loader
Dstv Habarileo  Mobile
AMAWAWA yajipanga kuinua kilimo Rukwa

AMAWAWA yajipanga kuinua kilimo Rukwa

Kwa kulitambua hilo na kulipa uzito wa kipekee serikali imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali kuhakikisha kilimo kinaendelea kuwa mkombozi wa Watanzania. Wadau mbalimbali nao wamekuwa wakijitahidi kushiriki katika mikakati hiyo kulingana na fursa zinazoruhusu. Kwa mkoani Rukwa kilimo pia ni msingi mkuu wa ajira kwa wakazi wake.

Vijana wengi wanaohitimu elimu ya msingi na sekondari wamekuwa wakijiajiri kupitia kilimo. Pamoja na changamoto ya uhaba wa soko la mazao wanayozalisha wapo walioweza kupata mafanikio kupitia kilimo. Wapo walioweza kujenga nyumba bora na wengine kuweza kumudu gharama za kusomesha watoto wao katika shule na vyuo mbalimbali.

Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto ambazo zimekuwa zikiikabili sekta hii yenye kutoa ajira kwa wakazi wengi mkoani hapa. Wakulima wengi bado wanalima kwa mfumo wa mazoea uliokuwa ukitumika tangu enzi za mababu. Mfumo huu kwa sasa hauna tija tena katika kilimo cha leo.

Hii imekuwa ikiwasababishia wakulima hasara kwa kushindwa kuzalisha ipasavyo huku wakiwa wametumia mtaji mkubwa. Kipo pia kilimo kinachoambatana na uharibifu mkubwa wa mazingira. Ni kutokana na changamoto hizi baadhi ya wadau waliona umuhimu wa kuwepo kwa chombo kitakachosaidia kutoa mwamko kwa wakulima.

Ndipo ikaundwa Asasi ya Maendeleo ya Wakulima na Wafugaji wadogo (AMAWAWA) mnamo mwaka 2009 na hatimaye mwaka mmoja baadae ikasajiliwa. Lengo la kuanzishwa kwa Amawawa ni kuwawezesha wakulima na wafugaji wadogo kuwa na nguvu ya pamoja.

Waweze kuwa na sauti ya pamoja ya kutetea na kutatua changamoto zinazowakabili ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikikwamisha jitihada zao za kupiga hatua kimaendeleo kupitia shughuli zao za kiuchumi.

Hata hivyo kutokana na unyeti wa jambo husika, kupitia asasi hii waanzilishi wake wakaona jambo la kwanza na muhimu kufanikisha lengo la kuanzisha kwake ni kuwa na kituo cha kutoa elimu ya kilimo na ufugaji wa kisasa kwa vitendo na si kuishia kuzungumza kama wanavyofanya wadau wengi wa kilimo.

Wengi wamekuwa wakiishia kupiga porojo majukwaani na utekelezaji wao kuishia kwenye makabrasha na vipeperushi. Katibu wa Amawawa, Petro Milambo anasema walengwa wakuu wa kituo hiki ni vijana. Hao ndio watakaonufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa kituo hicho kilichopo nje kidogo ya manispaa ya Sumbawanga. Kwa kupata mafunzo ya kilimo na ufugaji wa kisasa wataweza kuona umuhimu wa kujiajiri kupitia shughuli hizo.

Milambo anasema vijana wengi wamekuwa wakivikimbia vijiji vyao na kwenda mijini wakiamini huko kuna unafuu mkubwa wa upatikanaji wa ajira. Lakini matokeo yake huko mijini wamekuwa wakijikuta wanaingia kwenye makundi ya vijana yenye kujihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu.

“Vijana wengi wamekuwa na imani potofu kuwa mijini pekee ndiko wanakoweza kupata mafanikio ya haraka. Lakini hii yote ni kutokana na kilimo kuonekana hakiwaletei tija vijijini kwao. Huko mijini matokeo yake imekuwa ni kujiunga na vikundi vinavyofanya mambo maovu kama wizi na matumizi ya dawa za kulevya.” “Lakini wanakimbia kilimo kwa kuwa hawaoni kama kinaweza kuwaajiri.

Tukiwapa elimu tutawahamasisha kulima na kufuga kwa njia za kisasa ni dhahiri wataweza kujiajiri wakiwa vijijini kwao. Kamwe hawatatamani kwenda mijini kwa kuwa tayari wamekwishaona mifano ya wenzao waliokwenda huko na hawakupata mafanikio. Badala yake walirudi wakiwa wameharibikiwa baadhi yao wakiwa wagongwa baada ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi,” alisema Milambo.

Alisema kwa vijana kunufaika na ajira za kilimo na ufugaji wa kisasa wakiwa vijijini kwao kutawezesha hata wenzao waliokimbia kurudi na kuungana nao ili kwa pamoja waweze kuunganisha nguvu kwenye shughuli hizo. Kwa sasa vijana wengi wanakimbilia mjini na kuiacha sekta ya kilimo bila nguvu kazi kwani wazee wao ndio wanaobaki wakijihusisha na shughuli hiyo.

“Kwa hapa kituoni vijana ambao watakuwa wakija kupata mafunzo hapa kwa vitendo wataweza kujifunza mambo mbalimbali. Tayari tuna ng’ombe na mbuzi hapa nah ii yote ni maandalizi ya kuanza kutoa mafunzo ambapo tunataraji mwaka 2014 tunaweza tukaanza. Wakazi wa vijiji vinavyotuzunguka tunaamini watakuwa wa kwanza kunufaika na mafunzo.” “Watajifunza kilimo cha matunda na mboga kama unavyojua mkoa wa Rukwa hamasa ya kilimo cha matunda bado ni ndogo ikilinganishwa na mikoa jirani kama Mbeya.

Lakini kilimo cha matunda kina manufaa makubwa mno.” “Tukidhamiria kwa dhati kujikita katika kilimo hiki vijana wanaweza kujikuta wanapata mafanikio kwa muda mfupi sana na umasikini unaowasumbua kwa sasa ukabaki katika historia. Matunda kama mapera na matunda jiwe yanastawi sana mkoani hapa lakini hayalimwi kwa malengo.” “Lakini pia kilimo cha mboga kinachofanyika mkoani hapa ni cha kizamani.

Wakulima hawalimi kwa matarajio makubwa na kuona kama kinaweza kuwasaidia kunyanyuka kimaendeleo na jamii ikabaki inashangaa. Tunatambua kuna tatizo la miundombinu hasa ya kilimo cha umwagiliaji lakini tunaamini serikali nayo itakapoona tunafanya hili pia itaanza kujipanga kuwasaidia vijana wanapotoka hapa kwetu,” anasema.

Katibu huyo wa Amawawa anafafanua kuwa ufugaji wa kisasa wa sungura, nguruwe, kuku, mbuzi na ndezi panya pia vijana watafundishwa. Hiyo yote itakuwa miradi yenye kuleta kumwingizia kipato kijana mmoja mmoja au wakiwa katika kikundi. Kijana ama kikundi kikilima mchicha wakati huo huo kikawa na ng’ombe wa maziwa au mbuzi na pia mifugo mingine midogomidogo hatoweza kukosa fedha.

Ufugaji wa nyuki na samaki ni mafunzo mengine yatakayotolewa kituoni hapo kwa vijana. Ufugaji huu utawezesha kwa kiasi kikubwa utunzaji wa mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa yameharibiwa na kilimo cha mfumo wa kizamani miti na misitu mingi imefyekwa ili kupata mashamba ya kulima.

Lakini pia upo uchomaji moto wa mapori kwa ajili ya baadhi ya watu kutafuta wanyama wadogo wa porini kwa ajili ya kitoweo. Kwa kufuga samaki na nyuki kwa njia za kisasa vitoweo vitapatikana kwa urahisi na vijana watajiingizia vipato kwa kuuza samaki, asali na pia nta kutokana na mazao hayo kuwa na soko zuri.

Hii pia itasaidia kutunzwa kwa mazingira kwa kutochomwa moto misitu na kufyekwa hovyo miti. “Yapo mambo mengi mazuri ambayo vijana wakiwa hapa watajifunza. Na tunataka wakitoka hapa waone kuwa awali walikuwa wakicheza mijiji na waweze kujipanga kuanza maisha upya wakitaraji neema kwa wakati mfupi. Lini hatutoishia kutoa elimu kwa vijana watakaofika kituoni hapa pekee.

Tunataka pia wakulima wawe wanapanga ziara za kimafunzo na kuja hapa kujifunza wakaondoka.” Anasema upatikanaji wa vijana watakaojiunga na kituo hicho hawatatozwa ada badala yake mchango wao utakuwa nguvu kazi kwa kufanya shughuli za uzalishaji wakati wakiwa kituoni hapo ambapo watakula na kulala pia. Kata ndizo zitaachiwa jukumu la kupendekeza vijana kwa ajili ya kujiunga na kituo.

Akizungumzia maandalizi ya miundombinu kituoni hapo, Milambo alisema tayari wameweza kujenga jengo la utawala na pia jengo kwa ajili ya bweni la vijana. Yapo maji ya mserereko takribani umbali wa mita 600 ambapo kituo kinataraji kutega na kuyavuta hadi kituoni hapo kwa ajili ya matumizi ya kilimo.

“Tayari tunayo mabwawa tisa ya kuchimbwa kwenye eneo letu hili la kituo lililo na jumla ya ekari 15 japo tabia ya nchi nayo ni changamoto kwani asilimia kubwa ya mabwawa yetu yanaonekana kukauka lakini hali itakuwa nzuri baada ya kuvuta maji ya mserereko. Kwa sasa bado kukamilisha vyumba kwaajili ya kulala na vyoo.Lakini mabanda ya ng’ombe na mbuzi yako tayari,”.

Anasema wakulima pia wataweza kukitumia kituo hicho kupata habari za masoko ya mazao wanayozalisha na pia kituo kitabeba jukumu la kuwaunganisha na wateja mbalimbali hivyo hata vijana watakaohitimu kituoni hapo na kwenda kuzalisha hawatokuwa na tatizo katika kupata masoko ya mazao watakayozalisha.

Hata hivyo, anaitaja changamoto ya uhaba wa fedha kuwa kikwazo kingine kwa kuwa hadi hatua waliyofikia hakuna mfadhili mkubwa aliyejitokeza licha ya serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kuahidi kushirikiana kwa karibu na asasi hiyo kupitia kituo hicho.

Alisema fedha zinazotumika ni michango kutoka kwa wanachama wa asasi hiyo hali iliyopelekea baadhi yao kukimbia kutokana na michango ya kila siku. Awali walikuwa 30 lakini sasa wamebakia 15 pekee.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi