loader
CCM yashitukia upinzani kupenyeza wagombea

CCM yashitukia upinzani kupenyeza wagombea

CHAMA cha ACT-Wazalendo kinadaiwa kupenyeza wanachama wake kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye ngazi za kata, matawi na wilaya.

CCM imekionya chama hicho kufanya hivyo kwa kile kinachosadikiwa kuwa ni kwa lengo la kunasa siri na mikakati yake kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Yassin Mtalikwa alibainisha hayo akitoa taarifa ya hali ya chama kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Christina Mndeme anayefanya ziara mkoani Kigoma.

Mtalikwa alisema kuwa baada ya kubaini njama hizo za wanachama wa chama hicho cha upinzani kujipenyeza kugombea nafasi za uongozi ndani ya CCM, walichukua hatua kuhakikisha hakuna mgombea atakayepitishwa au kushinda kwenye uchaguzi bila kuwa mwanachama halisi.

Akizungumzia taarifa hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Mndeme aliwataka viongozi na wanachama kutokumbatia mamluki wenye nia ya kudhoofisha juhudi za chama hasa kwenye uchaguzi badala yake wawe kitu kimoja. Mndeme alisema ni lazima viongozi na wanachama washikamane wawe kitu kimoja, wapige vita aina zote za njama zenye lengo la kuwadhoofisha. Wakati huo huo alionya vitendo vya kutolewa kwa siri za vikao na za chama hicho akisema ni sumu kubwa kwa maendeleo yao.

“Hapa Kigoma kuna watu mchana wana kijani usiku wana nyekundu ni hatari sana hiyo, hawa ni mamluki msiwape nafasi, shikamaneni muwe kitu kimoja na kuwapiga vita hawa mamluki,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu shutuma dhidi ya chama chake, Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Mkoa wa Kigoma, Ibrahim Sendwe alisema: “Huko ni kutapatapa kwa baadhi ya wagombea ndani ya CCM ambao hawana uwezo kushindana. Badala yake wanataka kubebwa na huruma za wajumbe.” Sendwe alisema wao kama chama kikubwa cha upinzani, kusemwa kwenye vikao vya CCM ni lazima. Alisema inadhihirisha ipo dhamira ya baadhi ya viongozi kuwakata wagombea wao kwa madai ya usaliti.

Alisema hatua hiyo inatokana na baadhi ya viongozi kulenga kuwaengua wagombea wenye nguvu ambao si kambi yao kwa madai kwamba ni wapinzani au wasaliti.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/381956a53da53f46bb5f8191cec46746.jpeg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Na Fadhili Abdallah, Kigoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi