loader
Dstv Habarileo  Mobile
Daktari aichambua timu ya Madola

Daktari aichambua timu ya Madola

Tanzania katika michezo hiyo ilipeleka timu za ndondi, riadha, kunyanyua vitu vizito, judo, baiskeli, mpira wa meza na kuogelea, ambazo zote zilitoka mikono mitupu bila medali yoyote.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya, daktari aliyekwenda na timu hiyo Mwanandi Mwankemwa alisema kuwa, wachezaji wa timu ya Tanzania hawakuandaliwa kisaikolojia na kusababisha kushindwa kabla ya mchezo.

Alisema kuwa wachezaji wetu hawakuandaliwa vizuri kisaikolojia na ndio maana kama mabondia walikuwa wanaonekana kupigwa hata kabla hawajarusha ngumi hata moja. “Ukiwaangalia tu wachezaji wetu hata kabla ya pambano walikuwa wamepigwa kwani wengi wa mabondia wetu walikuwa wakipanda ulingoni hawarushi ngumi hadi wanapopigwa kwanza ndio nao wanaanza kuibuka,“ anasema.

Anasema hata katika michezo mingine pia kulikuwa kunaonekana wazi kuwa wachezaji wetu walikwenda katika michezo hiyo bila ya kuandaliwa vizuri kisaikolojia.

Wachezaji majeruhi:

Timu hiyo pia ilikwenda na baadhi ya wachezaji majeruhi huku wengine wakikumbwa na maumivu huko huko kabla ya kuanza kushindana katika michezo hiyo.

Mwanariadha Alphonce Felix ambaye alitakiwa akimbie mbio za mita 10,000 yeye hakushiriki kabisa baada ya kubainika kuwa alikwenda Glasgow akiwa majeruhi. Mwankemwa alisema kuwa Felix aliumia wakati wa mazoezi kule Ethiopia baada ya kubainika kuwa aliumia kifundo cha mguu na hakuweza kushindana.

Mchezaji mwingine ni muogeleaji Magdalena Mushi ambaye alipatwa na mafua makali, lakini alitibiwa na kupona huku Rahma Abdallah aliumia kiwiko baada ya kunyanyua kitu kizito. Bondia Furahisha Hamad aliumia kichwani baada ya kupigwa sana kichwani katika pambano bila ya majibu yoyote.

Mbinu za mchezo:

Anasema kuwa wachezaji wa Tanzania walionekana wazi kutokuwa na mbinu zozote za kiufundi na ndio maana wengine walianza vizuri lakini walishindwa kumaliza vizuri. Alitoa mfano wa ndondi kwa kushindwa kuanza ndondi hadi pale walipopigwa na mpinzani na ndio wanakurupuka na wao kuanza kurusha ngumi.

Imani ya watu:

Anasema kuwa imani nazo zilichangia kwani wakati ule ulikuwa ni kipindi cha mfungo na baadhi ya wachezaji waliendelea kufunga na wengine kujikuta wakiishiwa nguvu. “Wachezaji wetu wengi waliendelea kufunga hadi siku ya mchezo, kitaalamu siku tatu za kwanza za kufunga bado mtu anakuwa na nguvu lakini baada ya hapo, chakula mwilini kinakuwa kimeisha,“ alisema.

Anasema kuwa aliwauliza timu ya Pakistan kuhusu hilo walisema kuwa, wenyewe wachezaji wao walikuwa hawafungi wanapokuwa na ratiba ya kucheza, kwani wanakuja kulipia baada ya kumalizika kwa Ramadhani.

Lishe duni:

Wachezaji wetu wengi walionekana wazi kuwa na lishe duni kwani wengi walikuwa hawana nguvu. Pia kingine wachezaji wa timu ya Tanzania wakati wa michezo hiyo hawakuwa wakienda pamoja kula na badala yake ilikuwa ngumu kuwadhibiti wasile au wale kitu fulani. Anasema kuwa wachezaji wa timu za nchi zingine walikuwa wanakwenda kula pamoja na pia hiyo inaongeza mshikamano na ushirikiano katika timu.

Maoni na Ushauri:

Mwankemwa anashauri kuwa timu yoyote ya Tanzania itakayokwenda kushiriki mashindano nje ya nchi, lazima iwe na daktari na mtaalamu wa mazoezi. Mbali na hilo pia kuwepo na mtaalamu wa lishe, ambaye atasaidia wachezaji kupata lishe ya maana, ambayo itawasaidia kula vizuri na kuwawezesha kucheza vizuri pia.

Wachezaji wote hata wakiwa wamepiga kambi nje ya nchi wanatakiwa wote kurudi nchini kwa ajili ya kuagwa na kuondoka pamoja, hiyo itasaidia sana kuleta umoja katika timu. Wacheaji wote pia wafanyiwe majaribio kabla ya kwenda katika mashindano kwani wengine walipata vigezo hivyo muda mrefu huko nyuma.

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi