loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Amani itawale kipindi chote cha Pasaka

Pasaka kama zilivyo sikukuu nyingine za kidini huadhimishwa kila mwaka mara moja, ili kuwakutanisha Wakristo karibu na Mungu wakitumia muda huo, kutafakari upya fumbo la ukombozi.

Siku hii ni ya furaha baada ya kumalizika siku 40 za mfungo wa Kwaresima, ambazo humpa muumini muda wa kufanya tafakari na kutubu dhambi zake.

Tunaamini katika mfungo wa Kwaresima, umewapa watu muda wa kutosha, kufanya tafakari juu ya maisha yao na ikiwezekana kuachana na mwenendo mbaya, usiompendeza Mungu na jamii.

Imani hiyo inatokana na mafunzo mbalimbali, waliyokuwa wakiyapata waumini kutoka kwa viongozi wa dini wakati wote wa mfungo na hivi sasa tunasubiri kuona utekelezaji wa mafunzo ya viongozi wa dini.

Tunatarajia kuona `kuzaliwa’ upya kiroho kwa watu wengi, mabadiliko ambayo yatasaidia binadamu kujitambua na kujikita katika kufanya shughuli halali na za kimaendeleo ili waweze kujikwamua kiuchumi na pia kulisaidia taifa kujiimarisha kiuchumi.

Hatutarajii kuendelea kusikia juu ya matukio ya mara kwa mara ya mauaji ya albino, wizi, ufisadi, rushwa, ushirikina, uongo, mauaji na matendo mbalimbali, ambayo yamekuwa yakimchukiza Mungu, bali yale yenye mwenendo mzuri kwa jamii, kiasi cha kuifanya jamii ya Watanzania iwe yenye furaha, amani na utulivu.

Na pengine kwa kuanzia, tuanze na hili la amani na usalama wa kutosha, mambo ambayo kwa ujumla ndiyo yanayoweka mazingira mazuri ya ustawi kuanzia ngazi ya familia na hata taifa.

Wananchi wenyewe tunaweza kuwa mstari wa mbele, kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha Pasaka inaadhimishwa katika mazingira ya amani na utulivu.

Uzoefu unaonesha kuwa wahalifu mara nyingi hutumia fursa ya sikukuu, kufanya vitendo vya uhalifu vikiwamo vya uporaji. Lakini, kwa bahati mbaya ni kwamba, jamii inachangia kwa kuwaficha wahalifu husika.

Badala ya kuendelea na utamaduni huo, ni vyema tukatoa taarifa kwa Jeshi la Polisi juu ya jambo lolote, linaloashiria uvunjifu wa amani na usalama wa raia na mali zao kwa ujumla.

Ndiyo maana tunashauri Pasaka yenye utulivu na amani, isiyo na matukio ya kikatili dhidi ya watoto, wanawake na viongozi wa dini.

Inawezekana ili mradi tu kila mmoja atimize wajibu wake katika kuhakikisha amani inatawala katika kipindi chote cha Sikukuu ya Pasaka. Tunawatakia Pasaka njema.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi