loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Daniel Manege: Mwandishi aliyemnyanyua JB

Lakini wapo watu muhimu pengine zaidi ya hao. Wao ndio wenye majukumu makubwa ya kumfanya mtu huyo kuonekana anajua kuigiza au kuimba kutokana na kile kinachofanywa nyuma ya runinga. Wiki hii nilipata nafasi ya kuzungumza na Daniel Manege ambaye ni mwandishi wa stori na muswada ‘skripti,’ pia mwongozaji wa filamu zote zilizompa umaarufu mwigizaji Jacob Stephen ‘JB.’

Filamu ambazo alishawahi kuzitengeneza na kuwa maarufu sana zaidi ya yeye mtengenezaji ni Bado Natafuta, Shikamoo Mzee, Nakwenda kwa Mwanangu, Dereva Tax, Fikra Zangu, Zawadi Yangu, DJ Ben, Nipende Monalisa, Ukurasa Mpya na zingine ambazo kwa namna moja au nyingine zimeifanya Kampuni ya Jerusalem leo kuwa juu.

Filamu zote hizo zimeweza kufanya vizuri kwenye tasnia ya filamu, huku zingine zikipata tuzo mbalimbali, lakini hakuna mtu aliyewahi kufikiria kama filamu hizi huandikwa.

Manege alizungumzia lengo la kuingia kwenye tasnia ya filamu baada ya kuacha kufanya kazi aliyohitimu ya uhandisi wa viwanda katika ngazi ya shahada aliyomaliza mwaka 2010 aliyosomea kwa miaka minne katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM); hatimaye kuwa mwandishi mzuri wa filamu za Kitanzania, tena zenye umaarufu mkubwa.

“Niliingia kwenye tasnia ya filamu kwa kutaka kufuta msemo wa waigizaji wengi hawajaenda shule,” alisema Manege. Alisema baada ya kuhitimu elimu yake hiyo, alifanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja, huku akiwa mpenzi wa filamu za Kitanzania pamoja na vitabu mbalimbali.

Alisema alianza kuvutiwa na kazi za filamu na hatimaye aliamua kuachana na kazi yake mwaka 2011, aliandika filamu yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la You, Me and Him. “Filamu hiyo ya kwanza kuiandika ilikuwa kupima kile ambacho ninataka kukifanya kwenye tasnia ya filamu,” alisisitiza mwandishi huyo.

Baada ya kumaliza filamu hiyo, anasema alimpelekea JB ambaye aliipokea na baadaye kuifanyia kazi akiwa na Kajala Masanja na Issa Mussa ‘Cloud 112’. Hivyo anasema alishatengeneza filamu nyingi, lakini katika filamu zote ambazo zimepata umaarufu, filamu ambayo ilimsumbua zaidi ni ile ya Nakwenda kwa Baba yangu, aliyofanya JB na Amri Athuman ‘King Majuto.’

“Nilifanya kazi hiyo wakati ndio nilikuwa naacha kazi ofisini, nikaona ni bora niandike kama vile narudi nyumbani,” alifafanua Manege. Anasema lakini alipompelekea JB, aliipenda na kusema aibadilishe na aiandike Nakwenda kwa Mwanangu ili aigize na Mzee Majuto. Anasema hapo ndipo akili ilipoanza kumuuma kuibadili stori kutoka kwa mtoto anarudi kwa baba yake, na kuwa baba ndio anakwenda kwa mwanawe, jambo ambalo lilimchukua wiki tatu kuifikiria stori jinsi itakavyokuwa.

Anasema baada ya kufanya vizuri kwa filamu hiyo, ndipo akaanza kuwa na moyo wa kujifunza zaidi kwa kuamua kusomea kozi fupi fupi ili kuongeza uwezo wake juu ya filamu. Anasema alianza kuhudhuria semina mbalimbali zinazohusu masuala ya filamu ikiwemo zile zinazotolewa na Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) au Tamasha la Nchi za Majahazi.

“Nilikuwa na hamu ya kupata elimu zaidi kuhusu filamu hiyo, nilijaribu kusoma kila siku ili niweze kuleta mabadiliko,” alifafanua. Manege anasema alianza kuandika filamu nyingi ambazo zina vichekekesho, lakini pia zina mafunzo ambapo walizipa jina kama ‘Romantic Comedy’ ambazo ndizo zilizoanza kufanya vizuri zaidi.

Anasema kwa muda wote huo alikuwa akifanya kazi chini ya Kampuni ya Jerusalem iliyo chini ya JB, lakini kwa sasa ameamua kubadilika na kuanza kufanya pia na kazi zake mwenyewe. Lengo lake kubwa anasema siyo yeye kuigiza, isipokuwa kutoa wasanii wakubwa na wenye manufaa ili na wao watayarishaji, waandishi na waongozaji waje wajulikane na wawe na manufaa kwa kile ambacho wanakifanya.

“Mimi siyo mwigizaji ila nina mikakati ya kutoa wasanii wakubwa na wenye uwezo kulingana na stori zetu tutakavyozitengeneza,” alisema mwandishi huyu wa filamu. Anasema mpango huo alikuwa nao kwa muda mrefu, lakini alimkosa muda wa kujipanga, lakini hivi sasa anasema ameanza kupata msaada kwa baadhi ya watu ili kutimiza ndoto zake.

Anasema kiu yake ni kuona wasanii wapya wanaibuka na wanakuwa katika kiwango cha kimataifa, jambo ambalo anatamani kila siku kuliona linafanikiwa. Kwa sasa amesema akiwa na Kampuni ya Global Education ambayo ndiyo inamsaidia, ameandaa filamu ya Safari ya Gwalu ambayo itakuwa ni ya kwanza kutoka katika mikono yake.

“Mara nyingi nimekuwa nikiandika filamu na kuiongoza, lakini nilikuwa si mali yangu, hii ni ya kwanza kutoka kwangu,” anasema na kuongeza katika filamu hiyo atakuwa na wasanii wakubwa wawili akiwemo Salim Ahmed ‘Gabo’ na Juma Rajabu ‘Chacha.’ Pia alisema atachanganya na watoto ambao amewafanyia uchaguzi katika shindano maalumu la kumtafuta mtoto anayeweza kuigiza katika filamu hiyo.

“Nahitaji pia kukuza vipaji vya watoto hivyo nimeona niite shindano dogo kwa ajili ya kuchagua watoto wenye vipaji ili kuwaingiza katika filamu hiyo,” alisema. Alisema tayari watoto ambao amewatafuta ameshawafanyia uchunguzi na sasa yupo kwenye mikakati ya kuangalia ni yupi na yupi wanahitajika katika filamu hiyo.

Anasema watoto atakaowapata ndio hao atakaokuwa nao kama atahitaji kufanya filamu yoyote na watoto, kwa kuwa ana malengo marefu juu ya kukuza filamu za Tanzania. Daniel Manege, mwandishi wa filamu kali za Jerusalem, alizaliwa mkoani Tanga, na kusoma Shule ya Msingi ya Mgulani, Temeke, Dar es Salaam na kisha Kisarawe Junior Secondary wilayani Kisarawe, kabla ya kuhitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Old Moshi.

Mwaka 2006, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na kuhitimu mwaka 2010 katika Shahada ya uhandisi wa viwandani.

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya ...

foto
Mwandishi: Mohammed Mussa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi