Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu suala la Yanga na Azam Tv, kama wamekubaliana kurusha mechi zao, Mwakibinga alisema hawajakubaliana wala Yanga kulipwa chochote hadi watakaporidhia isipokuwa utaratibu uliokuwepo awali utaendelea.
Alisema wamezungumza na Polisi ili kuwa na ulinzi mkali kwa ajili ya Azam Tv, na ikiwa kuna mashabiki wa Yanga wataleta vurugu ili mechi yao isioneshwe, watachukuliwa hatua kulingana na sheria za nchi.
“Tulishakubaliana hatutaweza kurudi nyuma, Azam wataendelea na utaratibu wao kama kawaida wa kurusha moja kwa moja, na ikiwa kuna atakayesababisha vurugu watachukuliwa sheria,” alisema Mwakibinga.
Alisema kwa vile timu 13 zilikubali, tayari zililipwa kila moja Sh milioni 75 na nyingine zitamaliziwa ila kwa Yanga itaendelea kusubiri hadi wamalizane.
Alisema jambo la kufurahisha ni kuona kwamba Yanga wamefungua mlango kuwaruhusu Azam kufanya mazungumzo nao kwa ajili ya kukubaliana hivyo wanasubiri wamalizane.