loader
SMZ yafungua milango uwekezaji mafuta, gesi

SMZ yafungua milango uwekezaji mafuta, gesi

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema milango ya uwekezaji iko wazi katika sekta ya nishati hasa mafuta na gesi. Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah alisema hayo wakati akifunga Kongamano la Nne la Kimataifa la Nishati lililofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 3 na 4, mwaka huu.

Abdullah alisema kampuni nyingi kubwa zimeshiriki katika kongamano hilo kubwa na Zanzibar imekwisha fungua milango ya uwekezaji kwa wadau mbalimbali wa sekta ya nishati. Aliweka wazi kuwa serikali iko tayari kwa mazungumzo na wawekezaji wa kampuni ya aina yoyote iliyo tayari kuwekeza Zanzibar hususani katika mafuta na gesi kwa maslahi ya serikali, wananchi pamoja na mwekezaji husika.

Alisema serikali imepiga hatua kubwa katika sekta ya mafuta na gesi hivyo wawekezaji wanakaribishwa kutekeleza miradi iliyobainika. “Kongamano hili kubwa limefungua milango na kuongeza fursa zaidi za uwekezaji kwa nchi yetu, kwani wawekezaji walioshiriki katika kongamano hili wamefahamishwa juu ya fursa zilizopo kwa upande wa Tanzania Bara na pia Zanzibar,” alisema.

Alisisitiza: “Hivyo waje tuzungumze katika masuala ya uchimbaji wa mafuta au ufuatiliaji wa miradi mingine kwa maslahi ya pande zote mbili.” Aliipongeza Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wadau wengine kuandaa na kufanikisha kongamano hilo lililowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya nishati, zikiwamo kampuni kubwa zaidi ya 80.

Alisema mwitikio mkubwa wa washiriki katika kongamano hilo kutoka maeneo mbalimbali duniani ni matokeo ya ziara za Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kutembelea nchi na kampuni kubwa na kufanya nazo mazungumzo ya kutangaza fursa zilizopo nchini. Aliwataka waandishi wa habari kutumia vyema kalamu zao kuhabarisha umma na nje ya nchi mambo mazuri yanayotokea Tanzania kama walivyotangaza kongamano hilo.

Licha ya kongamano hilo, Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imesaini makubaliano ya kuendeleza mradi wa nishati jadidifu na Kampuni ya Masdar inayomilikiwa na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Akizungumza wakati wa utiaji saini, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema makubaliano hayo ni matunda ya ziara ya Rais Samia aliyoifanya nchini humo mwaka huu.

Alisema utekelezaji wa makubaliano ya miradi hiyo utafanyika kwa awamu mbalimbali kwa lengo la kuzalisha hadi megawati 2000 za umeme jua nchini. Mkuu wa Uendelezaji wa Biashara na Uwekezaji wa Masdar, Abdullah Zayed alisema miradi iliyopo katika makubaliano hayo, uendelezaji wake unategemea kufikia megawati 5000 kufikia mwaka 2025.

Katika kongamano hilo, wataalamu kutoka Wizara ya Nishati waliwasilisha mada kuhusu maendeleo ya sekta ya nishati nchini na ushiriki wa wahandisi wanawake katika nafasi za uongozi hasa katika sekta ya nishati.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6cfc3ba37056a99210a2842139b9dbd6.jpeg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi