loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Abiria wasaidie kuzuia ajali za barabarani

Katika ajali ya mkoani Dodoma basi la abiria la Morobest liligongana na lori la mizigo katika Kijiji cha Pandambili wilayani Kongwa na kusababisha vifo vya watu 17 huku wengine 56 wakijeruhiwa.

Aidha, katika ajali ya Arusha, madereva wa magari mawili yaliyogongana maeneo ya Sadeki wilayani Arumeru walikufa na watu wengine 14 walijeruhiwa. Ajali ya mkoani Dodoma ilihusisha basi hilo la Morobest lililokuwa likitoka Mpwapwa kwenda Dar es Salaam.

Basi hilo ni lenye namba T 258 AHV na lori lenye namba T 820 CKU, likitoka Dar es Salaam kwenda Dodoma. Kwetu sisi tunayachukulia matukio haya ya ajali kama matukio mabaya kutokana na kusababisha vifo vya watu 19, ambao kwa namna yoyote ile walikuwa wakitegemewa na familia zao sasa na hapo baadaye.

Hivyo basi kwa kutumia safu hii, tunapenda kutoa salamu za pole kwa ndugu na jamaa waliothiriwa kwa namna yoyote ile na ajali hizo huku tukimuomba Mungu kuwaweka mahala pema peponi marehemu wote na kuwajalia uponyaji wa mapema majeruhi wote wa ajali hizo.

Hata hivyo wakati ajali za barabarani zikizidi kuongezeka, lipo jambo ambalo tunadhani ni lazima jamii ya Watanzania hasa abiria wanaosafiri kwenda maeneo mbalimbali wakaanza kujifunza; nalo si lingine bali la kugeuka kuwa askari wa usalama barabarani wao wenyewe bila kusubiri wale wa Jeshi la Polisi.

Tunasema hivyo tukiamini kuwa endapo abiria wao wenyewe wataamua kuchukua majukumu ya kulinda usalama wa maisha na mali zao wao wenyewe, madereva ambao kutokana na uzembe wamekuwa wakisababisha ajali za mara kwa mara wataweza kudhibitika kirahisi kuliko ilivyo sasa.

Ni jambo la kawaida kabisa kwa madereva wa mabasi ya abiria kuendesha kwa mwendo wa kasi maeneo wanayojua kuwa hakuna askari wa usalama wa barabarani lakini wanapofika maeneo ambayo askari hao wameweka vizuizi hupunguza kabisa mwendo wa magari, ujanja ambao mwishoni husababisha maafa.

Ingawa katika ajali ya Dodoma, dereva wa lori ndio mwenye makosa kulingana na taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime kwa kulipita gari lingine bila kuchukua tahadhari ya magari yanayokuja mbele, lakini zipo ajali ambazo madereva wa mabasi wenyewe huwa chanzo.

Ni matumaini yetu kwamba abiria na wananchi wengine watatoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ambalo sasa linachukua hatua mbalimbali za kuwahusisha abiria katika udhibiti wa usalama barabarani, ili kuhakikisha kuwa lengo hilo linafanikiwa na kusaidia kupunguza ajali za barabarani.

Ni vema pia wasafiri wanapofika maeneo yenye askari wa usalama barabarani wanaotoa maelekezo kuhusu hatua za kuchukua wanapoona madereva wanakiuka sheria za usalama barabarani, wakayasikiliza kwa makini maelekezo hayo na kuyafanyia kazi badala ya kuyasikiliza na kuyapuuza.

Ni imani yetu kwamba kama kila mmoja atatimiza wajibu wake, bila shaka tutakuwa na usafiri barabarani ulio salama, hatua ambayo itamwezesha kila mmoja wetu kuyafikia malengo ya maisha aliyojiwekea kwa kuepukana na ajali ambazo mara nyingi husababishwa na uzembe wa madereva.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi