loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Chimbuko la Coalition of the Willing Afrika Mashariki

Ilifika hatua ya baadhi ya watu kutamka kuwa ni afadhali Tanzania ijitoe na tugawane mbao, kama ilivyokuwa mwaka 1977. Kikwete aliona tunakoelekea ni kubaya na ni vizuri aweke bayana msimamo wa nchi yetu. Ndipo alipotaangaza “hatoki mtu hapa.”

Wasiwasi ulianza kujitokeza pale wakuu wa Uganda, Rwanda na Kenya walipokutana mara tatu bila ya kuishirikisha Tanzania. Nchi mbili au zaidi wanachama hazikatazwi kuwa na makubaliano au ushirikiano katika mambo ambayo hayamo kwenye Mkataba au Itifaki ya Jumuiya.

Pia wanaweza kukutana kwa mambo ambayo yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na nchi nyingine.

Kuna mambo yapatayo manane ya msingi yaliyoamuliwa kufanywa kwa lengo la kuendeleza utengamano wa EAC. Haya ni mambo ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya.

Mambo manne kati ya hayo manane hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au kupata ridhaa ya Jumuiya.

Hata hivyo Kikwete akauliza, “Iweje leo hao wakuu watatu waache kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ambayo sote ni wanachama?”

“Iweje nchi tatu wanachama ziamue peke yao kuanza kutekeleza? Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye hivyo?” aliuliza Kikwete.

“Je wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya Afrika Mashariki na je wanataka kuunda yao? Je wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia vitimbi tutoke?” akauliza.

Alisema walipoulizwa kwa nini wengine hatupo wakasema eti wao wametangulia na sisi “tutakapokuwa tayari” tutajiunga. Yaani wao wameunda Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing au COW). Hivi ni nani hayuko tayari?

Walitualika tukakataa? Haya ni maneno mazito aliyotamka Kikwete alipoweka wazi kuwa tutaendelea kushiriki katika shughuli za Jumuiya na kuimarisha utengamano kwa kuzingatia Mkataba wa Jumuiya na Itifaki zake.

Akaongeza kuwa tutahakikisha kuwa Jumuiya haidhoofiki wala kufa. Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyoshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo.

Hii si kusema kuwa Tanzania inakataza nchi wanachama mbili au tatu zisikutane na kuzungumzia mambo yanayowahusu wao. Tatizo ni pale maazimio yao yanapoingiliana na maazimio yaliyofikiwa na wanachama wote wa EAC.

Ni vizuri tujiulize nini hasa chanzo cha kutengwa kwa Tanzania na kuundwa kwa hiki kikundi cha COW? Kikwete aliweka wazi kuwa kuna mambo ambayo Tanzania haikukubaliana na wenzetu na ndio labda yamepelekea kututenga. Tumetofautiana kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira na uhamiaji.

Tumekuwa tukisisitiza tujenge Jumuiya hatua moja baada ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha EAC.

Tumewaambia kuwa hatuna tatizo la kuongeza kasi ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yoyote au kwenda kasi ya kupindukia. Kwani mkataba unaelekeza tuanze na Umoja wa Forodha, ikifuatiwa na Soko la Pamoja kisha Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.

Kwa maneno mengine, tunakataa kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla ya kukamilisha hatua zingine, kwani Shirikisho lazima lijengwe juu ya msingi imara ya utengamano wa kiuchumi kwa manufaa ya wanachama wote, yaani Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Kifedha .

Wachambuzi wengine wanaona kutengwa kwa Tanzania kulichangiwa pia na sera ya Tanzania ya kuwatimua wale wanaoitwa wahamiaji haramu chini ya Oparesheni Kimbunga.

Ni lazima tukubali kuwa rafu ilitumika katika oparesheni hiyo ya kijeshi, na kuwa wengine walikumbwa kwa makosa. Wengi wao walitoka Rwanda na Kenya, nao wakalalamika kuwa ili kuishi na kufanya kazi hapa nchini wanatakiwa kulipa ada ya Dola 2,000. Pia wamelalamika kuwa mchakato mzima wa kupata cheti unachukua zaidi ya miezi mitano.

Matokeo yake wengi wakabanwa katika mtego na kutimuliwa. Ndipo nchi za jirani zikalalamika kuwa tunadhoofisha na kuhatarisha Jumuiya. Kulikuwepo pia na tuhuma kuwa Tanzania ilikuwa inachelewesha utengamano wa EAC kwa kutokubaliana na wenzetu.

Na ndipo walipotutenga Mkutano wa kwanza mwezi wa Juni uliwakutanisha marais Museveni, Kenyatta na Kagame. Mkutano wao wa pili ulihudhuriwa na mawaziri kutoka Burundi na Sudan Kusini. Hapa wakaamua kuharakisha Shirikisho bila ya Tanzania.

Wenyewe wakajiita kundi la walio tayari, wasiotaka kucheleweshwa na Tanzania “isiyo tayari”.

Ndipo Mwenyekiti wa Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Mheshimiwa Adam Kimbisa, akatamka kuwa wale waliokuwa wakisema Tanzania inachelewesha majirani wake wanapotosha ukweli. Kimbisa akasema Tanzania haijawahi kukataa utengamano bila ya kutoa hoja zake za kimsingi. Hivyo ni vizuri kuzingatia hoja hizo badala ya kulaumu.

Kilichokuwa kinalaumiwa zaidi na majirani zetu hasa ni kukataa kwetu kuingiza ardhi katika mambo ya EAC.

Ardhi ni suala la kila nchi, lakini mswada wa sheria ulitungwa na kuburuzwa ili ardhi iwe chini ya EAC.

Tanzania ikakataa kuburuzwa, na kuanzia hapo tukalaumiwa kuwa hatutaki utengamano, bila ya kujali kuwa Tanzania ilitoa bure ardhi kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili ijenge makao makuu yake.

Kwa maoni na ushauri tuwasiliane kwa, 0713-562181.

foto
Mwandishi: Nizar Visram

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi