MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imewashauri wakulima na wafugaji kutumia huduma za hali ya hewa na taarifa zinazotolewa, ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake kwa ajili ya uzalishaji wenye uhakika wa mazao ya kilimo na mifugo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Agnes Kijazi alisema hayo leo mjini Morogoro, akiwa kwenye banda la mamlaka hiyo katika viwanja vya Nanenane.
Alisema mamlaka imekuwa ikitoa taarifa mahususi kwa ajili ya sekta ya kilimo, hivyo wakulima waweze kuzifuatilia taarifa hizo, ili waweze kutumiza malengo yao ya uzalishaji mazao kwa uhakika .
“ Kwa mfano mkulima akitumia taarifa hii ya siku 10 anajua ni wakati gani aweze kupalilia, wakati wa kunyunyuzia dawa mazao yake,”alisema Dk. Kijazi.
Alisema taarifa hiyo pia inaweza kutumiwa na wafugaji kwa kuwasaidia kujua ndani ya muda wa siku hizo, mvua inaweza kuwa ni kubwa, hivyo kujiwekea malisho ndani kwa ajili ya kulishia mifugo, kujua ukame wa muda mrefu, ili waweze kupunguza malisho.
Alisema mamlaka itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ya namna bora ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake.