Azam iliyocheza kwenye Uwanja wa Azam Complex ilirejea kileleni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0. Azam na Mbeya City zote zimefikisha pointi 26 dhidi ya pointi 25 za Yanga. Mabao ya Azam jana yalifungwa na Kipre Tchetche,Joseph Kimwaga na Khamis Mcha 'Viali'.
Hata hivyo, pamoja na kipigo hicho, Ruvu Shooting iliyo chini ya kocha Charles Mkwasa, ndiyo iliyotawala mchezo hasa katika kipindi cha kwanza, hali iliyomfanya kipa wa Azam Mwadini Ally kuokoa hatari mara kwa mara langoni mwake.
Kutoka kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wenyeji Mbeya City waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wageni wao Ashanti. Bao hilo lilipatikana baada ya beki wa Ashanti kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa.
Kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga, Coastal Union na Mgambo Shooting za huko zilitoka suluhu huku Mtibwa Sugar ikiifunga Rhino mabao 2-0 katika mechi nyingine iliyochezwa kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani.
Ligi hiyo inaendelea tena leo kwa mechi moja ambapo Prisons itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine kumenyana na JKT Oljoro.
Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo unatarajiwa kukamilika Novemba 6 na 7 kwa JKT Ruvu kumenyana na Coastal Union, Ashanti United itacheza na Simba, Kagera Sugar itakuwa mwenyeji wa Mgambo Shooting, na Ruvu Shooting itacheza na Mtibwa Sugar.
Mechi nyingine itakuwa kati ya Azam na Mbeya City , Yanga na JKT Oljoro na Rhino itacheza na Prisons ya Mbeya.