loader
Reli ya Tazara kuboreshwa kuwa SGR

Reli ya Tazara kuboreshwa kuwa SGR

TANZANIA na Zambia zimekubaliana kuiboresha Reli ya Tazara kuwa ya kisasa (SGR) kwa kuwa katika dunia ya sasa reli ni SGR, na si vinginevyo.

Hayo yamebainishwa na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu Dar es Salaam wakati akizungumza baada ya mazungumzo yake na mgeni wake, Rais Hakainde Hichilema aliyefanya ziara rasmi ya kikazi jana.

Rais Samia alisema uboreshaji wa reli ya Tazara kuwa SGR pamoja na bomba la kusafirisha mafuta (Tazama), ilikuwa moja ya ajenda zilizopewa kipaumbele kwenye mazungumzo yao ili miundombinu hiyo itumike kama ilivyokusudiwa na waanzilishi wake, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Baba wa Taifa wa Zambia, Kenneth Kaunda.

Alisema kwa sasa Tazara haihudumii vyema nchi hizo mbili, lakini pia jinsi Tazama inavyofanya kazi kwa sasa ni tofauti na lengo la kuanzishwa kwake, hivyo wamekubaliana kutupia jicho kwenye miundombinu hiyo ili ilete manufaa kwa pande zote mbili.

“Tumekubaliana kwamba tuboreshe Tazara kwa kuwa dunia ya leo reli ni SGR, kwa hiyo tumekubaliana tuwe na mradi wa pamoja, tutafute fedha pamoja kupitia ‘PPP’ (Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi) pengine na marafiki zetu waliotujengea reli hii tuone jinsi tutakavyoweza kuiboresha kwenye kiwango cha SGR,” alisema Rais Samia.

Kuhusu bomba la mafuta la Tazama, alisema lengo la kuanzishwa kwa bomba hilo ni kupeleka mafuta kwenye kiwanda cha kusafishia mafuta ndipo yauzwe, lakini lengo hilo kwa sasa limeshuka kwa kiasi kikubwa kiwanda hicho hakitumika kwa kiasi kikubwa.

Kwa mujibu wa Rais Samia, Zambia wamebadilisha sera zao kwenye masuala ya nishati na watakuwa wakiagiza bidhaa za petroli ambazo zimekamilika badala ya mafuta ghafi, hivyo baada ya kupeleka mafuta ghafi, watakuwa wakipeleka mafuta yaliyosafishwa.

“Pia tukakubaliana kuwa bomba lile ni dogo na kuna haja ya kujenga bomba kubwa litakalopeleka mafuta kwa wingi.

Bandari ya Dar es Salaam na vitendea kazi vilivyopo, viwasaidie kupunguza ughali wa mafuta katika nchi yao,” alisema Rais Samia.

Mwaka 2016, Rais mstaafu wa Zambia, Edgar Lungu alipofanya ziara ya kikazi nchini, Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli alisema utendaji wa Tazara umeshuka kutoka usafirishaji wa tani milioni tano za mizigo mwaka 1976 hadi kufikia usafirishaji wa tani 128,000.

Kuhusu utendaji kazi wa bomba la mafuta la Tazama, alisem nao ukishuka kutoka uwezo wa kusafirisha tani milioni 1.1 za mafuta hadi kufikia tani 600,000 kwa mwaka.

Awali, Watanzania walimpokea kwa shangwe Rais Hichilema ikiwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kuja Tanzania katika ziara rasmi ya kikazi tangu aapishwe kuwa Rais wa Zambia, Agosti mwaka jana.

Kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam, ujio wa Rais Hichilema ilitanguliwa na baraka ya mvua mapema jana asubuhi iliyofanya eneo hilo la uwanja wa ndege na maeneo jirani, kuwa na hali ya hewa tulivu, jua la wastani na mawingu ya hapa na pale huku ngoma za asili ikiwamo Kiaso ya Zanzibar, Ngokwa ya JKT Mgulani na matarumbeta zikitumbuiza. Saa 4:43 asubuhi, ndipo ndege ya Rais Hichilema ilipotua kiwanjani hapo na saa 4:52 aliteremka na kukanyaga ardhi ya Tanzania kwa mara ya kwanza akiwa Rais wa Zambia na kupokelewa na mwenyeji wake Rais Samia aliyewaongoza Watanzania katika mapokezi hayo.

Baada ya hapo, marais wote wawili walikwenda moja kwa moja kwenye jukwaa rasmi dogo lililoandaliwa na kupokea heshima ya mizinga 21 huku Nyimbo za Taifa za Tanzania na Zambia zikipigwa.

Baada ya mizinga 21 kupigwa, Rais Hichilema alikagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na baada ya kumaliza kukagua, alirejea tena kwenye jukwaa na Nyimbo za Taifa za nchi hizo mbili zikapigwa.

Baada ya kupokea heshima hiyo ya kijeshi, Rais Hichilema akiongozana na mwenyeji wake walipita kuwasalimu viongozi waliojitokeza kumlaki, kisha kupata burudani kutoka kwa ngoma za asili zilizokuwa zikitumbuiza kiwanjani hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari uwanjani baada ya viongozi hao kuondoka kwenda Ikulu, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omari Kumbilamoto alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuifungua nchi na kufanya wageni wengi kuja nchini.

Kumbilamoto alisema ujio wa Rais Hichilema na ujumbe wake ni fursa muhimu ya kibiashara kwa Jiji la Dar es Salaam yenye bandari inayohudumia siyo tu Watanzania, bali na Wazambia pia.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/7f1237a1038bd58eb8288aabbb797c11.jpeg

Tume Huru ya Uchaguzi na ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi