loader
Utafiti wabaini kizunguzungu cha mbuzi, kondoo tishio Babati

Utafiti wabaini kizunguzungu cha mbuzi, kondoo tishio Babati

UGONJWA wa kizunguzungu cha mbuzi na kondoo husababishwa na mnyoo aina ya tegu kutoka kwa mbwa. Mnyoo tegu ni ule wenye pingilipingili, hupatikana kwenye utumbo mdogo wa mbwa.

Hivi karibuni Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk Jahashi Nzalawahe, alitoa taarifa ya matokeo ya utafiti wa ugonjwa wa kizunguzungu cha mbuzi na kondoo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Katika mkutano huo kulikuwepo na wataalamu wa mifugo, wafugaji, wenyeviti wa vitongoji na kata, watafiti kutoka SUA, maofisa mifugo, madiwani na maofisa kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Dk Nzalawahe aliweka wazi kuwa kwa kiasi kikubwa ugonjwa huo huchangiwa na minyoo tegu ambayo hupatikana kwa mbwa.

Ofisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Gilbert Mbesere alisema katika eneo la Babati kuna mbwa karibia 17,500 lakini wamekuwa wakiendelea kuzaliana kwa wingi na mbwa wengi hufuatana na wafugaji.

Anasema Tarafa ya Mbogwe ni eneo lenye malisho na lina kiwango kikubwa cha ugonjwa huo kutokana na kuambukizwa na kinyesi cha mbwa.

Wakati Mbesere akielezea hayo, Mfugaji Dorcas Bayai kutoka Kijiji cha Minjigu, Kata ya Ngaiti wilayani Babati, Manyara, anasema kwa muda mrefu kata yao imekuwa ikisumbuliwa na ugonjwa huo bila wao kujua ulikuwa ukisababishwa na nini.

 

Anasema kama wafugaji wanapokuwa wakiona mbuzi au kondoo ana dalili za ugonjwa huo humchinja, mara nyingi kwenye kichwa hukuta uvimbe na wadudu, kisha hutoa hilo eneo na kulitupa.

Mfugaji mwingine, Essaya Leboi ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kakoi, Kata ya Ngaiti, anasema ana mbuzi na kondoo wapatao 50, lakini kwa kipindi cha mwaka jana na mwaka huu mpaka sasa wamekufa zaidi ya mbuzi na kondoo 15. Kakoi anakiri kumiliki mbwa wanne ambao huenda nao malishoni.

Hiyo ni mifano michache tu ya wafugaji wa Halmashauri ya Manyara ambao wamekuwa wakisumbuliwa na ugonjwa huo unaosababisha vifo kwa wanyama wao.

Dk Nzalawahe anasema utafiti huo ulioanza mwaka 2019/2020 unabainisha kuwa mbwa ana minyoo tegu hivyo anavyojisaidia kuna pingili za mayai, zinapasuka na kuacha mayai kwenye majani.

“Hizo pingili zina uwezo wa kutembea zinaenda kwenye majani, kisha zinapasuka na kuacha mayai, mbuzi na kondoo wakila maambukizi yanaenda kwenye utumbo, kinatoka mtoto wa mnyoo kinaingia kwenye ubongo au uti wa mgongo,” anasema Dk Nzalawahe.

Anasema mnyoo anapokwenda kwenye ubongo au uti wa mgongo hapo ndipo maambukizi yanapotokea na kusababisha ugonjwa huo wa kizunguzungu.

Kutokana na hali hiyo, anasema elimu inahitajika ili kuzuia maambukizi hayo kwani mbuzi au kondoo anapoonesha dalili za ugonjwa huo, mfugaji humuuza na mnunuzi hununua na kumchinja, anapokutana na uvimbe mwilini kwake hukata sehemu ile na kuitupa, mbwa huila na kusambaza maambukizi tena.

Anataja dalili za ugonjwa huo kuwa ni nyingi lakini baadhi yake ni kuzubaa kwa mnyama, kisha huanza kujitenga na wenzake, kupooza shingo, miguu, mgongo, kuzimia, macho hupofuka na kutafuna meno, mwisho wa dalili hizo ni mnyama kufa.

Ili kudhibiti ugonjwa huo anashauri wafugaji waboreshe ufugaji wa mbwa kwani kwa utafiti walioufanya kila kaya ina mbwa wasiopungua watatu ambao huachwa wakizurura, hawana eneo wala hawapewi chakula bali hujitafutia. Mbwa pia wanapaswa kupewa dawa za minyoo.

Dk Nzalawahe anasema hasara inayopatikana kwa wafugaji na taifa kiuchumi ni kubwa kwani utafiti umebaini kuwa zaidi ya Sh bilioni 2.9 hupotea kutokana na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, kaya moja kwa mwaka inapoteza Sh 356,895. Kaya zilizopo kwenye wilaya hiyo ni 8,333 hivyo fedha hiyo ikizidishwa na kaya hizo inapatikana zaidi ya Sh bilioni mbili kwa mwaka.

Anashauri ili kupunguza hasara hiyo serikali kwa kushirikiana na wafugaji iwe na mpango mkakati endelevu wa kudhibiti ugonjwa wa kizunguzungu kwa kutoa elimu na kusimamia matumizi ya dawa sahihi ya minyoo kwa mbwa.

Anaeleza kuwa kwenye utafiti uliopita ilioneshwa kuwa kukiwa na kundi la ng’ombe, kondoo au mbuzi 100 kati ya hao 20 wanapata maambukizi.

“Bahati mbaya kwa sasa hakuna dawa ya ugonjwa huo,” anasema.

Naye Meneja wa Mfuko wa Kuendeleza Sayansi na Teknolojia kutoka Costech, Ntufye Mwakigonjwa anasema tafiti hizo zinazofanyika zinachangia kwenye sera na mipango ya serikali hivyo alishauri uongozi wa mkoa, wilaya na halmashauri kulichukua hilo kwa umuhimu wake.

 

Anasema mradi huo uliidhinishwa na bodi ya Costech mwaka 2018/2019 hivyo kupitisha Sh milioni 70 katika kutatua changamoto hiyo ya minyoo tegu.

Mwakigonjwa anasema uongozi wa mkoa huo wa Manyara, wilaya na halmashauri waangalie jinsi wanavyolichukua jambo hilo kwa kuwa changamoto iliyopo ni kubwa.

Anasema watafiti wapo kwa ajili ya kuonesha ukubwa wa tatizo uliopo ili liweze kutoa majibu chanya kwa jamii, hivyo anashauri wafugaji kuboresha aina ya ufugaji wao ili kuweza kuondoa hali hiyo.

“Kwenye utafiti huu kuna kitu cha kufanya lazima kichukuliwe kwenye mipango ya serikali,” anasema.

Diwani wa Kata ya Kisangaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira kwenye Halmashauri ya Babati, Adam Ipingika anasema watalichukua hilo na kulipeleka kwenye kamati kisha kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani liweze kufanyiwa kazi.

Naye Diwani wa Kata ya Endakiso, Hasani Omaridodo anasema kuwa kwenye makabila yao ya Wamasai na Wabarbaige, mbuzi anapokufa hula nyama yake kwa kutumia mitishamba.

Ugonjwa huo uliripotiwa kwa wingi mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kusambaa katika maeneo mengi ya Tanzania na kusababisha hasara kwa wafugaji na taifa.

Juhudi za awali za kitafiti kujua kisababishi cha ugonjwa huo zilianza mwaka 2008 hadi 2009 katika Wilaya ya Ngorongoro.

 

Tiba ya ugonjwa huo bado haijapatikana hivyo katika kutafuta njia rahisi na sahihi za kudhibiti maambukizo, watafiti wa magonjwa ya mifugo kutoka SUA waliomba ufadhili wa serikali kupitia Costech.

Utafiti ambao umewahusisha wafugaji wa mbuzi na kondoo wa wilayani Babati ulilenga kuainisha hasara za kiuchumi zinazotokana na ugonjwa huo katika ngazi ya kaya.

Pia kutathmini kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo katika ngazi ya kaya, pamoja na kutathmini maambukizi ya minyoo tegu kwa mbwa inayosababisha ugonjwa husika kwa mbuzi, kondoo na hata binadamu.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ec371acea737d53a0e3f29f34208421f.jpg

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi