loader
Dstv Habarileo  Mobile
ALLY SALEH KIBA: Soko la muziki limevamiwa

ALLY SALEH KIBA: Soko la muziki limevamiwa

Hiyo ni kauli ya msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ally Salehe Kiba maarufu Ally Kiba. Bila kutaja ni watu gani hao, kwa mtizamo na fikra zake anawafahamu ni akina nani. Msanii huyu alipotea katika soko la muziki kwa miaka mitatu akiangalia namna soko linapoelekea na wakati huo akiendelea kuwa shabiki wa muziki wa wasanii wenzake.

Baada ya kipindi chote alichokaa nyumbani akitafakari atoke vipi, amekuja na kudondosha nyimbo mbili mpya ya Mwana na Kimasomaso ambazo zinaendelea kuchezwa na kufanya vizuri katika vituo mbalimbali vya redio nchini. Lakini wakati akitambulisha nyimbo zake hizo, anasema soko limeingiliwa kiasi cha kuwakatisha tamaa baadhi ya wasanii wenzake kushindwa kusonga mbele kimuziki.

Anasema kuna watu wamekatishwa tamaa sababu ya fitna za watu hao na mwishoni wamerudi nyuma. Kiba anasema kwa upande wake hawezi kurudi nyuma kwa vile muziki ndio maisha yake, isipokuwa ukimya wake alikuwa akiangalia aje vipi kuwafurahisha mashabiki wa muziki.

Msanii huyu licha ya kukaa nyumbani kwa muda, muziki wake umekuwa ukikubalika na kuendelea kufanya vizuri katika nchi mbalimbali kiasi cha kualikwa kwenda kufanya shoo. Aidha, mashabiki wa Tanzania kupitia mitandao ya kijamii walikuwa wakijiuliza msanii huyo amepotelea wapi, wengine wakimtaka arejee tena kwa vile hufurahia nyimbo zake na jinsi anavyoimba.

“Nimerudi kwa sababu nimehamasika jinsi ambavyo mashabiki wamekuwa wakinihitaji kila wakati, na wengine wakitoa maoni kwenye vyombo vya habari wanataka kuniona nikija, inaonesha kwamba kazi zangu haziwezi kufa kutokana na ubora,” anasema Kiba. Anasema mashabiki hao wamemwomba asikae muda mrefu kama alivyofanya siku chache zilizopita, na badala yake aendelee kutoa muziki mzuri watamuunga mkono.

Albamu yake ya mwisho ilikuwa inaitwa My Everything aliyoitoa mwaka 2011 na kufanikiwa kufanya vizuri. Baadhi ya nyimbo zilizompandisha zaidi ni Dushelele, Cinderela ambayo ilivunja rekodi kwa kuuza nakala nyingi kuliko nyimbo zake zote. Dushelele pia ilitingisha Afrika Mashariki na Kati na kufanikiwa kushinda Tuzo za Muziki za Kilimanjaro mwaka 2012.

Ili kurudi katika kiwango chake cha zamani, anasema amejipanga na ataendelea kuwapa mashabiki burudani nzuri kwa kuimba muziki utakaofanya vizuri nje ya Tanzania. Anasema kuna nyimbo nyingine ameziandaa na ataziachia siku za karibuni baada ya nyimbo zake za Mwana na Kimasomaso kufanya vizuri.

Katika wimbo wake wa Kimasomaso ambao ni kopi ya gwiji wa taarabu, Issa Matola, anasema ameuimba kisasa kwa ajili ya kuleta ladha tofauti. Kitendo cha kuchukua wimbo huo wa zamani na kuubadilisha kwa kuimba kwa mtindo wa kisasa, ni kuonesha wazi kwamba anaenzi muziki wa zamani, ukiwa na ujumbe ambao ni wa kuelimisha.

Ni kama mduara ukiusikiliza, lakini amejaribu kwa uwezo wake, na amefanikiwa ingawa wimbo wa Mwana unaonekana ni mkali zaidi katika mapigo na hata ujumbe wenye kuelimisha jamii. Wimbo huo wa Mwana umejaribu kuzungumzia maisha ya mtoto wa kitajiri anayejiingiza katika starehe na kukutana na mitihani ya kimaisha.

Zaidi kama haujawahi kuusikia ni kama ufanane na Dushelele kwa mapigo yanayovutia kucheza. Ni kweli Kiba ana ugomvi na Diamond? Hakika siku za karibuni kumekuwa na taarifa kwamba Ally Kiba haelewani na msanii mwenzake, Nassib Abdul maarufu kama Diamond Platnum.Suala hilo Kiba analikanusha kuwa sio kweli na kwamba hana msanii yeyote anayemchukia.

Licha ya kukanusha hayo, katika nukuu zake kwenye vyombo vya habari siku zilizopita, ilidaiwa kuwa Diamond hapatani na Kiba kutokana na taarifa kwamba aliwahi kushirikishwa na Diamond kwenye muziki, lakini baadaye Diamond akafuta kile kipande alichoingiza Kiba.

Wakati huo, Diamond ndio alikuwa ameanza kung’ara tofauti na sasa ambapo nyota yake imezidi kumpaisha kutokana na kukubalika haraka ndani na nje na hivyo, kuonekana kumfunika Kiba. Aidha, taarifa nyingine zilikuwa zinasema kuwa Kiba aliwahi kusema kuwa Diamond anasafiria nyota yake.

Hayo yote yalizungumzwa na kujadiliwa kwenye mitandao ya kijamii, lakini pamoja na kukanusha, bado inaonesha wazi hakuna mawasiliano mazuri kati yao. Katika akili zangu ndogo nimegundua kuwa wasanii wote wawili ni wakali na kila mmoja anajiona yuko juu ya mwenzake, hakuna anayetaka kushindwa. Kitendo cha kila mmoja kujiona ni bora kuliko mwenzake siku zote huwa kinasababisha matatizo.

Jambo la muhimu kwa maendeleo ya muziki wao ni kupatana na kufanya muziki pamoja. Ukiachilia hayo, Kiba kwa sasa ni baba wa watoto watatu kwa wazazi tofauti, lakini hajaoa wala kuweka bayana mke wake mtarajiwa atakuwa ni nani, licha ya kuwepo kwa taarifa kadhaa za kujihusisha kimapenzi na baadhi ya nyota wa muziki nchini.

Jambo kubwa analojivunia ni kufanya kazi na wasanii wa kimataifa hasa katika mradi ule wa msanii wa Marekani, R. Kelly na kuunda Kundi la One 8, na kufanikiwa kutoa wimbo wa pamoja. Pia anajivunia kuendelea kukubalika kwa mashabiki na muziki kiasi cha kumuulizia na kumtaka kurudi tena jukwaani.

“TUNALIMA, tunavuna sana kuliko kawaida, unaweza ukajikuta unauza ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi