loader
Dstv Habarileo  Mobile
CHAUSIKU WAMBURA: Saratani ya macho inanitesa

CHAUSIKU WAMBURA: Saratani ya macho inanitesa

Ni kauli ya Chausiku Wambura (45), mkazi wa kijiji cha Bwitengi kilichopo umbali wa kilometa 30 kutoka mji wa Mugumu, wilayani Serengeti, alipozungumza na mwandishi wa makala haya. Unapomuangalia huwezi kujua kuwa anakabiliwa na maradhi ya saratani.

Pengine utatambua hilo atakaponyanyua uso wake kukuangalia ambapo utakutana na jicho pekee la kushoto lililosalia likitiririsha usaha. Saratani ni kundi la magonjwa yanayosababishwa na mgawanyiko usio sawa na usiodhibitika wa seli na kuunda uvimbe unaovamia na kuzidhuru tishu katika mwili wa binadamu. Saratani isiyotibiwa inaweza kuwa ugonjwa unaoshambulia tishu nyingine mwilini na kusababisha kifo.

Kuna aina zaidi ya 100 za saratani zinazotofautishwa kwa kuzingatia zimeingia katika kiungo gani cha mwili na kukiathiri na kuanza kuenea mwilini.

Hata hivyo, aina zote hizo za saratani zina sifa tatu muhimu zinazofanana. Sifa hizo ni ukuaji usiodhibitika wa seli, uwezo wa kuvamia na kushambulia tishu nyingine na uwezo wa kusambaa katika viungo vingine vya mwili kupitia mishipa ya damu au mfumo wa limfu(lymphatic system).

Unapomuangalia Chausiku utagundua kuwa jicho lake moja limeondolewa na utakutana na jicho la kulia, jicho pekee alilosalia nalo likitoa usaha.

Utagundua pia ni mtu anayehitaji msaada wa hali na mali, ili aweze kujitibia maradhi yanayomkabili. Anasema maisha yake yote katika kipindi cha miaka kumi iliyopita tangu alipogundulika kuugua ugonjwa huo wa saratani yamekuwa ni kilio usiku na mchana kutokana na maumivu makali anayoyapata ya saratani ya jicho.

“Nahitaji msaada ili nikafanyiwe upasuaji kwa jicho hili la pili linalonisumbua,” anasema na kuongeza kuwa alifanyiwa upasuaji wa jicho la kwanza katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyoko jijini Mwanza ambalo kwa sasa limeziba na halioni tena. Anasema anahitaji kiasi cha Sh 350,000 kwa ajili ya kwenda kufanyiwa upasuaji wa jicho lake la pili katika hospitali hiyo, lakini kiasi hicho cha fedha kwake imekuwa mtihani mkubwa kukipata.

Uwezo wa kufanya kazi

Anasema kwa sasa amepoteza uwezo wake wa kufanya kazi kama ilivyokuwa hapo awali alipokuwa mama mwenye nguvu za kutosha, akilima na kufuga ng’ombe na sasa ni tegemezi. Anasema kabla ya kuugua ugonjwa huo, alikuwa na uwezo wa kulisha familia yake ya watoto sita aliowazaa, wanne wakiwa ni wa kiume na wengine wawili wa kike walifariki dunia kwa malaria.

Kwa hivi sasa anaishi kwa kuomba msaada kwa makanisa, na wasamaria wema, ambao anasema humpatia msaada kutokana na watoto wake kutokuwa na uwezo wa kumsaidia kuzalisha mali kutokana na umri wao kuwa mdogo. Kutokana na ulemavu alio nao hivi sasa anasaidiwa kazi za kupika na mtoto wake wa kike ambaye ni wa mwisho kuzaliwa, Neema Hereni mwenye umri wa miaka minane.

Anasema Neema humsaidia kazi zote za nyumbani, kupika na kutafuta kipato cha familia, kwa kuomba fedha kwa wasamaria wema. Wakati mwingine Neema hupatiwa msaada wa chakula kutoka kwa majirani na makanisa ambao humsitiri yeye Neema, mama mtu na mdogo wake. Neema anaenda kuteka maji lita kumi kisimani umbali wa kilomita 2 kila siku.

Ndiye huokota kuni za kupikia na huenda shule mara moja moja wakati ambao mama yake hupata unafuu wa maumivu na anapozidiwa Neema hulazimika kukaa nyumbani kumhudumia mama yake.

Historia ya ugonjwa

Anasema alianza kuhisi dalili za awali mwaka 2005 ambapo alienda katika hospitali ya wilaya ya Mugumu na ndipo alipoelezwa anakabiliwa na ugonjwa wa saratani. Lakini dalili za kuwashwa ziliongezeka hadi alipopata msaada mwaka 2005 kutoka kwa msamaria aliyempa Sh 360,000 na kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambapo alifanyiwa upasuaji wa jicho la kulia.

“Baada ya kufanyiwa upasuaji nilipona kabisa, lakini ilipofika mwaka 2008 dalili zile za mwanzo zilinirudia na niliporudi hospitalini ya wilaya nikaelezwa kuwa nina ugonjwa wa saratani, na hadi sasa natumia dawa za kutuliza maumivu,” anasema.

Anasema anahitaji msaada wa fedha kwa ajili ya matibabu katika hospitali ya Bugando, ingawa hajui atadaiwa kiasi gani kutokana na kupanda kwa gharama za maisha na matibabu. Anahitaji msaada pia kwa watoto wake kwenda shule. Kwa hivi sasa hawasomi, wako nyumbani na ndio kwa sasa hufanya shughuli za uzalishaji mali ikiwa ni pamoja kumfanyia usafi wa mwili.

Maisha ya ndoa

Aliolewa mwaka 1986 na kubahatika kuzaa watoto sita lakini kwa bahati mbaya mume wake alifariki dunia mwaka 2005 na kumuachia kazi ya kulea familia peke yake. Katika watoto wanne ambao wako hai, kijana wake wa pekee Juma Hereni (18) anasumbuliwa na ugonjwa wa kuanguka na sasa anaishi kwa bibi yake.

Mtoto wake mwingine ni Esther Hereni (16) aliyezaa watoto wawili yupo nyumbani na sasa hana kazi wala makazi maalumu. “Bado ni mdogo sana lakini aliniachia hapa wajukuu wawili, Julius wa miaka minne na Judith wa miaka miwili,” anasema, hali inayoonesha kwamba binti huyo alizaa mwanawe wa kwanza akiwa na umri wa miaka 12.

Hata hivyo, Chausiku anasema mara moja moja, Esther akipata kitu huko katika utafutaji wake huwa anamkumbuka mama yake kwa kumtumia pesa. “Esther amekuwa msaada mkubwa kwetu ingawa hana kazi ya kuajiriwa. Siku hizi nasikia anafanya kazi ya kuuza baa,” anasema.

Anasema mtoto wake wa tatu, Frank Hereni (9) yeye alitoroka nyumbani baada ya tukio la kuchomewa nyumba zao na mtu waliye na ugomvi wa kifamilia, ambapo anasema hadi sasa hajulikani aliko. Ugomvi huo ulitokana na tuhuma za kijana wake kununua kondoo wa wizi.

Majirani wanasemaje?

Mmoja wa majirani zake, Sarah Machota anasema Chausiku anakumbwa na mateso yasiyoelezeka kutokana na ugonjwa huo wa saratani na kuwa hana msaada wowote. “Licha ya kusaidiwa na mwanawe Neema, maisha yake yako hatarini. Kwa kweli anahitaji msaada wa fedha za matibabu, chakula na malazi, maana baada ya kuchomewa nyumba zake, vitanda na nguo zake zote ziliteketea kwa moto,” anaeleza Machota.

Samwel Bwigeki ambaye ana undugu na Chausiku Wambura anakiri pia kwamba Chausiku anaishi katika mateso makubwa, lakini kutokana na umaskini unaowakabili wengi kijijini hapo, akiwemo yeye wameshindwa kumsaidia.

“Ndugu yetu amepata mateso ya muda mrefu. Ameuza kila kitu alichokuwa nacho ili akatibiwe lakini bado pesa hazikutosha. Tunamuachie Mungu ili awaguse watu wamchangie akatibiwe,” anasema. Kwa matatizo aliyo nayo Chausiku ni dhahiri anahitaji mchango wa hali na mali kwa kila anayeguswa.

Kikubwa anachohitaji mwanamke huyo ni kusafirishwa hadi Bugando kupata matibabu ama hospitali ya saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam. Wanaotaka kufika kwa Chausiku wanaweza kufika kwenye ofisi za gazeti hili za jijini Mwanza au kuwasiliana na Mwandishi kupitia 0756 823 420.

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi