loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Chifu wa Wagogo anayetaka hadhi yao itambuliwe

Hawa ni machifu wa Ukoo wa Biringi ambao walitawala miaka mingi iliyopita. Ninafika katika eneo hili lenye nyumba nyingi na watu wengi na mara ninakuwa mbele ya Chifu Ally Biringi tukisalimia. Ni mtu mkarimu na mcheshi. Aninikaribisha nyumbani kwake kwa bashasha. “Hapa ndipo Ikulu na unayemuona pale ni mama yangu,” anasema Chifu baada ya kusalimiana.

Anayenitambulisha kwake ni bibi moja mzee ambaye wakati ninaingia ninamkuta akila ugali wa mtama kwa mlenda. Bibi huyo, ingawa anaonekana ni mzee ninamuamkia kwa lugha ya Kiswahili kama kubahatisha. Siamini kama anakijua lakini kwa mshangao anaitikia pia kwa bashasha huku akinikaribisha chakula.

Ninamsalimia na kumtania kama bibi yangu. Tunacheka. Ikulu hiyo ina nyumba zaidi ya 20 ambazo wanaishi wake wa Chifu, watoto na hata wajukuu.

Akiwa amezaliwa mwaka 1943, Chifu Ally Biringi anasema ana wake wanane na kwamba kupitia wake hao alibahatika kupata watoto 56 lakini walio hai mpaka sasa ni 38, wa kike 20 na wa kiume 18. Anasema kutokana na watoto hao ana wajukuu zaidi ya 100.

Akiwa na miaka 71 sasa, mke wake wa kwanza alimuoa mwaka 1959 lakini alifariki dunia mwaka 1994 na mke wa mwisho alimuoa mwaka 2011.

Pamoja na hayo anasema baba yake mzazi, mzee Ngalya Biringi alikuwa na wake 12 na watoto zaidi ya 60. Ukoo wa Biringi ni miongoni mwa ukoo wa machifu wa Kigogo ambapo anasema asili ya Wagogo wengine walitoka Usukumani, Uhehe na Ungoni lakini Wagogo ambao wana asili ya Wahehe ni wengi na wamekuwa wakiwafanya kama wajomba.

Anasema wakati wa utawala wa kikoloni machifu walikuwa wakiitwa watemi akiwemo Chifu Mazengo wa Mvumi. Ally Biringi ni mjukuu wa Chifu wa Wagogo, Salehe Issa Biringi aliyeishi Makulu Dodoma.

Baada ya kufariki dunia alimwachia mikoba mwanawe Ngalya Biringi ambaye pia alifariki dunia mwaka 1972 na ndipo baada ya kifo hicho Ukoo ulimchagua yeye Ally kuwa Chifu. Hii ilikuwa Juni 1972.

“Baba alifariki mwaka 1972 akiwa hapahapa Makulu Dodoma na baada ya kifo chake ukoo ukanichagua na kunirithisha mikoba na vitu vyote vya mila na desturi,” anasema. Pia anasema kimsingi Chifu anatakiwa kuwa ni mtu anayependa watu, mshauri na awe anaipenda jamii yote na asiye na majivuno na kwamba huenda ndio maana ukoo uliamua kumchagua yeye miongoni mwa watoto kadhaa wa baba yake.

“Kimsingi uchifu huu si wa kuchaguana. Chifu akifa anapewa cheo hicho mtoto wake mkubwa ila wanaangalia kama ana akili timamu lakini kama mtoto mkubwa hafai anapewa hata mtoto mdogo. Ukimpa uchifu mtoto mkorofi si ataua Ikulu?” Anasema. Vilevile anasema Chifu si lazima awe na wake wengi.

"Hata ukiwa na mke mmoja unaweza kuwa Chifu. Kadhalika Chifu huwezi kuacha mwanamke, mnatengana tu kwani ukiacha mke huwezi kuwa mtawala," anasema.

Anataja miongoni mwa vitu alivyoachiwa kuwa ni pamoja na mawe ya tambiko yanayotumika kuita mvua pale mvua zinapochelewa kunyesha.

“Kwenye mikoba niliyoachiwa kuna mashuka meusi ya kujifunika, mkia wa ng’ombe (mpuza), vyungu kwa ajili ya kuwekea dawa za asili na fimbo yenye kifundo kilichochongoka (nyolele).

Anasema vitu vyote hivyo hutumika kwenye utunzaji wa mawe. Anasema kuna wazee wa kimila waliochaguliwa ambao huosha mawe hayo kwa kutumia mafuta ya kondoo na kisha kutambika na wakati wa kutambika wanaita majina ya watu waliokufa lakini kabla ya yote wanamuita Mungu ili atangulie sala yao.

“Kuna mawe jike na mawe dume lakini mawe jike yanakuwa na duara katikati wakati ya kiume yanakuwa ni makubwa na baada ya kuyaosha kwa kutumia mafuta ya kondoo ndipo shughuli za matambiko hufanyika,” anasema.

Aidha wanaofanya kazi ya tambiko ni wazee wa kimila kwa masharti kwamba wanatakiwa kuwa weusi na mtu mweupe haruhusiwi kushiriki kazi hiyo kwani wanaamini kuwa mtu mweupe ni kama radi. Pia tambiko la kuomba mvua limekuwa likifanyika kwenye kaburi la babu yao aliyefariki muda mrefu.

“Imani ndiyo hupelekea kufanya matambiko na kabla ya kufanya hivyo huanza kwa kumuomba Mungu na si lazima tunapofanya tambiko lazima mvua inyeshe,” anasema.

Anasema Wagogo wamekuwa na ngoma ya asili maarufu kama Muheme ambayo imekuwa kichezwa wakati wa sherehe na wakati wa kupeleka watoto suna au wakati wa sherehe yoyote kama za kimila au za kitaifa, ambapo ngoma hiyo imekuwa ikichezwa kwa kutumia mabega.

Alipoulizwa yeye kama Muislamu ana mudu vipi kufanya mambo ya kimila ikiwa ni pamoja na kuoa wake zaidi ya wanne kinyume na mafundisho ya dini hiyo, Chifu Biringi anakiri kwamba yeye ni Muislamu lakini kutokana na uongozi alionao katika jamii analazimika kuegemea zaidi kwenye mila.

Kwa mujibu wa machapisho mbalimbali, neno Wagogo linatokana na msafara wa kale wa Wanyamwezi kwamba ulipambana na kundi la Wagogo waliopiga kambi karibu na miti iliyoanguka hali iliyopelekea baadaye kujulikana kama watu wa magogoni. Pia jina hilo inasemekana kuwa na uhusiano na ile namna ya ujenzi wa nyumba za Wagogo ambapo hutuma mbao nyingi.

Kihistoria kila ukoo ulikuwa na kiongozi aliyekuwa akiitwa majina kutegemea kabila kama vile, mtemi, omukama, mwami, mangi na kadhalika ingawa wazungu walipokuja wakapendelea kuwaita sultani au chifu.

Tangu enzi za mababu Wagogo walijenga nyumba za tembe na hii kutokana na majani ya kuezekea kuwa haba ambapo mapaa yalijengwa kwa kutumia fito na udongo.

Historia na maendeleo ya Wagogo, yanaelezwa katika machapisho hayo kwamba iliathiriwa na ukame na biashara ya watumwa, mambo anayosema yalileta athari mpaka leo, kwani kabila hilo ni kati ya makabila fukara hapa nchini.

Chakula kikuu cha Wagogo ni ugali wa uwele na wao huchukulia ugali wa mahindi kama mwepesi. Lakini kutokana na mabadiliko ya kilimo, ugali wa matama unaonekana kuliwa zaidi na watu wa kabila hilo katika siku za karibuni.

Tohara Chifu Biringi anasema zamani watoto wa kike na wa kiume walikuwa wakipelekwa tohara. Sasa tohara kwa watoto wa kike imezuiliwa, lakini watu wanaofuata mila wanaona kama mila hiyo imepuuzwa.

Aidha mwanamume asiyetahiriwa alikuwa akiitwa Layoni na kama alikuwa hataki kufanya tohara alikuwa akitengwa na makundi ya watu waliotahiriwa.

Anasema mtoto wa Kigogo hutakiwa kwenda tohara akiwa na miaka saba na kuendelea ambapo wazazi huanza kwa kukaa vikao na kuamua siku ya kupeleka watoto wao jandoni.

Pia watoto wamekuwa wakikaa huko kwa muda wa miezi miwili ambapo ngoma ya Hambalaa hupigwa na hukaa porini huku wakipatiwa mafunzo ya kuwa na utii ikiwemo kupiga hodi kabla ya kuingia ndani na masuala muhimu ambao humfunza adabu mtoto na kuheshimu wakubwa.

Lakini miaka ya nyuma mwanamke au mwanamume kama hajafanyiwa tohara alikuwa haoi wala haolewi na wanaume walikuwa wakikataa watu wasiotahiriwa na wanawake walikuwa wakikataa wanaume wasiotahiriwa.

“Watu wenye mila zao wanaona vigumu kuacha na kuamua kuendeleza mila hizo ila mara nyingi kwa kificho sana,” anasema. Kuoa na kuolewa

Anasema mwanamume akitaka kuposa mke wazazi wa pande mbili wanakutana kisha wanapanga mahari na sehemu ya kukabidhiana mahari hiyo na hapo vikao vya ndoa vinaendelea kufanywa.

Kama mwanamume anatoka kwenye koo ya kitajiri hulipa ng’ombe kati ya 30 hadi 40 ama mbuzi kwa idadi kama hiyo. Kama ni mwanamume anayetoka koo ya kimasikini hulipa mahari ya wastani wa ng’ombe 20 na mbuzi 20.

“Kama mwanamke akiolewa na kugundulika kwamba hazai mwanamume anaomba ruhusa ya kuoa mwanamke mwingine atakayemzalia watoto,” anasema. Pia anasema endapo kutatokea mafarakano na wanandoa wakashindwa kuishi pamoja na kuamua kuachana kinatafutwa chanzo cha ndoa ili kujua mustakabali wa mahari.

"Endapo chanzo cha kuvunjika kwa ndoa hiyo ni mwanamke basi wazazi wake watalazimika kurudisha ng’ombe zote zilizotolewa kama mahari lakini kama mwanamume ndiye mkorofi basi itakuwa ni hasara kwake," anasema.

Albino walifukiwa wakiwa hai Anasema mila na desturi za kale za Wagogo zilikuwa haziwatabui watoto waliozaliwa na ulemavu wa ngozi (albino) na kwamba walionekana kama mkosi.

“Kwa jinsi nilivyosikia miaka ya nyuma mtoto akizaliwa albino alikuwa akizikwa akiwa hai lakini wengine walikuwa wakiachwa waishi kwa imani kuwa watakuja kupotea wenyewe,” anasema.

Anasema bado kuna imani kuwa albino wamekuwa wakipotea kwani hata ukiuliza watu wengi wanasema hawajawahi kwenda kuzika albino, ingawa hata alisema dhana hiyo si ya kweli.

Pamoja na hayo anasema sasa wameamua kuenzi baadhi ya mila kwa kuzitambua na sasa kwenye uongozi wake kuna kanda inaandaliwa ambayo itakuwa na nyimbo za kimila.

Pamoja na hayo anasema kuna Wagogo wafugaji ambao wamekuwa wakiishi maisha ya dhiki licha ya kuwa na mifugo mingi. “Kuna Wagogo wafugaji wanaishi maisha duni wakati wana utajiri mkubwa wa ng'ombe.

Ninawashauri wauze ngombe wajenge nyumba za kisasa. Ufugaji wa ng’ombe wengi kwa sasa umepitwa na wakati kwani ardhi inakuwa ndogo kutokana na idadi ya watu kuongezeka,” anasema.

Mahakama za machifu Anasema Chifu Salehe alikuwa na Mahakama iliyokuwa karibu na reli eneo la Makulu lakini pagale hilo halipo sasa.

“Miaka ya nyuma kulikuwa na mahakama ambazo zilikuwa zikiendesha kesi za kimila ambapo Mahakama moja tayari ilishafutika na kilichobaki ni udongo unaoonesha hapo. Pale palikuwa na jengo miaka mingi iliyopita,” anasema.

Pia kuna mahakama nyingine eneo hilo ambalo ilitumiwa na Chifu Salehe Biringi ambapo sasa jengo lake limekuwa likitumiwa kama ofisi ya Kata.

Aidha anasema wakati wa utawala wa hayati Mwalimu Julius Nyerere kulikuwa na uchifu wa mshahara ambapo machifu walikuwa wakienda Hazina wanapewa posho na mahakama hizo zilikuwa zikiendesha kesi za kimila pekee na kesi nyingine zilikuwa za Serikali. Lakini anasema baadaye machifu walianza kufanya kazi bila mshahara na Mahakama zikaondolewa mikononi mwao.

Anasema kuna tamko lilitolewa la kusitisha kazi za mahakama hizo ambapo mpaka leo majengo yamekuwa yakitumika kwa shughuli nyingine na hata katika maeneo mengi nchini mahakama hizo hazipo kutokana na kubomoka kwani zilijengwa miaka mingi iliyopita.

Mzee huyo bado anatamani utawala wa kichifu kurudi tena nchini kutokana na jamii kupuuza baadhi ya mila hata zile zenye manufaa, hali inayopelekea kuongezeka kwa vitendo viovu ikiwemo mauaji, ubakaji na hata wizi.

“Tunakoelekea Uchifu unaweza kurudi na mimi ninatamani urudi na kutambuliwa vyema kuliko ilivyo sasa kwani ulisaidia sana kupunguza matukio ya ajabu ajabu,” anasema na kuongeza kwamba kimsingi machifu wengi kama yeye bado wanatoa huduma kubwa kwa jamii ingawa hawalipwi chochote na Serikali.

Anasema kama angepata bahati ya kuonana na Rais Jakaya Kikwete angemueleza umuhimu wa kurudisha Uchifu kama baadhi ya nchi zilivyofanya ikiwemo Uganda. Anasema Uchifu una nafasi kubwa ya kupambana na mambo ya kisasa yasiyo na kwani mambo mengi mazuri ya kale yalipelekea watu kuishi kwa umoja na kuheshimiana.

Anasema hilo linachangiwa na watu kuiga utamaduni wa nchi nyingine huku wakisahau mila na desturi za makabila yao.

Anazitaja mila na desturi za Wagogo kuwa ni pamoja na kuwa na ndonya, kutoga masikio na kuvaa kaniki. Wiki ijayo tutaangalia zaidi mila hizo.

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi