loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Balozi Iddi: Bunge la Katiba litamaliza kero za Muungano

Inaelezwa kwamba haina maana kuwa katiba iliyopo sasa ambayo ilitungwa mwaka 1977 imepitwa na wakati kabisa na haina uwezo tena wa kufanya kazi na kuleta maendeleo kwa wananchi, bali dhana ni kuwa katiba mpya itabeba mabadiliko mengi yaliyoikumba nchi yetu na dunia kwa ujumla na hivyo kuwa na katiba itakayodumu kwa miaka mingine mingi.

Nia ya Rais Jakaya Kikwete kuanzisha mchakato wa Katiba mpya ni kushirikisha makundi yote ya wananchi katika kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo sasa, ambazo zimekuwa zikisababisha malalamiko na malumbano yasiyokuwa na tija hususan katika muungano wa pande zote mbili.

Makamu wa pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hivi karibuni, anasema kero za muungano zilizopo sasa njia pekee na ufumbuzi wake ni Bunge Maalumu la Katiba ambalo linatazamiwa kuanza tena shughuli zake Agosti mwaka huu.

Balozi Iddi anasema ushiriki wa wajumbe wa Bunge Maalumu kikamilifu utasaidia kuzipatia ufumbuzi kero hizo ambazo zimekuwa zikisababisha malalamiko ya muda mrefu dhidi ya muungano uliopo sasa ambao umedumu kwa muda wa miaka 50. Kwa mfano, Balozi Iddi anasema hadi sasa wajumbe wengi wa Bunge Maalumu kutoka Zanzibar hawajavitumia vizuri vikao vya Bunge hilo vilivyopita kuwasilisha kilio cha Zanzibar katika mambo yaliyomo katika Muungano.

“Mheshimiwa Spika, Bunge Maalumu linatazamiwa kuanza tena vikao vyake mwezi wa Agosti mwaka huu huko Dodoma, lakini Wazanzibari wakiwemo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wabunge hatujalitumia vizuri Bunge hilo,” anasema. Anasema kwa upande wa Zanzibar, zipo kero nyingi ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa ajili ya kuimarisha Muungano na kwamba baadhi yake zimekuwa zikidhoofisha uchumi wa Zanzibar.

Balozi Iddi analaumu baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu wa Zanzibar kutoka nje ya vikao na kuwaunga mkono wajumbe wengine na hivyo michango muhimu yenye maslahi kwa upande wa Zanzibar kushindwa kutolewa.

Anasema kitendo cha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka katika Chama cha Wananchi (CUF) kutoka Zanzibar kususia vikao hivyo hakileti sura nzuri na lengo la kuzipatia ufumbuzu kero za muungano zilizomo katika katiba ya sasa ama hata ambazo hazimo.

“Mimi sikuona sababu ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka CUF kususia vikao vile kwa kuungana mkono na wajumbe wengine wa upinzani,” anasema. Anasema kufuatia kitendo cha wapinzani kususa vikao vya Bunge la Katiba, matatizo na kero za Muungano kwa upande wa Wazanzibari kamwe hayatapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud wakati akijibu moja ya swali la wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliotaka kujua suala zima la ufumbuzi wa kero za Muungano, anasema mchakato wa Bunge Maalumu unaoendelea ndiyo njia muafaka wa kuzipatia ufumbuzi kero za muungano.

Aboud anafafanua zaidi kwamba jumla ya kero sita za muungano hazijapatiwa ufumbuzi hadi sasa na nyingine zinahitaji mabadiliko ya katiba. Anazitaja baadhi ya kero ambazo hazijapatiwa ufumbuzi wake na ambazo zinahitaji marekebisho kupitia katika mchakato wa Bunge la Katiba ni pamoja na suala la mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya muungano.

Anasema kuhusu suala la mafuta na gesi Wazanzibari ikiwemo Baraza la Wawakilishi wamepitisha azimio la kuondolewa katika orodha ya mambo ya muungano na kupata ridhaa ya wengi. Hata hivyo, anasema suala hilo linahitaji kupata ridhaa ya mchakato wa mabadiliko ya katiba kupitia Bunge Maalumu ambalo linatazamiwa kuendelea na vikao vyake katika awamu ya pili mwezi wa Augosti mwaka huu.

“Waheshimiwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, napenda kuwajulisha kwamba mchakato wa Katiba kupitia Bunge Maalumu la Katiba ndiyo utakaozipatia ufumbuzi kero za muungano zinazolalamikiwa na wananchi wengi wa Zanzibar kwa sasa,” anasema. Anasema kitendo cha wajumbe wa Bunge hilo kutoka Zanzibar kususia vikao hivyo kamwe hautozipatia ufumbuzi kero za muungano na kitakachobakia kwa Wazanzibari ni kulalamika tu.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui anasema miongoni mwa kero ambayo haijapatiwa ufumbuzi hadi sasa ni suala la wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa ushuru mara mbili wakati wanapoingiza bidhaa zao nchini. Anasema suala hilo ambalo ni moja ya kero za muungano zilizopo kwa muda mrefu, baadhi ya watendaji ikiwemo mawaziri wanadai kwamba zimepatiwa ufumbuzi na tatizo hilo halipo tena, jambo ambalo anasema si kweli.

“Si kweli hata kidogo, bado wafanyabiashara wa Zanzibar wakati wanapoingiza bidhaa zao katika soko la Tanzania Bara wanatozwa ushuru mara mbili,” anasema. Anasema malalamiko hayo ya wafanyabiashara kutoka Zanzibar ambayo hayajapatiwa ufumbuzi wake hadi sasa kwa kiasi kikubwa yanadhoofisha uchumi wa Zanzibar pamoja kuwafanya baadhi ya watu kuuchukia muungano.

Anatoa mfanowa karibuni wa wafanyabiashara kutoka Zanzibar ambao makontena yao ya mizigo yalikwama katika bandari ya Dar es Salaam kwa muda wa miezi miwili kufuatia uamuzi wa watendaji wa mamlaka ya kodi ya mapato nchini (TRA), kitendo ambacho kinaonesha wazi kwamba kero za muungano bado zipo.

“Mizigo ya makontena ya wafanyabiashara kutoka Zanzibar ilikwama Tanzania Bara bila ya sababu za msingi kwa sababu maelezo ya risiti za makontena hayo zinasema kwamba yanatakiwa kufika Zanzibar kama kituo chake cha mwisho ambapo ndipo yatakapolipiwa kodi,” anasema.

Mazrui anazitaka serikali zote mbili kuzipatia ufumbuzi kero za Muungano zaidi katika masuala ya biashara na ushuru wa forodha kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya uchumi wa Zanzibar. “Njia pekee ya kuzipatia ufumbuzi kero za muungano ni kulitumia Bunge Maalumu la Katiba lenye wajumbe mbalimbali ikiwemo kutoka Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano,” anafafanua.

Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee anasema baadhi ya watendaji wa Serikali ikiwemo wa taasisi za ukusanyaji mapato na kodi wanasababisha kwa makusudi migogoro ambayo huzorotesha maendeleo ya muungano. Kwa mfano, Mzee anasema kwa mujibu wa sheria ya kodi, ushuru unapaswa kutozwa katika eneo ambalo mzigo ndiyo kituo chake cha mwisho na si vinginevyo.

“Nawaomba watendaji wa mamlaka zinazosimamia kodi nchini kuacha kusababisha matatizo ambayo yatapelekea wafanyabiashara wetu kupata hasara katika utekelezaji wa majukumu yao,” anasema. Mzee anasema uchumi wa Zanzibar pamoja na mapato yake kwa asilimia 60 unategemea usafirishaji wa bidhaa mbali mbali zinazofanywa na wafanyabiashara wa ndani na nje.

Anasema vikwazo kama hivyo vitarudisha nyuma maendeleo ya Zanzibar na kuwavunja moyo wafanyabiashara hao kiasi cha wengine kuhamisha shughuli zao. Kero nyingine ya muungano ambayo imekuwa ikitajwa ni Zanzibar kutoruhusiwa kujiunga katika taasisi na mashirika ya kimataifa. Lingine linalolalamikiwa ni kuundwa kwa Tume ya pamoja ya fedha.

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi