loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dar yashika kasi, uandikishaji BVR

Hata hivyo, baadhi ya vituo vilivyoko kwenye maeneo yenye watu wengi, makundi ya vijana yamegeuza tatizo la foleni kama kitegauchumi kwa kuuza namba wanazowahi kwa watu wasioweza kuvumilia kupanga foleni. Kazi ya kuboresha daftari la kudumu la wapigakura katika jiji la Dar es Salaam imeanza Julai 22 na inatarajiwa kumalizika Julai 31, mwaka huu.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili jana katika Manispaa tatu za Jiji la Dar es Salaam ambazo ni Temeke, Ilala na Kinondoni umebaini kuwapo kwa misururu mirefu ya wananchi hususani katika maeneo ambayo yana wakazi wengi huku wananchi hao wakionesha kutokata tamaa.

Katika vituo vingi, licha ya wananchi kujitokeza kuanzia mapema alfajiri, na kuwapo kwa changamoto ya mashine kushindwa kufanya kazi kutokana na kupata joto, wananchi hawakuondoka.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema changamoto ya foleni kwa Dar es Salaam ilitarajiwa kutokana na mkoa kuwa na wananchi wengi ukilinganisha na mikoa mingi.

Alisema hata hivyo, Tume ambayo imekuwa ikitumia mashine 8,000 kukamilisha kazi ya kuwaandikisha wananchi imejitahidi kufanya zoezi hilo kwa ufanisi.

“Maeneo mengi, kazi ya uandikishaji imekuwa ikienda vizuri, lakini kuna baadhi ya maeneo hususani yale yenye wakazi wengi yamekuwa na changamoto ya foleni na kuwa tayari Tume imeshaongeza idadi ya mashine katika maeneo hayo,” alisema.

Aidha, Lubuva ameelezea kusikitishwa na namna vyombo vya habari vinavyoandika kazi ya uandikishwaji na kuonekana kuchochea vurugu wakati kazi hiyo ikiendelea vizuri katika maeneo mengi.

“Pamoja na kufanya vizuri katika maeneo mengi, vyombo vya habari sio rafiki katika kusaidia shughuli hii, changamoto zinazotokea za mashine kutotambua alama za vidole, au kupata hitilafu hata kwa walioanza kutumia mfumo huu walizipata,” alisema.

Namba zageuzwa biashara

Kutokana na kuwapo misururu mirefu na baadhi ya wananchi kutokuwa wavumilivu, baadhi ya vijana wameigeuza kero ya foleni katika vituo kama sehemu ya kujipatia chochote, kwani katika baadhi ya maeneo wamekuwa wakiamka alfajiri kuwahi foleni na wakishapata namba huziuza kwa watu wenye haraka kuwahi kwenye shughuli zao.

Katika kituo cha Tabata Shule, vijana hao wametajwa kuwa huuza namba kwa watu wasiotaka usumbufu wa kukaa foleni kwa kati ya Sh 5,000 hadi Sh 10,000.

Hali kama hiyo pia ilijitokeza katika kituo cha uandikishaji Sinza, jambo ambalo liliwafanya maofisa wa Tume kubadili utaratibu na kuzuia utoaji wa namba ambao ulikuwa ukifanywa na baadhi ya vijana.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamekuwa wakiibua mbinu mbalimbali za kutaka kupata urahisi wa kuandikishwa kwa wanawake kubeba watoto, huku wengine wakijifunga bandeji na wengine kwenda na vyeti au faili la X-ray ili kuonesha uhitaji wao na kupata huduma kwa haraka.

Aidha, baadhi ya vituo wameshtukia mchezo huo, hivyo kama mama amefika na mtoto wake, wamekuwa wakilazimisha amnyonyeshe ili kuthibitisha kama mtoto huyo ni wake.

Uandikishwaji

Waandishi wa gazeti hili waliopita katika baadhi ya vituo mbalimbali, walibaini kuwapo kwa ongezeko la mashine za BVR, jambo ambalo limerahisisha kazi hiyo kwenda haraka na kuongeza idadi ya wanaoandikishwa kwa siku.

Huko Temeke, katika vituo viwili vya Shule ya Msingi Tandika, gazeti hili limeshuhudia ongezeko kwa mashine na kuwapo mashine nane, jambo ambalo limeongeza kasi ya uandikishaji huku kituo cha Shule ya Sekondari Tandika kikiwa na mashine mbili na idadi ya watu walikuwa wa wastani.

“Hapa kwetu mashine ni nyingi na wananchi wanaendelea kujiandikisha vizuri japokuwa kuna changamoto kadhaa ambazo zimejitokeza ikiwemo baadhi ya wananchi kutofuata utaratibu na kutaka kujiandikisha bila kufuata foleni na utaratibu ambao tumejiwekea,” alisema mmoja wa kiongozi wa serikali ya mtaa ambaye ni mwangalizi katika kituo cha unadikishaji. Katika kituo cha Wailesi, wananchi waliojitokeza walionekana kuwa watulivu kwenye foleni wakati kazi hiyo ikiendelea.

Wilaya ya Kinondoni kulikuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi waliojitokeza kwenda kujiandikisha kwa siku ya jana kutokana na wengi wao kusema kuwa wameamua kutumia muda huo wa mapumziko ya wiki kupata vitambulisho vya kupiga kura.

“Mimi nimekuja leo na nimefurahishwa na utaratibu ambao unafanyika hapa, ukifika unaulizwa kama wewe ni mwenyeji wa hapa na unaandikwa jina. Nina imani nitapata kitambulisho changu leo,” alisema mkazi wa Tandale, Hamis Juma aliyefika kujiandikisha katika kituo cha kujiandikisha cha Muharitani eneo la Tandale.

Kwa upande wa kituo cha Tandale Magharibi, kulikuwa na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha wakiwa kwenye misururu mirefu. Katika kituo cha Mwananyamala Kisiwani, kulikuwa na idadi kubwa ya wananchi waliokuwa wamejitokeza aneo hilo.

“Tumefika hapa tangu saa 12 asubuhi, lakini mpaka muda huu (saa saba mchana) tulikuwa bado tuko kwenye foleni ndefu hasa kutokana na eneo letu kuwa na watu wengi na mashine hizi hazitutoshi,” alisema Paulina John.

Aidha, katika vituo vya Tandale, viongozi wa Serikali za mitaa waliweka utaratibu wa kuhakiki majina ya watu wanaokwenda kujiandikisha ili kuondoa tatizo la watu wasio raia na kutoka maeneo mengi kutotumia eneo hilo kujiandikisha.

“Hapa tunahakiki kila jina la mkazi anayekuja ofisini kwetu tuna majina ya wakazi wa eneo letu, na pia kuna watu ambao ni wahamiaji ambao wana umoja nao tunawatambua, sasa mtu ambaye si raia akija kujiandikisha hapa kwetu na kumbaini tunamchukulia hatua za kisheria,” alisema kiongozi huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Hata hivyo katika kituo hicho na kituo pacha na Mwananyamala Kichangani kulikuwa na utaratibu wa kutengwa mashine moja inayowahudumia wajawazito, mama wenye watoto, walemavu na wenye dharura mbalimbali.

Katika wilaya ya Ilala shughuli ya uandikishwaji ilikuwa shwari kukiwa na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha na kuongozwa na viongozi wao wa serikali za mitaa waliokuwa wakiita majina ili kuepuka wananchi wa maeneo mengine kujiandikisha.

Mmoja wa kiongozi wa serikali wa mtaa eneo la Buguruni, Juma Hassan alisema zoezi linaenda vizuri na pia wameweka utaratibu ambao unawawezesha watu wa makundi maalumu kama vile wazee, walemavu na akina mama wenye watoto kujiandikisha na kupiga picha kwa haraka zaidi.

“Hapa leo tulitoa namba 200 za wananchi wa kawaida na zingine 60 kwa makundi maalumu. Makundi maalumu tayari tumeshawaandikisha wote na wameondoka, hakuna aliyeleta fujo na kila mtu aliyepo hapa anafuata utaratibu vizuri,” alisema Hassan.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi