara ni wanufaika. “Aidha, vyuo vitano vya elimu ya juu vilivyopo Wizara ya Fedha na Mipango navyo vitanufaika kufanya jumla ya wanufaika kufikia 22 na wizara ya elimu ikiwa ya 23,” anasema.

Akielezea maudhui na umuhimu wa makubaliano hayo anasema ni aina ya mikataba ya ufanisi ambayo ina vipengele mbalimbali vya kuhakikisha wanufaika wa mradi wanatekeleza kwa wakati na kwa kufuata kanuni.

Profesa Mdoe anasema kuna kifungu kimeipa mamlaka Wizara ya Elimu kusitisha utekelezaji na kuhamisha matengeo ya fedha ya taasisi moja na kuyapeleka kwenye taasisi nyingine.

“Mfano Wizara ya Elimu itaweka vihunzi hasa katika ujenzi na mfano ifikapo tarehe fulani taasisi ambayo itakuwa haijaingia mikataba na kuanza ujenzi basi fedha hizo zitahamishwa.

“Hii itasaidia Wizara ya Elimu kuondokana na uzembe uliokwisha tokea kwa taasisi kukaa na fedha za mradi zaidi ya miaka mitatu bila mikataba yoyote ya ujenzi kufanyika licha ya mahitaji makubwa ya miundombinu vyuoni,” anasema.

Kwenye hilo, Profesa Mdoe anasema mara nyingi katika utekelezaji wa miradi mikubwa kama huo, wasimamizi wa miradi wanapojiingiza kwenye matumizi mabaya ya madaraka ikiwemo kuingilia michakato ya manunuzi kama ya kwenye ujenzi na manunuzi ya vifaa husababisha ucheleweshaji na wakati mwingine kusimama kwa miradi.

“Kama Wizara hatutafumbia macho kiongozi atakayekiuka maadili ya kazi kwa sababu tu za kutaka kujinufaisha na mradi kinyume na taratibu zilizopo. Niwaambie ukweli, msipokuwa makini katika usimamizi wa utekelezaji wa mradi huu, wengine tutawaona mahabusu, mahakamani na hata magerezani,” alisema.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda anasema mradi huo ni wa miaka mitano, utekelezaji wake ulipaswa kuanza Septemba mwaka jana. Anasema mradi huo unatekelezwa na serikali kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 425 sawa na Sh bilioni 972 ambao ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.

Malengo ya mradi huo anayataja kuwa ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuboresha mitaala ya programu za kipaumbele ili iendane na mahitaji ya soko la ajira na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa elimu juu nchini.

Mradi huo umebainisha programu 14 za fani za vipaumbele vya taifa ambayo ni uhandisi na teknolojia, Tehama, malighafi asilimia za kisayansi, sayansi ya afya, mipango miji, mazingira na teknolojia na nishati jadidivu.

Vilevile rasilimali maji, mabadiliko ya tabianchi, kilimo na kilimo biashara, hifadhi ya wanyamapori, utalii na ukarimu, taaluma ya viwanda na ualimu.

“Wanufaika wa Mradi huu ni vyuo vikuu vyote vya serikali 14, taasisi tatu zinazosimamia elimu na sayansi ambazo ni Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

“Taasisi tano za elimu ya juu zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) pamoja na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA),” anasema.

Anaongeza kuwa asilimia 70 hadi 80 ya fedha za mradi zitatumika katika kuimarisha miundombinu ikiwemo vyumba vya mihadhara na madarasa 130, hosteli 34, kumbi za mikutano ya kisayansi 23, maabara ama karakana za kufundishia 108 pamoja na miundombinu ya shambani na vituo atamizi 10.

Pamoja na kusomesha wahadhiri 623, wanawake 268 na wanaume 355 katika shahada ya uzamivu na wahadhiri 477, wanawake 197 na wanaume 280 katika shahada ya umahiri pamoja na mafunzo ya muda mfupi. “Kupitia mpango huu jumla ya wahadhiri 3,500 wanatarajiwa kupata mafunzo kwa vitendo viwandani ifikapo mwaka 2026.

“Kuhuisha na kuandaa mitaala mipya zaidi ya 290 iendane na mahitaji ya soko la ajira na uchumi wa kati wa viwanda,” anasema. Vilevile kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma programu za kipaumbele kutoka wanafunzi 40,000 kwa mwaka 2020 hadi kufikia 106,000 mwaka 2026.

Akishuhudia utiaji saini huo Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga anasema fedha hizo zitasaidia kujenga vyuo vikuu mikoani ambapo kampasi mpya zitajengwa katika mikoa 17 ambayo ni Lindi ambapo tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam litajengwa huko.

Mikoa mingine ni Ruvuma, Songwe, Rukwa, Simiyu, Kigoma, Tabora, Shinyanga, Singida, Dodoma, Kagera, Mwanza, Tanga, Mara, Manyara na Katavi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2f58398cc4fd47dc9a32baf24b9f3163.png

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi