loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

CCM yasikitishwa wapinzani kususa Bunge

Hayo yalisemwa na Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu wakati alipozungumza na wanachama wa chama hicho katika majimbo ya Mtoni na Magogoni.

Jabu alisema mchakato wa kupata Katiba mpya ndiyo nafasi pekee kwa Wazanzibari kupata Katiba ambayo itazipatia ufumbuzi kero za Muungano zilizopo hivi asa ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa kiwango kikubwa na wananchi.

Akifafanua alisema kwa muda mrefu Wazanzibari wanalalamika kuwapo kwa kero na kubanwa katika mambo mbalimbali katika Muungano, lakini kwa bahati mbaya hakuna sehemu muafaka ya kuwasilisha malalamiko hayo.

“Watanzania tunapaswa kumshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuamua kuanzisha mchakato wa Katiba mpya ambao huo ndiyo utakaoyapatia ufumbuzi matatizo mbali mbali yaliomo katika Muungano wetu,” alisema Jabu.

Hata hivyo, alisema amesikitishwa na tabia ya wapinzani kugomea mchakato huo bila ya sababu za msingi na hivyo kushindwa kuwatendea haki wananchi wa Zanzibar ambao mategemeo yao makubwa ni kuwakilishwa kupitia ushiriki mzuri wa wajumbe walioteuliwa na Rais katika Bunge hilo.

“Sisi tulitaka wapinzani washiriki vizuri katika mchakato wa Katiba wakiwa ndani ya Bunge na kutoa mchango wao vizuri lakini kwa bahati mbaya wamegoma,” alisema Jabu.

Jabu aliwataka wapinzani watambue kuwa Katiba mpya haiwezi kupatikana nje ya Bunge Maalumu la Katiba kwa kuitisha mikutano ya hadhara au kutishia kufanya maandamano ya nchi nzima. Baadhi ya mambo ambayo Wazanzibari wanataka yaondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano yaliopo sasa ni suala la nishati ya mafuta na gesi. Jabu alisema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wanaendelea na kazi ya kuichambua rasimu hiyo, ikiwamo mambo yote ambayo yanaonekana kikwazo katika Muungano kwa ajili ya kupata Katiba nzuri.

“Hatua tuliofikia ni kubwa na hatuwezi tena kurudi nyuma na kuwasubiri wapinzani kwani yapo baadhi ya mambo tumeyazungumza vizuri sana ambayo ni kikwazo katika Muungano,” alisema Jabu.

Wanachama wengi wa CCM wameunga mkono msimamo wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuendelea na mchakato wa Katiba bila ya kuwasubiri wapinzani.

Mjumbe wa nyumba kumi kutoka Magogoni, Haji Faki aliwataka wajumbe wa Bunge hilo, wasikubali kuyumbishwa na wapinzani, ambao wamekuwa wakijaribu kudhoofisha mchakato wa Katiba.

Aidha alisema uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM, unastahili kupongezwa ambao umelitaka Bunge hilo kuendelea na vikao vyake huko mkoani Dodoma.

“Tunawapongeza wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa kuamua kuendelea na mchakato wa vikao vya Bunge la Katiba bila ya wapinzani kwani Watanzania wanataka Katiba mpya na si malumbano,” alisema Jabu.

RAIS John Pombe Magufuli anaongoza kwenye ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi