loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Cheka na ubabaishaji wa mapambano

Siku chache baada ya kupata taarifa hiyo, gazeti hili lilimtafuta Cheka kuzungumza naye kuhusu pambano hilo, na kusema kwamba ni kweli lengo ni kuwapa nafasi mabondia walioonesha uchu wa kupambana naye kutumia fursa hiyo. Alisema pambano hilo lingefanyika Oktoba mosi na baadaye ikaelezwa litafanyika Novemba mosi, mwaka huu.

Pia, alisema kwa kutumia kampuni yake mpya atakuwa akiandaa mapambano mengi na kuzunguka katika mikoa yote Tanzania kwa ajili ya kuinua vipaji vya mabondia ili kuvisaidia. Baada ya wiki kama moja, Rais wa TPBC, Chaurembo Palasa akaita waandishi wa habari na kuzungumzia pambano hilo kwamba wameliidhinisha hivyo kutoa baraka zote.

Wakati huo, mpinzani aliyetarajiwa kucheza naye, Paschal Ndomba alisema pambano hilo limekuja wakati muafaka wa kumwonesha bondia huyo wa Tanzania kwamba yeye ni zaidi yake.

Kauli ya Ndomba ilitokana na ukweli kwamba alikuwa akitamani kwa miaka mingi kucheza naye, lakini akidai kuwa mpinzani wake huyo alikuwa akimkwepa kwa muda mrefu kwani kuna baadhi ya watu humdanganya bondia huyo wa Morogoro kuwa akicheza naye atapigwa.

Alisema kila alipojaribu kukutana na kuzungumza naye, alimuahidi kuandaa pambano litakalowakutanisha pamoja hivyo, wakakubaliana wakutane kwa mara ya kwanza kuoneshana nani mkali kati yao. Hilo lilimpa furaha kubwa Ndomba ambaye alikuwa akimwinda Cheka kwa miaka mingi na kuona sasa wakati umefika kwake kuwaonesha Watanzania uwezo wake.

Ndomba anasema katika kuafikiana makubaliano, alikwenda hadi Morogoro wakasaini mkataba chini ya Kampuni ya Cheka ili wapigane Novemba mosi. “Cheka alikuwa hataki kuja kunifuata kwa sababu nilitaka kucheza naye nikaamua nitumie gharama zangu mwenyewe nimfuate Morogoro ili tu tusaini huo mkataba wa kupigana,” anasema Ndomba.

Anasema anachosubiri kwa sasa ni siku ifike kama walivyosaini ili wapambane na kutimiza kile walichokusudia. Ndomba anafafanua kuwa baada ya mkataba huo, alianza mazoezi ya nguvu chini ya makocha watano kwa gharama zake mwenyewe, kwani kiasi alichoingia makubaliano na Cheka ni kidogo sana.

Anasema aliamua kukubali kiasi kidogo kwa vile anataka kujenga heshima kwa kumshinda Cheka, kwani kwa kipindi cha zaidi ya miaka saba hajawahi kucheza naye. Anasema aliwahi kupambana na mabondia wengine kama Rashid Matumla, Thomas Mashali, Mkenya Joseph Odhiambo na mabondia wengine mbalimbali nchini.

Pia, amewahi kupambana na mabondia kadhaa katika nchi za Ulaya na Marekani ambako aliishi kwa muda mrefu na kuingia makubaliano na kampuni moja ya ngumi iliyopo Miami nchini Marekani. Jambo la kushangaza, hivi karibuni Cheka alibadilisha mawazo ghafla akisema hawezi kupigana na Ndomba kwa sababu haeleweki.

Pambano lao lilikuwa lisilo la ubingwa. Hata hivyo, hakutaka kuweka wazi zaidi kinachoendelea hadi kujitoa na kusema haeleweki wakati tayari wana mkataba. Katika mazungumzo na gazeti hili, Cheka alidai kuwa hakusaini mkataba na Ndomba wakati awali, Rais wa TPBC Chaurembo Palasa aliweka wazi ukweli kwamba wamesaini mkataba.

Jambo la kushangaza ni kwamba Cheka alitangaza kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuwa atapambana na bondia wa Kenya ndani ya mwezi ujao. Hakuzungumzia pambano dhidi yake na Ndomba ambalo bado linasubiriwa kwa sababu halijawekwa wazi kama lipo au halitokuwepo kwa vile mpinzani wake hajapata taarifa rasmi za pambano hilo kutokuwepo.

Ndomba anasema yeye kwa vile hajapewa taarifa hizo ataendelea na mazoezi kama walivyosaini. Anasema pambano lazima liwepo kwa sababu kwanza ametumia gharama kubwa kuwatafuta makocha wa kumuandaa dhidi ya pambano hilo. Pia, mashabiki wake wanalisubiri kwa hamu kuona nani mkali kati yao, hivyo hatambui kwamba limevunjwa kwa sababu mkataba wake anao na hajafanya mazungumzo yoyote na Cheka.

Ndomba anasema tabia ya Cheka kutangaza mapambano na kuahirisha ni la kawaida kwa sababu aliwahi kufanya hivyo kwa baadhi ya mabondia wengine, lakini kwa vile walikuwa hawakusaini mkataba walikuwa wakishindwa kumchukulia hatua. Anasema yeye ambaye ana mkataba naye asipotekeleza kama walivyokubaliana huenda akamchukulia hatua za kisheria.

Anasema Cheka ametangaza kutopambana naye ili kutompa nafasi Ndomba kujiandaa kwa mazoezi, kwani humwogopa kwa muda mrefu. “Sasa mimi nasema kuwa pambano lipo na nitaendelea na mazoezi kwasababu sina taarifa na mkataba ninao, ninasubiri siku ifike kama hataandaa nitamchukulia hatua,” anasema.

Kwa kuangalia hayo ni dhahiri kuwa Cheka anaonekana kutokujiamini kwa watu anaowachagua kupambana nao. Kwani aliwezaje kutangaza kupambana na Ndomba hadi kusaini mkataba kama alikuwa haeleweki, kwa nini alikubali kusaini? Akiulizwa hilo anadai kuwa mtu mwenyewe haeleweki.

Jambo linaloshangaza ni kitendo cha yeye kusema anawapa nafasi mabondia waliokuwa na hamu ya kupambana naye. Sasa leo anazungumza mambo mengine kinyume cha kile anachokisema, kampuni yake itafikia wapi kama wanaanza na ubabaishaji kama huo? Kinachohitajika ni Cheka kujirekebisha na kujenga msimamo kabla ya kuchukua hatua bila kushawishiwa na mtu ili anapofanya maamuzi fulani yasije kumwingiza kwenye matatizo.

Pia, ikiwa ataendelea na tabia ya kutangaza mapambano na baadaye kujitoa bila sababu zinazoeleweka, itafikia wakati na mabondia wenzake watamdharau hivyo anahitaji kujirekebisha. Watu wanaweza wakafikiri pengine kwa sababu ni kampuni yake ndio inayoandaa mapambano, hatawatendea haki mabondia ndio maana anajiamulia bila kuwashirikisha wapinzani wake.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi