loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

China, Urusi, Ujerumani Mashariki za kwanza kutambua Mapinduzi ya Zanzibar

Kwa wakati ule dunia ilikuwa ikikabiliwa na vita baridi vya Mashariki vikiongozwa na nchi iliyokuwa Jamhuri ya Kisovieti ya Urusi na kundi la nchi za Magharibi lililokuwa likiongozwa na Marekani. Ushawishi wa mapema ulijitokeza katika kila kundi ambapo kwa wakati ule Zanzibar ilikuwa na uhusiano wa karibu na nchi za Urusi, iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki pamoja na Cuba.

Kwa mujibu wa aliyekuwa Waziri katika Serikali ya hayati Karume, Ali Sultani, Mapinduzi ya Zanzibar yalitambuliwa kwa mara ya kwanza haraka na nchi mbili ambazo zilichukua jukumu la kusaidia maendeleo ya Zanzibar.

Nchi zinazotajwa kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar haraka ni China na iliyokuwa Ujerumani Mashariki na kufuatiwa na Urusi ambapo katika kipindi cha harakati za ukombozi za Wazanzibari kudai uhuru, tayari vijana wa chama cha Afro Shirazi Party walikuwa wakipelekwa katika nchi hizo kwa ajili ya mafunzo mbali mbali ikiwemo ya kijeshi.

‘China na Ujerumani Mashariki, Urusi na Cuba ndiyo nchi za kwanza kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar... Nchi hizo pia zilijitolea kwa kiasi kikubwa kutupatia misaada na wataalamu wakiwemo wale wa kijeshi katika vikosi vyetu vya Ulinzi na usalama wa taifa na kikosi cha wanamaji cha KMKM,” anasema.

Sultani anasema hadi kufikia Aprili 26 mwaka 1964 ambapo Zanzibar iliungana na Tanganyika na kuzaliwa kwa taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tayari jumla ya nchi 18 zilishayatambua Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha anasema jumla ya nchi 9 zilifungua Ofisi za ubalozi kamili Zanzibar yakiwemo mataifa makubwa ya Marekani, Urusi, Ujerumani Mashariki, China, Uingereza na Ghana.

Akifafanua zaidi Sultani anasema katika bara la Afrika nchi ya kwanza kuyaunga mkono Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa Ghana na ilifanya hivyo tarehe Januari 28, mwaka 1964 na baadaye kufungua ubalozi kamili. Alitaja sababu iliyopelekea Ghana kuyatambua mapema Mapinduzi ya Zanzibar ni uhusiano wa asili wa viongozi wakuu wa nchi hizo katika kupigania uhuru akiwemo Mwalimu Nyerere, Karume pamoja na hayati Kwame Nkrumah.

Kwa mfano, anasema, Ghana ilikuwa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika kupata uhuru wake kutoka kwa Muingereza katika mwaka 1957 ambapo Rais Kwame Nkrumah aliwaalika baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika kuwapa mbinu na ujanja wa kudai uhuru.

“Nakumbuka kabisa Mzee Karume alialikwa kwenda Ghana na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa Zanzibar kwa ajili ya kupewa mbinu za kujenga mikakati ya kudai uhuru kutoka kwa Muingereza,” anasema.

Aidha mikutano ya PARFMECA kwa kiasi kikubwa ilisaidia kuwakutanisha viongozi hao ambao kwa wakati huo walikuwa katika harakati za kupigania uhuru, mikutano ambayo ilikuwa kwa ajili ya kudai uhuru.

“Nyerere, Kwame Nkrumah na Karume walikuwa na mawazo ya pamoja ambayo lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha kwamba bara la Afrika linakuwa huru na kwa wakati ule Nkrumah alikuwa na muelekeo wa mapema katika kupiga vita harakati za ukoloni wa Kingereza,” anasema.

Rais Nkrumah katika kuwaunga mkono wana wa Afro Shirazi alimleta wakili Swanzi kwa ajili ya kuwatetea wana ASP ambao walishtakiwa kwa mauaji katika fujo za Juni 1963. Kuanzia hapo marais na viongozi wakuu wa nchi mbali mbali duniani walikuwa na hamu kubwa ya kuitembelea Zanzibar na kujionea harakati zake za kupigania uhuru.

Miongoni mwa viongozi mashuhuri waliotembelea Zanzibar alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya watu wa China, hayati Chou En Lai Juni 5, mwaka 1965 ambapo aliwasili katika uwanja wa ndege wa Zanzibar na kulakiwa na Rais wa Zanzibar, hayati Abeid Amaan Karume na Makamu wa Pili wa Rais, hayati Rashid Mfaume Kawawa.

Wengine ni Rais wa Liberia Tubman, Mfalme Haille Selassia wa Ethiopia, Rais wa Misri, Gamal Abdell Naseer na Rais wa Yugo slavia, Broaz Tito. Ujerumani Mashariki ilisaidia ujenzi wa kwanza wa nyumba za maendeleo za kupigiwa mfano ziliopo Kikwajuni mjini hapa, ambazo mafundi wazalendo walipata ujuzi uliosaidia kujengwa kwa nyumba nyingine za maendeleo ziliopo Michenzani, Kilimani na sehemu nyingine za vijijini na Pemba.

Aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Makame Mzee anasema Ujerumani walileta meli kubwa ambayo ilibeba kila kitu cha ujenzi kwa ajili ya majengo ya Kilimani ikiwemo saruji na vifaa vingine.

“Ujenzi wa nyumba za Kilimani ni msaada mkubwa wa rafiki zetu Wajerumani ambao walitusaidia pia kwa upande wa Kikosi cha majini cha KMKM kutupatia vifaa vya kijeshi,” anasema. China kwa upande wake ilisaidia maendeleo ya Zanzibar ambapo ilijikita zaidi katika kusaidia ujenzi wa viwanda mbali mbali vya uzalishaji wa bidhaa.

Kwa mfano, China ilisaidia ujenzi wa kiwanda cha ngozi na viatu kilichopo Maruhubi mjini hapa, ambacho kilizalisha bidhaa zinazotokana na viatu vya ngozi. Aidha China ilisaidia ujenzi wa kiwanda cha Sigara, kiwanda cha sukari kilichopo Mahonda kwa ajili ya kupunguza tatizo la kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi.

“Wachina walitusaidia sana katika kutupa ujuzi wa ujenzi wa majengo mbali mbali pamoja na viwanda kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa muhimu za ndani,” anasema. Aidha China ilisaidia ujenzi wa Kiwanja cha mpira cha Amaan ambacho katika miaka ya 1972 kilikuwa ndiyo kiwanja kikubwa katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati.

Kiwanja hicho kilifunguliwa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Nyerere mwaka 1971. Ali Sultani aliyepata kuongoza Wizara ya Elimu na baadaye ile ya Afya anasema China ilitiliana saini makubaliano na Zanzibar kubadilisha wataalamu na madaktari katika fani mbalimbali kuja Zanzibar kufanya kazi.

Anasema madaktari wa kwanza wa Kichina walifika Zanzibar katika mwaka 1965 na kuanza kusaidia kutoa tiba kwa wananchi wa Zanzibar ambapo kwa wakati huo madaktari bingwa wazalendo walikuwa watano tu.

“Mpaka tunafanya Mapinduzi, daktari bingwa wa kutibu maradhi ya binadamu mzalendo nakumbuka alikuwa marehemu Kingwaba Hassan Kingwaba,” anasema Sultani.

Utaratibu huo wa madaktari bingwa wa China kuja Zanzibar umekuwa ukiendelezwa ambapo madaktari hao wapo katika hospitali zote kuu za Unguja na kule Pemba wapo katika Hospitali Kuu ya Abdalla Mzee ambayo ilijengwa kwa msaada wa nchi hiyo pia. Kuanzia mwaka 1967 hadi mwaka 2013 zaidi ya madaktari wa China waliokuja Zanzibar kwa ajili ya matibabu wamefikia 200.

Mwandishi wa kitabu cha historia ya hayati Abeid Amaan Karume na Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Shaaban, anasema Mapinduzi ya Zanzibar yalizusha mivutano kwa mataifa makubwa huku kila mmoja akitaka ‘kujipendekeza kwa Zanzibar’ na kukubalika. Shaaban anasema hayati Karume aliliona hilo mapema na katika kukata mzizi wa fitina alitangaza kufungwa mara moja kwa kituo cha upelelezi cha kijeshi cha Marekani kilichopo Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.

Kituo hicho kilichojulikana kwa jina la ‘Mercury project’ kwa ajili ya mawasiliano ya anga za juu kilifungwa rasmi Aprili 7, mwaka 1964. Aidha Karume alitangaza kufukuzwa kwa Balozi wa Marekani nchini Zanzibar, Frank Calucci na Ofisa wa Ubalozi Robert Gordon ambao walituhumiwa kufanya njama za upelelezi na kutaka kuipindua Serikali halali ya wananchi wa Zanzibar ikiongozwa na Karume Februari 16, mwaka 1964.

“Hayo ni sehemu ya maamuzi mazito yaliyochukuliwa na Rais hayati Karume kwa taifa kubwa la Marekani na kisha kutangaza Zanzibar kujiunga na Umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote,” anasema Shaaban.

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi