loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Dodoma na changamoto za wananchi kujiunga CHF

Mkazi wa kijiji cha Mkoka Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma, Thomas Dulle, anataka kuwe na mkataba kati CHF na wananchi waliojiunga ili pale ambapo kutakuwa na ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma waweze kushtaki mfuko huo.

“Sasa tunalazimishwa kujiunga na CHF kila kaya lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa dawa mara mtu anapougua na kwenda zahanati au kituo cha afya,” anasema. Dulle anasema kama kutakuwa na mikataba ya kuwachukulia hatua CHF wanapokosa huduma kutasaidia mfuko huo kutimiza wajibu wake kikamilifu kwa kuhakikisha dawa zinapatikana kwenye vituo vya afya.

Hata hivyo, Tito Chibango, anasema wananchi wamekuwa wakihamasishwa kujiunga na CHF, lakini wanapougua wanakosa dawa hospitalini lakini wale ambao wanalipia papo kwa papo wamekuwa wakipata dawa na hivyo kuona kama mpango huo hauna maana kwao.

Pamoja na changamoto hizo, miongoni mwa juhudi zinazofanywa katika maeneo mbalimbali nchini ni pamoja na kuhamasisha wananchi kujiunga kwa wingi na CHF kwani inaelezwa kwamba wananchi wengi wanapojiunga na mfuko ndiyo jawabu la dawa kupatikana kwa uhakika kwenye vituo vya afya.

Katika Mkoa wa Dodoma wananchi wamekuwa wakichangia Sh 10,000 kwa kaya ambayo huwezesha watu sita wa familia kupata matibabu kwa kipindi cha mwaka mzima. Japo kumekuwa na changamoto mbalimbali za wananchi kusita kujiunga na mfuko huo lakini elimu bado inaendelea kutolewa kwa lengo la kuhakikisha wananchi zaidi wanajiunga.

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Dodoma, Imelda Likoko, anasema wanaendelea na juhudi za kuhakikisha wananchi wengi wanapata fursa ya kujiunga na mfuko huo.

Pia anasema CHF imejizatiti katika kuhakikisha kunakuwa na dawa za kutosha katika vituo vya kutolea huduma na kwamba jambo la msingi ni wananchi kujiunga kwa wingi.

Anasema wakati mwingine ukosefu wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma unasababishwa na utendaji mbovu wa wasimamizi, hali inayozua malalamiko kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa siku ya wadau wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) na CHF uliofanyika hivi karibuni mkoani Dodoma, Meneja huyo anasema katika kipindi cha Julai 2009 hadi Juni 2013, CHF imeweza kuandaa mfuko wa ukusanyaji taarifa kutoka halmashauri.

Mfuko huo kwa sasa una taarifa muhimu zinazohusu utekelezaji wa CHF kwa wilaya zote ikiwemo idadi ya kaya zilizojiunga, viwango vya michango kwa kila halmashauri, mafao yatolewayo, utendaji wa bodi za afya za halmashauri na mashirika yanayosaidia halmashauri kuhusu CHF. Likoko anasema mfuko umefanya jitihada ya kuhakikisha elimu ya CHF inawafikia Watanzania wengi zaidi kwa kutekeleza programu mbalimbali za uhamasishaji.

Pia mfuko unaendelea kuboresha utunzaji wa taarifa za wanachama wa CHF na sasa umeanzisha kanzi data za CHF na kuchapisha rejister 6,000 za wanachama zitakazosambazwa katika vituo vya tiba ndani ya halmashauri.

Anasema mfuko huo unaendelea kutoa elimu kwa wadau vijijini, kata kwa kata ambapo hadi Juni 2013 hakuna wilaya ambayo elimu ya kata kwa kata haijafanyika na baadhi ya wilaya kata zake zote zimeshafikiwa angalau mara moja.

Pia takwimu za mfuko zinaonesha kwamba hadi kufikia Juni mwaka huu jumla ya kata 3,491 kati ya kata 3,335 zilizopo nchini zitakuwa zimehamasishwa.

Akielezea hali ya mfuko wa Afya katika Mkoa wa Dodoma, Meneja huyo anasema mpaka sasa jumla ya kata 222,410 zimejiunga.

Anasema Wilaya ya Chamwino inaongoza kwa kuwa na asilimia 17.4 ikifuatiwa na Wilaya ya Bahi yenye asilimia 16.5, Mpwapwa asilimia 15.3, Kongwa asilimia 15.3, Manispaa Dodoma asilimia 4.6, Kondoa asilimia 3.2 na Chemba asilimia 2.9. Kutokana na takwimu hizo inaaminisha ni asilimia 10.7 tu ya wakazi wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma ndiyo waliojiunga na CHF.

Akielezea changamoto za CHF anasema baadhi ya bodi za afya za halmashauri zimepitwa na wakati, uhamasishaji hafifu wa halmashauri kuhusu CHF na wakati mwingine si endelevu lakini bado juhudi zinaendelea kuhakikisha kaya nyingi zaidi zinajiunga ili kuondokana na changamoto ya ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Mafanikio ya mfuko huo ni pamoja na halmashauri zote kupatiwa hati rasmi na kupitisha sheria ndogo za halmashauri ukiondoa Wilaya ya Chemba iliyoanzishwa hivi karibuni.

Anasema bodi za afya za halmashauri zilishazinduliwa na kuelimishwa isipokuwa Wilaya ya Mpwapwa, pia baadhi ya halmashauri zimeomba tele kwa tele (mpango wa halmashari kuongezewa pesa na serikali) na kulipwa maombi yao ikiwemo Chamwino na Bahi.

Anasema Manispaa ya Dodoma na Kondoa bado hazijalipwa maombi ya tele kwa tele kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya taarifa.

Akielezea matarajio ya mfuko, Likoko anasema ni kuongeza idadi ya wanachama kwa kujumuisha makundi mengine katika jamii na kuendelea kutoa elimu ya bima ya afya kwa umma ikiwa ni pamoja na vikundi vya ushirika.

Matarajio mengine anasema ni kuhamasisha halmashauri ili zihamasishe wananchi katika sekta isiyo rasmi kujiunga na CHF na kuharakisha madai ya CHF ya tele kwa tele ili kuziwezesha halmashauri kuboresha huduma za matibabu.

Mengine ni kuendelea kusajili vituo vya huduma ikiwemo maduka ya dawa vijijini na kuendeleza ukaguzi wa vituo ili kuimarisha ufanisi na huduma bora, pia kuendelea kutoa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa vituo.

Anasema ni muhimu kwa halmashauri zote kuifanya CHF na NHIF kuwa ajenda ya mkoa kwa kuhamasisha zaidi na kuhakikisha bodi zinafanya kazi zao.

Pia halmashauri kusimamia vizuri matumizi ya fedha za NHIF, papo kwa papo na zile za malipo ya tele kwa tele ziweze kuboresha huduma ya afya kwenye vituo kama kununua dawa.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ezekiel Mpuya, anasema kuna halmashauri zinafanya vizuri na nyingine zinalegalega na kwamba jambo hilo linatakiwa kuangaliwa kwa makini ili kurekebisha mapungufu kwenye maeneo mengi kwa kuweka jitihada za kutosha.

Anayataja mambo hayo kuwa ni kama usimamizi wa matumizi ya dawa kwenye vituo ili kulinganisha idadi ya wateja, kiasi cha dawa kilichopokelewa na kiasi cha dawa kilichotumika.

“Eneo hilo likitilia mkazo tutajikuta tukiwa na na dawa nyingi," anasema.

Pamoja na hayo anasema malipo ya papo kwa bado kwenye maeneo mengi hayatiliwi maanani kwani wakati mwingine risiti za halmashauri zimekuwa hazitumiki na vituo na halmashauri nyingine hazijaweka viwango vya kutoza wananchi wanaohitaji kulipia papo kwa papo. Anasema kiwango cha papo kwa papo kinatakiwa kuwa kikubwa ili kuhamasisha wananchi kujunga na CHF.

“Kuna halmashauri zinawatoza wananchi hadi Sh 3,000 ili kuhudumiwa, hilo linawahamasisha kujiunga na CHF, lakini halmashauri za Dodoma hazima kauli moja kila mtu anatozwa kivyake kama ni Sh 500 au vinginevyo,” anasema. “Tumejenga maeneo kwa ajili ya dawa lakini wateja wanakosa dawa wakati kwenye dirisha maalumu kuna dawa za kutosha,” anasema.

Anasema katika sekta ya afya inahitaji msaada mkubwa kwa viongozi kama wakuu wa wilaya, madiwani na watendaji wengine. Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya mpya ya Chemba, Francis Isack anasema CHF iliacha sana wananchi katika suala la uhamasishaji.

“Uhamasishaji ufanyike kwa kutumia viongozi wa maeneo yao na hata madaktari ili kuhakikisha yale wanayoeleza yanakuwa sahihi. Hiyo itatoa imani kwa wananchi,” anasema.

Christopher Kangoye, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, anasema huduma za matibabu za mfuko wa NHIF, CHF, inahitajika sana kwa wananchi. “Lakini uwajibikaji haupo na badala yake watu wamejijengea tabia ya kulalamika, madawa hakuna nani anawajibika, mtumishi akibainika anasababisha kutopatikana dawa au awajibishwe; haitoshi kutoa maagizo, kama kuna tatizo lijulikane liko wapi,” anasema. Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa, anasema wananchi wengi wanasita kujiunga na mfuko huo kutokana na gharama ndogo za kuchangia papo kwa papo pindi anapougua.

“Mwananchi anaona hata akiwa hana kadi ya CHF akiwa na Sh 3,000 anatibiwa,” anasema. Mkwasa anasema watumishi wenye zahanati na vituo vya afya wanaipenda sana papo kwa papo kwani wanakusanya fedha wanazotoa wananchi wanapofika kutibiwa hivyo kuona hata kama watu wakijiunga au wasipojiunga ni sawa tu.

Pia Mkuu huyo wa Wilaya anataka kufanyika kwa ukaguzi wa kushtukiza kwenye maduka ya dawa yaliyo karibu na hospitali ambayo yamekuwa wakimilikiwa na watumishi wa afya.

“Watumishi wengi wa vituo vya afya na zahanati wana maduka ya dawa na dawa nyingine wanazouza ni za wizi. Mgonjwa akienda hakuna dawa na anaelekezwa duka la kununua,” anasema.

Anasema jambo la msingi ni kuangalia namna ya kudhibiti tatizo hilo, la mtumishi na duka la dawa karibu na eneo analofanyia kazi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi amesema kuna umuhimu kwa serikali za vijiji kutunga sheria ndogondogo kushughulikia wananchi ambao hawataki kujiunga kwa makusudi na CHF. Dk Nchimbi anasema serikali za vijiji zinatakiwa kuwa na sheria ndogondogo ambazo watazisimamia ili wananchi wajiunge na CHF ili wawe na uhakika wa kupata matibabu mwaka mzima.

Anasema wananchi wanapokuwa na uhakika wa matibabu wanakuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, ikiwemo kilimo na shughuli nyingine za uzalishaji.

Anasema licha ya elimu kutolewa baadhi ya wananchi wamekuwa wagumu kujiunga na mfuko huo na hivyo kunatakiwa jitihada za ziada ili kuhakikisha wananchi wanahamasika. Anasema bila afya mtu hawezi kuwa na maendeleo ya kiuchumi, kielimu na hata tambo za kisiasa hazitakuwepo kwani hata ukiwa na bajeti kubwa kiasi gani unapoingia kwenye mgogoro wa kiafya bajeti yote inasambaratika. Mkuu wa Mkoa anasema katika mkoa wa Dodoma ni asilimia 10.7 ndiyo waliojiunga na CHF. “Hii inamaanisha kuwa asilimia 89.3 wako wapi? Huwezi kujivuna kama kuna mafanikio kwa wananchi kujiunga na CHF bila kuangalia kwa nini asilimia kubwa bado wako nje," anasema. Anasema kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha wanazingatia afya zao kwa kuhakikisha wanapata matibabu pindi wanapougua ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

“Inawezekana tatizo la ukosefu wa chakula katika Mkoa wa Dodoma linatokana na watu kutokuwa na uhakika wa afya zao ambao wameshindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo,” anasema.

Pamoja na hayo anataka watendaji kuangalia na kufuatilia kwa makini ili kufahamu kwa nini watu hawataki kujiunga na CHF licha ya kuwa sasa kumekuwa na mpango wa kuhamasisha wananchi kufuga kuku ili wawe na uhakika wa kupata fedha za kujiunga na CHF. Anasema sasa wanataka kuangalia thamani ya kuku katika kuleta ustawi ngazi ya familia kwani mkakati kama huo unaweza kusaidia watu wengi zaidi kujiunga.

Anataka watendaji wa mfuko huo kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa zinakuwa bora kwani lawama huwa haziendi kwa mfuko bali kwa serikali iliyopo madarakani.

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi