loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Bandari ya Tanga: Nyenzo muhimu ya uchumi Tanzania

Moja ya nchi ambazo zimebahatika kuwa na rasilimali hiyo ni Tanzania, ambayo ina bandari kadhaa baharini na kwenye maziwa makuu. Kwa mtazamo wa kawaida Mungu ameifungulia Tanzania milango ya fursa za mafanikio kiuchumi, kwa kuipatia rasilimali hii muhimu.

Hata hivyo kuwepo kwa fursa ni kitu kingine na kuitumia fursa hiyo kuinua kiuchumi ni kitu kingine, na hapo ndipo penye vita ambayo kwa sasa Waziri wa Usafirishaji, Dk Harrison Mwakyembe anapambana nayo. Hivi karibuni waziri huyo alitembelea bandari ya Tanga, ziara iliyomchukua hadi wilayani Pangani kuikagua bandari ndogo iliyopo wilayani hapo.

Hali aliyojionea katika ziara hiyo ilimhuzunisha na kumfanya awe mkali kwa watendaji wa bandari, kwani bandari hizo zimekuwa zikiendeshwa katika mazingira ambayo hayatoi fursa ya kuchangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi. Anacholilia Dk Mwakyembe ni kutaka kuona kuwa bandari zinatoa mchango mkubwa kwa ukuaji wa uchumi wa nchi, na hili litawezekana tu pale kutakapokuwepo watendaji makini na wazalendo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Dk Mwakyembe katika ziara yake ni kwamba, kama vile uzalendo umetoweka miongoni mwa baadhi ya watumishi wa bandari, kila mmoja anafanya awezavyo kujinufaisha kibinafsi na akadiriki kutumia neno hili “wameigeuza bandari ya Tanga kuwa shamba la bibi.”

Wadau wa usafirishaji kwa upande wao kila mmoja amekuwa na la kusema na mmoja wao ni Ramadhani Manyeto ambaye alisema kuwa bandari hiyo imefika mahali pa kuwatoza malipo ya muda wa ziada wateja wake hususani wale wanaotaka kusafirisha au kutoa mizigo yao siku za mwisho wa wiki ambazo sio za kazi kwa sekta za umma kwa utaratibu uliozoeleka (Jumamosi na Jumapili).

Amesema utaratibu huo umekuwa ukilalamikiwa na wadau na kuwafanya wengine kuisusa bandari hiyo na kuamua kupitishia mizigo yao kwenye bandari ya nchi jirani, kitu ambacho kinakosesha mapato serikali. Ameshauri serikali kuchukua hatua za haraka kukomesha usumbufu kama huo ambao umekuwa kero kwa watumiaji wa bandari na kuinusuru ili isiendelee kupoteza wateja.

Dk Mwakyembe ameshangazwa na taarifa hiyo na kutaka apewe maelezo ya kina ambayo pamoja na ufafanuzi kutoka kwa kaimu meneja wa bandari Alfred Liundi alionesha kutoridhishwa na majibu yaliyotolewa. Hata hivyo Dk Mwakyembe ametoa changamoto mpya kwa watendaji wa bandari ya Tanga kwa kuwataka waanze kufanya kazi kibiashara na sio kwa mazoea kwa kuwa bandari ni lango la biashara.

Alisema kutokana na kipindi hiki cha ushindani kibiashara, mazoea hayana nafasi bali kinachotakiwa ni kwa watendaji kubadilika kutokana na ushindani uliopo na matakwa ya wateja wao ili waendelee kuwa sokoni.

Amesema vikwazo vidogo vidogo, usumbufu usio wa msingi kwa wateja na kutokuwajibika kwa watendaji na hasa vitendo vya kuhujumu mapato ya bandari na kuipunguzia serikali mapato, kamwe hayawezi kuvumilika kwani serikali kwa sasa imeamua kwa dhati kukuza uchumi wake na bandari ni moja ya sekta muhimu ya kufikia malengo hayo.

“Jamani kero ndogondogo kama hizi ndizo zinaathiri utendaji wa bandari zetu lazima tubadilike na tudhamirie kwa dhati kuona kuwa tunawavutia wateja wengi ili waweze kutumia bandari zetu jambo ambalo litainua pato la taifa kwa haraka,” alisisitiza Dk Mwakyembe.

Amemtaka kila mtendaji kujua kwamba kwa sasa serikali iko katika mchakato kabambe na kauli mbiu ya ‘matokeo makubwa sasa’ kwa hiyo kila mtendaji anapaswa kujielekeza katika muelekeo huo ili matokeo makubwa yenye tija yaweze kuonekana katika sekta ya uchukuzi ikiwemo bandari.

Ametamka bayana kwamba baada ya kuisafisha bandari ya Dar es Salaam sasa ameelekeza nguvu zake kwa bandari zingine ikiwemo bandari ya Tanga ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini. Amesema kwa kipindi hiki hatakuwa tayari kuona uzembe ukiendelea kutokea ambao unaathiri kwa kiwango kikubwa ufanisi wa bandari hapa nchini, na kutishia kuwawajibisha watendaji wote watakaobainika kuigeuza bandari kama shamba la bibi.

Amesisitiza kuwa hivi sasa watendaji wanaotaka kuwepo katika nafasi zao hawana budi kubadilika kifikra na mtazamo, na kuanza kuiendesha bandari kwa mfumo wa kibiashara zaidi.

“Hatuwezi kuendelea kufanya kazi kwa mazoea...kufanya kazi kwa mazoea kumetufikisha hapa tulipo ni lazima tubadilike sasa tunahitahji kuwa washindani zaidi katika sekta ya usafirishaji kwa kuondoa kero ndogondogo ili kuwavutia wateja wengi wa ndani na nje ya nchi,” alisema Dk Mwakyembe.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa bandari ya Tanga, Alfred Liundi anasema kuwa wamejipanga vya kutosha kuhakikisha kuwa bandari inabadilika kwa maana ya kuwavutia wateja zaidi.

Ameahidi kuondoa kasoro ndogondogo za kiutendaji ambazo kimsingi zilikuwa kama kero kwa wateja ili kuifanya badari ya Tanga kuwa moja ya bandari zenye huduma nzuri nchini. Aidha amesema kuna hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa ili kuongeza ufanisi wa bandari ya Tanga zikiwemo kuboresha baadhi ya vitengo ikiwemo kitengo cha makontena ili kuongeza ufanisi.

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) ...

foto
Mwandishi: Nestory Ngwega

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi