loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dogo Aslay atoka kivingine

Kila siku utawasikia wanasema mimi maisha yangu na muziki, na wengine wanasema mimi maisha yangu ni kuigiza, lakini hawana mpango wa kwenda kuongezea elimu ya hicho wanachosema ni maisha yao. Lakini hali ni tofauti kwa mwanamuziki mdogo aliyemaliza elimu yake ya sekondari katika Shule ya Temeke iliyopo Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Aslay Sadiq maarufu kwa jina la ‘Dogo Aslay’.

Akizungumza na gazeti hili, Dogo Aslay alieleza jinsi alivyojipanga baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari katika shule hiyo na mikakati yake mipya. Anasema wasanii wengi wa Tanzania, wanatamani kufanya kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri kupitia muziki, lakini wengi wao wanasomea mambo mengine na kuanza muziki kwa kusema wao wana vipaji.

Lakini anasema yeye amefikiria tofauti sana kwani lengo lake kwa sasa ni kwenda kusomea muziki kabisa na sio kufanya muziki wa kubabaisha. Anasema ingawa hajajua ni chuo gani atakwenda kusomea, lakini pendekezo kubwa lipo kwenye kusoma muziki Zanzibar ambako anaamini wapo wakongwe wa muziki tofauti.

“Nimepanga kutafuta chuo kikubwa cha muziki inawezekana ikawa Bagamoyo au Zanzibar, na elimu yangu ianzie kwenye muziki na hata kama kuna vitu vingine vitafuata,” anasema msanii huyo. Anasema wakati alipokuwa katika shule hiyo, alitunukiwa Tuzo na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema akiwa kama shujaa wa shule na mwanafunzi mwenzake wa kike ambaye alikuwa akijishughulisha na masuala ya urembo.

“Tulitunukiwa tuzo hiyo kutokana na sisi kuwa wanafunzi pekee ambao tumefanikisha kuitangaza shule kutokana na vipaji vyetu,” alieleza. Kwamba kutokana na heshima aliyopewa na mkuu huyo wa wilaya, kumemfanya afikirie zaidi juu ya muziki na jinsi anavyoweza kutumia muziki katika maisha yake yote.

Anasema ingawa kimafanikio si makubwa sana katika muziki huo, lakini imeweza kuonesha nuru kubwa katika maisha yake ikiwemo kusaidia wazazi wake. Aslay anasema kwa sasa muziki umeweza kumsaidia kukutana na watu maarufu na viongozi ambao kwa kawaida ingekuwa ngumu sana kuonana naye na hata kumpa jina kwa watu wengine.

Anasema kingine ambacho anaweza kujivunia kupitia muziki ni kutembea nchi nyingi za Afrika na nje ya Afrika, jambo ambalo Watanzania wengi hawajafika na wala wengine hawategemei kufika nje ya nchi. “Mwanzo sikuwa na lengo la kufika hata Kenya, kwa maana nilikuwa najiuliza nifuate nini? Tofauti na sasa najua nchi yoyote naweza kwenda kufanya matamasha kulingana na kazi yangu,” anafafanua.

Anasema pia anajivunia kuwa miongoni mwa wanamuziki wa kwanza wadogo kushiriki katika Tuzo za Kora mwaka jana kutokana na wimbo wake ni Nataka niwe nawe. “Tuzo hizo wasanii wengi si Tanzania ila Afrika nzima wapo wanaotamani kushiriki, lakini wanakosa nafasi hiyo. Lakini mimi niliweza kushiriki ingawa sikushinda,” anasema Dogo Aslay.

Kuingizwa kwake kwenye tuzo hilo, anasema kumemuongezea nguvu kwa kuamini ipo siku anaweza kufanya vizuri na hata kuchukua moja ya tuzo hizo maarufu zinazofanyika Afrika. Aslay anasema kupitia muziki, amefanikisha kumjengea nyumba mama yake ingawa haijaisha kabisa, lakini kwa sasa ipo sehemu mzuri kukamilika.

Pia anaweza kukidhi mahitaji yake muhimu na familia, jambo ambalo bila muziki huo asingeweza. Anasema kwa sasa lengo lake kubwa ni kumiliki bendi ingawa kwa sasa tayari wameshazindua bendi yao mpya ya Mkubwa na Wanawe iliyozinduliwa Machi 2, mwaka huu katika Maisha Club, Dar es Salaam.

“Bendi imekamilika, ni bendi mpya tukiwa na wasanii wakali na sasa tunaanza kazi,” anasema. Aslay anasema lengo lao kwa sasa ni kuitangaza zaidi bendi hiyo kwa kutoa nyimbo mpya. Anasema ingawa kwa sasa watu wanaijua zaidi kupitia wimbo wao Yamoto, lakini tayari wameshaanza kurekodi nyimbo nyingine kwa ajili ya kuipa nguvu na kuleta ushindani katika bendi nyingine.

“Ingawa kwa sasa tuna lengo la kuikuza bendi yetu, lakini pia tunaangalia mtu anahitaji nini kutoka kwetu. Anahitaji bendi au anahitaji muziki wa CD,” anafafanua zaidi. Anasema kwamba wapo watu wanahitaji muziki na kwa kuwa hawana fedha za kulipia muziki wa moja kwa moja ‘live,’ jambo ambalo wanatumia CD katika kupiga muziki huo.

Lakini anasema wapo wengine wao wanapenda muziki wa bendi, hivyo wapo tayari kugharamika ili wapate muziki huo kupitia kwenye shughuli zao au katika baa.

“Tupo tayari kwa kupiga mziki wa aina yoyote, watu wasijali kuhusu sisi na wala kuhusu bendi, tunajadiliana,” anaeleza Aslay na kuongeza kuwa akipata mafanikio makubwa, anatamani siku moja amiliki bendi yake mwenyewe, kutokana na kutamani maisha yake yawe katika muziki zaidi.

Aslay Sadiq ni mzaliwa wa Temeke aliyemaliza shule ya msingi sekondari wilayani humo. Wimbo uliompa umaarufu mkubwa ni ‘Naenda kusema’ aliofanya chini Kampuni ya Mkubwa na Wanawe, akiwa chini ya meneja wake, Yusufu Chambuzo na Mkurugenzi wa kundi hilo na kundi la TMK, Wanaume Family, Saidi Fela ‘Mkubwa.’

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Mohamed Mussa

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi