loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Azimio la Bunge la EAC na mjadala ‘mpya’ wa hotuba ya Rais

Kutengwa huko kunatokana na nchi ya Kenya, Uganda na Rwanda kufanya mikutano ya kujadili mambo yanayogusa ushirikiano wa EAC bila kuishirikisha Tanzania.

Nchi nyingine ambayo haishirikishwi katika masuala hayo ni Burundi. Katika mkutano huu wa Bunge, pamoja na mambo mengine Bunge litajadili kwa kina hotuba ya Rais Kikwete kuhusu EAC aliyoitoa bungeni Novemba 7 mwaka huu ambayo si wabunge pekee bali wasomi na wananchi wengi waliipongeza hasa msimamo wake wa Tanzania kutojitoa katika Jumuiya hiyo.

Msimamo wa Rais Kikwete pia ulizingatia umuhimu wa umoja ambapo yeye kama kiongozi mkuu mwenye dhamana ya Taifa hili, alieleza wazi kwamba Tanzania haipo tayari kunyooshewa vidole kuwa sababu ya kuvunjika kwa jumuiya hiyo kwa kuwa nchi ina sifa na historia nzuri ya kusababisha muungano badala ya utengano.

Kikwete katika hotuba yake alitolea mfano wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Taifa moja la Tanzania kwamba ni moja ya ishara njema kwa Bara la Afrika na dunia nzima kuhusu muungano, hivyo matamanio ya nchi ni kuona Afrika inakuwa kitu kimoja katika maeneo inayokubaliana badala ya kutengana.

Ingawa Rais Kikwete alionesha wazi kwa sura, vitendo na kauli kwamba haelewi kwanini baadhi ya wakuu wa nchi wanachama wa EAC wanaitenga Tanzania katika mambo fulani fulani yanayogusa makubaliano ya ushirikiano uliopo na kufunga mjadala kwa kusema kwamba watatafuta kujua kulikoni lakini kamwe Tanzania haifikirii wala haitajitoa EAC.

Siku mbili baada ya hotuba hiyo iliyokonga nyoyo za Watanzania wengi kama sio wote, Bunge lilipitisha Azimio la kupongeza tamko la Rais Kikwete kuhusu msimamo wa Tanzania kwenye EAC na kumuelezea Rais kama kiongozi mwenye ukomavu mkubwa wa kidiplomasia na uongozi.

Aidha, azimio hilo lilimuunga mkono Rais Kikwete kuwa, Tanzania isijitoe kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwataka watu wa Afrika Mashariki kuilinda na kuitetea Jumuiya hiyo kwa nguvu zote na kuweka pembeni tofauti za kimitazamo ili kuiimarisha jumuiya hiyo.

Azimio hilo liwasilishwa bungeni na Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na ile ya Ulinzi na Usalama na lilisomwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Kamati hizo mbili chini ya Kanuni ya 54 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili 2013, ziliwasilisha bungeni azimio hilo na kueleza tamko la Rais Kikwete limeongeza ubora wa Tanzania kwa mataifa ya nje na kazi na wajibu wa Tanzania wa awali na sasa wa kuwa kiini cha kuunganisha nchi na si kuzitenganisha. Lowassa, awali wakati jambo hilo lilipoibuka bungeni, hakushauri Tanzania ijitoe, lakini alipendekeza ikiwa Kenya, Uganda na Rwanda zimejitenga hakuna haja ya kulumbana nao badala yake Tanzania iangalie upande mwingine kwa kuzishirikisha nchi kama Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako kwa mujibu wa Lowassa alisema ni kuzuri zaidi.

Hakuwa Lowassa pekee aliyelitazama hilo kwa namna hiyo, bali wabunge kadhaa walizungumzia hilo kwa mitazamo yao kabla ya hotuba ya Rais Kikwete huku wengine wakishauri Tanzania ijitoe kabisa huku wengi wakieleza suluhisho si kujitoa bali kutafuta sababu ya wenzetu kututenga na kuzifanyia kazi na kushauri kamwe nchi isiyumbe kwa hilo.

Kabla ya hotuba ya Kikwete pia Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta katika ufafanuzi mbalimbali wa hoja za Wabunge kuhusu suala hilo, alisema sio sahihi kusema nchi hizo zimejitoa katika EAC wala Tanzania, lakini kuna mienendo ya chinichini isioashiria ustawi wa Jumuiya na watapata jibu la nini kinachoendelea muda mfupi ujao. Bunge hili pia bila shaka litapatiwa majibu sahihi ya sintofahamu hiyo kutoka kwa waziri mwenye dhamana ya ushirikiano huo na Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta.

Sehemu ya Azimio ilieleza hivi; ‘Tanzania imekuwa mwanachama wa EAC tangu mwaka 2005 na kwa kuwa nchi ya Kenya, Rwanda na Uganda zimekuwa zikifanya vikao na majadiliano mbalimbali bila kuishirikisha Tanzania wakati nchi yetu haijawahi kufanya jambo lolote la kuashiria kutaka kujitoa wala kutamka kuwa inataka kujitoa kwenye jumuiya hiyo, tunampongeza Rais Kikwete kwa kuliona hilo kwamba hatutajitoa EAC,’.

‘Bunge linaazimia kwamba linamuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete kuwa Tanzania isijitoe kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki na kuwataka watu wa Afrika Mashariki kuilinda na kuitetea Jumuiya’.

Baada ya azimio hilo kusomwa, Spika Anne Makinda aliwahoji wabunge ili kupitisha azimio hilo la Bunge na wabunge wote waliunga mkono hoja hilo na Bunge likapitisha azimio hilo.

Makinda alisema kutokana na kupitishwa kwa azimio hilo, Bunge lijalo, linaloanza wiki hii, wabunge watapata nafasi ya kutosha kuijadili hotuba ya Rais kuhusu suala hilo kwa kina kwa mustakabali wa Taifa.

Kinachotarajiwa katika mjadala wa hotuba hiyo ni muendelezo wa msimamo wa Rais Kikwete na majibu ya Serikali kuhusu nini kinachoendelea hivi sasa na hatua za kuchukua kuirejesha Jumuiya kwenye mstari.

Wabunge wachache waliopata nafasi kuchangia azimio hilo kabla halijapitishwa, walimpongeza Rais Kikwete kwa asilimia 100 na kusema msimamo na kauli hiyo imedhihirisha ukomavu wake wa kisiasa na uongozi.

Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia alisema, “Rais Kikwete kaonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa na uongozi. Lakini ni wakati wa kutafakari ni wapi tumekosea ili kubadili mtazamo na yale ambayo wenzetu wanayazungumza yatuwezeshe kuongeza kasi kuona kesho kuna nini ili tuchukue hatua,” amesema Mbatia.

Huenda wabunge wakati wakijadili hotuba hiyo kwa mapana yake, watagusia pia suala lililogusiwa kwa uchache na Mbatia kuhusu changamoto ya wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutokuwepo bungeni wakati Rais Kikwete akitoa msimamo wa nchi kupitia hotuba yake.

Jambo hili linaonesha wazi kuwa mara nyingi hakuna ushirikiano na mrejesho wa yanayojiri katika Bunge la EAC hata inapotokea kutofautiana baina yao hali aliyodai inakosesha nchi kujua yanayoendelea katika Jumuiya hiyo.

Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni alisema kuwa kauli ya Kikwete yenye msimamo wa Serikali na azimio la Lowassa, ni imani yake kuwa ana kila sababu ya kumpongeza Rais Kikwete na Bunge zima kwa hatua hiyo.

“Kujitoa EAC ni kutofikiri, tumejenga Taifa lenye hofu sana, tunakosa nguvu kama Taifa, tunakosa namna ya kuwajumuisha, tusilalamike, tukae ndani tutafakari, wapi tumekosea ili kuchukua hatua, tujiulize kwa nini imekuwa na kufikia hivi ilivyo? Kuna tatizo la ndani na lazima tulione na kufikiria namna ya kukabiliana nalo,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema nchi nyingine za EA zina malengo katika EAC na ni vema Tanzania ikafahamu kwa wazi nini malengo yetu kwa jumuiya hiyo. Anasema wabunge wa Kenya wakienda EA wanapewa maelekezo lakini wa hapa hawaripoti bungeni wala Bunge halijapewa taarifa yoyote.

“Wabunge wameanza kususia vikao na kununiana, wabunge hao wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, hayo yanapelekea wenzetu watuone hatupo nao, changamoto hii iwe ni kiashiria na mwito wa kuamsha Watanzania kujua nafasi kubwa ya jumuiya ipo kwa Tanzania kutokana na mazingira ya kijiografia hivyo kutumia fursa zilizopo,” alisema Mbowe.

Mbunge wa Viti Maalum na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Anna Abdallah alichangia azimio na kueleza kuwa wizara mbalimbali nchini zina matatizo katika kutekeleza majukumu yao jambo linalochangia wenzetu kutuona kama hatupo makini, alipendekeza mambo yaliotekelezwa yawekwe wazi na ambayo bado ili jamii ijue tulipo katika EAC.

Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama (CCM) alimpongeza Rais na kusema amefanya sawa, ametekeleza wajibu wake wa kitaifa kwani kitendo cha kuwaambia Watanzania hatuondoki katika EAC, ameonesha ni kiongozi anayetambua maana ya umoja na si utengano.

Ukurasa wa mjadala wa azimio ulifungwa na mkutano huu wa 14 wa Bunge, utafungua majadiliano mapya ya hotuba ya Rais Kikwete utakaotoa mtazamo wa Bunge la Tanzania katika EAC. Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi