loader
Mabasi zaidi yatikia tiketi za kieletroniki, muda waongezwa

Mabasi zaidi yatikia tiketi za kieletroniki, muda waongezwa

MKURUGENZI wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Habibu Suluo amesema wamiliki wa mabasi ya masafa marefu wamekuwa na mwitikio mkubwa kuingia kwenye mfumo wa kutoa tiketi kieletroniki.

Amebainisha Julai 26, mwaka huu kulikuwa na mabasi 550 yaliyoanza kutoa tiketi hizo za eletroniki, lakini hadi kufikia Julai 31, jumla ya mabasi 1,432 yaliingia kwenye mfumo huo kati ya mabasi 3,932 yaliyopo kwenye mfumo wa vidhibiti mwendo (VTS).

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Suluo alisema pamoja na kwamba mamlaka hiyo ilitoa muda hadi Julai 31, ndio mwisho kwa mabasi yote kuhakikisha yameingia kwenye mfumo huo wa tiketi za eletroniki, wameamua kuongeza muda wa mwezi mmoja ili kutoa elimu zaidi juu ya suala hilo kabla ya kuchukua hatua.

“Tuliweka wazi kuwa ifikapo Julai 31, tutafanya tathmini ya mabasi yote yaliyoanza na yasiyoanza kutumia mfumo huu. Hatuwezi kuanza tu kutoa adhabu kwa sababu haya ni mabadiliko na mabadiliko ni hatua,” alieleza bosi huyo wa Latra.

Alisema wameshauriana na Wizara ya Fedha na Mipango kutoa elimu kwanza kwa wamiliki kuhusu umuhimu wa kuingia kwenye mfumo huo wa kutoa tiketi za eletroniki na baada ya hapo sasa ndipo wataanza kuchukua adhabu kwa watakaokiuka.

Suluo alisema mfumo huo unasaidia mambo mengi ikiwamo kudhibiti mapato ya wamiliki yaliyokuwa yakiishia kwa watu wao wa kati, abiria kukata tiketi kwa nauli halali, lakini pia kuipatia serikali mapato kupitia kodi.

“Nashukuru suala hili linakwenda vizuri na hawa wenzetu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) wengi sasa wameanza kutuelewa.

Tunatarajia baada ya mwezi mmoja mabasi yote yaingia kwenye mfumo,” alisema Suluo.

Alisema mamlaka hiyo iko kwenye hatua za mwisho za kuzindua programu tumizi itakayoainisha nauli zote zinazotozwa na mabasi ya masafa marefu na daladala nchini kutoka eneo moja kwenda jingine.

“Tunataka Mtanzania awe na uwezo wa kujua nauli ya kutoka Mbagala hadi Temeke ni shilingi ngapi, Dodoma hadi Dar es Salaam ni shilingi ngapi kupitia simu yake ya kiganjani. Tutaanisha nauli hizo kwa kuzingatia madaraja ya mabasi,” alisema.

Aidha, alisema wameanza kufuatilia kwa umakini mabasi yote yanayochezea mfumo wa kudhibiti mwendo na tayari juzi amepokea ripoti inayobainisha namna baadhi ya mabasi yanavyochezea mfumo huo na kuuzima na kuendelea na mwendo kasi.

“Sasa tayari ripoti imelitambua basi moja lililozima mfumo huu na sisi tumelifungia hadi litakapourekebisha. Tuna uwezo wa kulifungia basi lisitembee hata kwa siku 90 kupitia mfumo wetu huu lakini tunaona wataingia hasara hawa wamiliki,” alisema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3d9cbd661d6f943b9a84486f1846ab7b.jpeg

Tume Huru ya Uchaguzi na ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi