loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

BEST-AC na mafanikio lukuki ya kibiashara

Kwa miaka kumi ya programu hiyo, yapo baadhi ya mambo yameanza kuchukua mwelekeo mwingine ikiwa ni juhudi za programu hiyo kuwezesha mazingira ya biashara kuwa bora zaidi. Programu hii ambayo ilianza Juni 2004, ilimalizika siku chache baada ya kutimiza miaka kumi na shughuli za kuhitimisha programu hiyo zilifanyika katika ukumbi wa Kituo cha Utamaduni wa Ufaransa jijini Dar es Salaam na watu kadhaa walipata fursa ya kuizungumzia.

Wengi wa waliozungumza walisema kwamba programu hiyo imeweka ramani nzuri ya mafanikio katika mazingira ya kufanya biashara. Programu hii ya BEST-AC ambayo ilikuwa inafadhiliwa na Uholanzi, Denmark, Sweden na Uingereza baada ya kumalizika kwake inaingia programu ya BEST-Dialogue ambayo imezinduliwa mwezi huu.

Programu hii iliyokuwa ni kipengele cha tano cha uboreshaji wa mazingira ya kufanyia biashara nchini, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu imeelezwa na wadau mbalimbali waliozungumza na HabariLeo kwamba imesaidia kubadili mwelekeo wa ufanyaji biashara nchini na kuifanya serikali kuwa na muda wa kusikiliza wadau katika masuala ya biashara.

Wapo waliosema kwamba kutokana na programu hiyo wamepata mafanikio hasa ya kutambuliwa kuwapo kwao na ushauri wao kusikilizwa. Miongoni mwa waliokiri waziwazi umuhimu wa BEST AC ni taasisi inayoshughulikia nyaraka za mizigo kwenye meli kama zimezingatia sheria ya uingizaji na utoaji, Tanzania Ship Tally Association.

“BEST-AC imetusaidia sana. Imetupatia fedha na ushauri ambao umetufanya kufanya utyafiti na kutengeneza hoja za msingi za kutengeneza kanuni ambazo zitasaidia utawala wa sekta ya meli nchini,” anasema makamu Mwenyekiti wa Tanzania Ship Tally Association, Hezekiah Teveli.

“Kwa msaada wa BEST-AC kanuni za ukaguzi wa mizigo kuona kama taratibu zimezingatiwa zimekamilika na kupelekwa serikalini na sasa tunasubiri zifikishwe wizarani kwa maidhinisho,” alisema Teveli. Teveli na taasisi yake wanaamini kwamba tatizo la mizigo ya magendo litamalizwa nchini kama serikali itachukua hatua ya kuimarisha ukaguzi wa mizigo inayoingia au kutoka kuona kama ina nyaraka sahihi.

Inadaiwa kwamba Tanzania hupoteza mamilioni ya dola kutokana na uvushaji kimagendo wa mizigo, hasa ya raslimali zake kama wanyama, pembe za ndovu, madini, vyakula na bidhaa nyingine nyingi. Imeelezwa hali hiyo inasababishwa na kutokuwepo kwa taratibu za ukaguzi wa mizigo inayotolewa au kuingizwa katika meli.

Teveli anasema hapo awali serikali haikuwa inajua umuhimu wa sekta hii ili kuweka kanuni za ukaguzi na sasa wametambua na kuanza kushughulikia kutokana na jinsi BEST AC ilivyowezesha kutengeneza hoja baada ya kufanya utafiti wa kina. Kukosekana kwa kanuni kumefanya Sheria ya Meli ya mwaka 2002 (Shipping Agency Act of 2002) kuwa ya upande mmoja, ikifaidisha mashirika na mawakala wa meli na kuiacha hoi nchi.

Nayo chemba ya biashara ya Iringa (TCCIA) imeshukuru BEST-AC kwa msaada wake hasa katika masuala ya mizani na vipimo kwenye mazao. Kwa msaada wa BEST-AC kulifanyika utafiti na kuonekana kasoro katika vipimo na mizani, na kutokana na hilo serikali ilitoa miongozo na sasa wakulima wanafaidika kwa mabadiliko yaliyotokea ambayo yamefanya wafanyabiashara kuwa na vipimo sahihi kwa wakulima.

Mwenyekiti wa zamani wa TCCIA Iringa, Enock Ndondole anasema nyaraka walizotengeneza za ushawishi baada ya kuona madhila yanayowakumba wananchi zilifanya wakulima wengi kujua mtindo mbovu uliopo na hivyo kutaka kuwepo kwa mabadiliko huku serikali nayo ikiweka vyema ukaguzi wa mizani kuzuia wizi.

Aidha kutokana na tafiti hizo, serikali iliweka wakaguzi wa kuangalia kama wafanyabiashara wanafuata maelekezo ya serikali kuhusu vipimo. Katika utafiti wa mwaka 2013 uliofadhiliwa na BEST-AC ilijulikana kwamba wakazi wa Iringa na Njombe pekee walikuwa wanapoteza zaidi ya shilingi bilioni 2.5 kwa kutokuwepo kwa vipimo sahihi kwa ajili ya mahindi na mpunga pale nafaka zilizokuwa zikiuzwa kwa mfumo wa lumbesa.

Ndondole alitaka mrithi wa BEST-AC, yaani BEST Dialogue kuendelea kusaidia uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini ili kukuza uchumi wa mtu mmoja na taifa kwa ujumla.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi