loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

EAC: Wenzetu wameghafilika, tuwazindue

Tofauti na talaka zinazotolewa siku hizi, ukifuatilia mafundisho hayo kwa usahihi wake, hadi talaka kutolewa, ni lazima mambo mengi yawe yamepitiwa kwa kuanzia na ukubwa wa kosa lenyewe.

Wakati siku hizi makosa kama ya mke wa mtu kugombana na mawifi zake, kushindwa kumpikia mume na mengine ya kipuuzi kama hayo yanaweza kuwa sababu za talaka, mafundisho ya Kiislamu yanaonesha makosa makubwa mawili ndio yanaweza kumfanya mtu kufikiria kutoa ama kuomba talaka; kosa la kuzini ndani ya ndoa na au mwanandoa mmoja kuasi amri halali za Mwenyezi Mungu.

Kadhalika, ili talaka ‘halali’ itolewa ni lazima taratibu kadhaa ziwe zimefanyika; mashauriano ya wanandoa kwa wanandoa, ushauri wa kadhi aliyefungisha ndoa, wazazi wa pande zote mbili kukutana na hata wanandoa kuhamana vyumba, lengo likiwa kupata muda wa kufikiria upya, huenda aliyekosa akajirudi baada ya kugundua neema anayoikosa kwa mwenzie.

Kwa mujibu wa mashehe, kama aliyekosewa atasamehe kwa lengo la kuokoa ndoa, basi ni jambo linaloaminika kumfurahisha sana Mwenyezi Mungu na huyo hupata thawabu nyingi. Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unapita katika mtikisiko mkubwa kutokana na washirika wengine wa jumuiya hiyo kwa maana ya nchi za Tanzania na Burundi kutengwa na wenzao wa Kenya, Uganda na Rwanda.

Hata wiki iliyopita, kulikuwa na habari inayoonesha kwamba ‘wanaojitenga’ walikuwa wanafanya kikao kingine bila kuwashirikisha wenazao wa Tanzania na Burundi, ambazo kwa pamoja zinaunda Jumuiya hiyo. Sijui kwa nini Burundi nayo inatengwa, lakini sababu za kutengwa kwa Tanzania zimetajwa na watu kadhaa ikiwa ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe.

Moja ya sababu hizo inaelezwa kuwa ni Tanzania kuonekana kama inasuasua katika kurahakisha baadhi ya malengo ya jumuiya hiyo. Yaani nchi zingine zinataka hatua za kuelekea kwenye shirikisho la kisiasa zifanyike haraka lakini Tanzania imekuwa haitaki papara katika jambo hili. Kila uamuzi lazima ijipe muda wa kuutazama na kuurudisha kwa umma kupata baraka kabla ya kusonga mbele.

Lingine linalotajwa ni Tanzania kugomea ardhi yake kwamba iendelee kutawaliwa na sheria za Tanzania. Zipo taarifa kwamba baadhi ya nchi hizi zina tatizo la ardhi na zilikuwa zikiimezea sana mate ardhi ya Tanzania na hivyo uamuzi wa Tanzania umekuwa ‘kigingi’ kwao.

Sababu nyingine inayotajwa ni uamuzi wa Tanzania ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kupeleka majeshi ya kulinda amani nchini Kongo. Zimekuwepo tuhuma za muda mrefu kwamba nchi za Rwanda na Uganda zina maslahi nchini Kongo yanayobebwa na waasi waliokuwa wakisumbua nchini Kongo kwa muda mrefu, lakini zenyewe zimekuwa zikikanusha.

Nchi inayonyooshewa kidole zaidi ni Rwanda. Kuna lingine linatajwatajwa kwamba eti viongozi wa mataifa yenye nguvu kama Marekani na China kupishana kuja kuitembelea nchi hiyo kutokana na kuvutiwa na raslimali zake, amani na uongozi thabiti, imewakera pia majirani wake hao na kuamua kujitenga.

Kama zipo sababu nyingine sijasikia ama zimejificha lakini hizi ndizo zinazotajwa tajwa, ingawa mimi ninaamini kwamba sababu kubwa ni jumuiya hii, ingawa inatajwa kwamba itakuwa ya wananchi kwa maana ya kutegemea mawazo na uamuzi wao, lakini imeendelea kuwa ya viongozi kuliko umma wa wananchi wa eneo hili la Afrika Mashariki.

Ingawa Watanzania miaka michache iliyopita walihofia kuchukuliwa ardhi yao pamoja na ajira na wageni, walipohojiwa idadi kubwa walionesha kwamba wanaipenda jumuiya.

Ninaamini ukiongea leo hii na wananchi wa kwaida wa nchi za Kenya, Rwanda na Uganda watasema wanaipenda jumuiya, na hivyo hisia zangu zinanielekeza kuamini kwamba katika mikakati ya kuanzisha jumuiya ndani ya jumuiya kama hali inavyojionesha, ni misimamo ya viongozi wa nchi hizo na siyo wananchi wa nchi hizo.

Kwa mantiki hiyo, kama hizo hapo juu ndizo sababu za wenzetu kutaka kujitenga, labda wakijisadikisha kwamba watafaidika mbali bila Tanzania na Burundi kwa vile wanaweza kujenga reli yao kutoka Mombasa hadi Kigali, wakaungana na Sudani ya Kusini na kujenga bomba la mafuta hadi Mombasana na mengine mengi, bado ni sababu ambazo hazijai kwenye kiganja.

Ingawa, kama nilivyodokeza hapo juu, talaka ni ruksa inayomkasirisha Mwenyezi Mungu, bado sababu hizo, kama hakuna nyingine nzito, na siamini kama zipo, hazina uzito wa kuwafanya hawa wenzetu wafikirie kututenga ama na sisi kufikiria kujiondoa.

Hawa ni sawa na mwanandoa mmoja aliyeghafilika, aliyerubuniwa na mpita njia, au aliyelewa neema na kujisahau alikotoka na hivyo anahitaji msaada wa kumkumbushwa kwamba ndoa yake ikivunjika atasababisha pande zote mbili, akiwemo yeye mwenyewe kukosa neema alizokuwa anazipata ama kuzitarajia.

Ni mwanandoa anayepaswa kukumbushwa na si kukimbia kwamba kuvunja ndoa yake kuna hasara kubwa kwa watoto (wananchi) kuliko anavyofikiri. Ukisikia baadhi ya maneno ya Watanzania wakiwemo baadhi ya wabunge, utaona wapo wanaotaka ikiwezekana tuchukue hatua mara moja kutoa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hata serikali juzi Bungeni imesimama itatoa msimamo baada ya siku mbili. Kimsingi uamuzi wa kujiondoa si mwafaka, licha ya ukweli kwamba hata hatua ya kufikiria tu kufanya hivyo bado sana haijafika. Sisi Tanzania yatupasa tuchukue kila juhudi kuhakikisha jumuiya haifi, hata kama ni kwa kuwabembeleza hawa waliojisahau kwa kuwakumbusha tena na tena kwamba sote tunategemeana.

Tuwambia pia kwamba kuna wenzetu katika jumuiya wanaotutegemea zaidi kuliko sisi tunavyowategemea. Tuchukulie mfano wa majirani zetu wa Kenya; wakati inasemekana katika bidhaa za viwandani ambazo sisi tunauza kwao ni Konyagi na dawa za meno zaidi lakini wao wana bidhaa lukuki za viwandani wanazotuuzia ambazo pia tunaweza kuzipata kwingineko.

Wakati sisi sehemu kubwa tuna chakula cha kutosha, wao wanatutegemea sana katika eneo hilo. Viongozi wa dini wanasema kwamba binadamu ana kasumba ya kusahau neema anayopata, mpaka anapoikosa. Yaani akiwa na anapokua na mkono anasahau kwamba ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na siku akiukosa ndipo atagundua umuhimu wake.

Vivyo hivyo, mtu aliye katika ndoa anaweza kugundua umuhimu mkubwa wa mwanandoa mwenzake pale atakapomkosa. Sisi tusiruhusu kufika kuvunjika kwa jumuiya na ndio maana ninashauri viongozi wetu wavae uvumilivu na kusaka vikao vya kuwakumbusha wenzetu wakumbuke neema watakazozikosa jumuiya ikivunjika.

Twende kuongea nao tukikumbuka wosia wa busara wa Mwalimu Nyerere aliyotuambia kwamba kuwatenga wenzako ni kunafanya dhambi ya ubaguzi ambayo haiwezi kuishia hapo. Lazima itakutafuna na hivyo sisi tukitaka kubaki salama ni kuhakikisha hatuchangii katika dhambi hii.

Tuwakumbushe wenzetu na sisi wenyewe kujikumbsha vilevile kile ambacho Mwalimu Nyerere na wenzake walikipigania katika Tume ya Kusini (South Comission). Tume hiyo ambayo maoni yake inaonekana hayafanyiwi sana kazi na viongozi wetu wa Afrika, iligundua kwamba Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara imetengwa na dunia, hivyo inapaswa kushirikiana sana yenyewe kwa wenyewe.

Mwalimu Nyerere alisema kwamba, nchi hizi majirani zinapaswa kwenda kusaka msaada ama soko nje baada ya kukosa kabisa ufumbuzi wa suala husika katika nchi zao ama kwa majirani zao. Akasema Tanzania, kwa mfano, kama inatafuta profesa wa mambo ya moyo, inapaswa kumtafuta kwa majirani zake na ikimkosa kabisa ndipo iende ughaibuni kwa maana ya Ulaya, Marekani ama Japan.

Tume hiyo ya Kusini, baada ya utafiti wake iligundua kwamba, Ulaya, Marekani na Asia kila siku zimekaa mkao wa kuinyonya Afrika na kwamba kuendelea kufanya nazo biashara badala ya kufanya biashara sisi kwa sisi, ni kuziongezea uwezo wa kututawala. Mwalimu Nyerere alisema inashangaza sana kuona nchi hizo ambazo zimeendelea katika kila nyanja, zinaungana, lakini sisi katika ‘vijinchi vyetu hivi’ tunahubiri utengano kama mazuzu fulani hivi.

Shime Watanzania. Huu ndio wakati wa kuonesha busara zetu, kuokoa jumuiya kwa sababu ya manufaa yake kwetu na vizazi vijavyo. Tuwakumbushe wenzetu kwamba, sisi na viongozi wetu wote tutaondoka lakini Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda zitabaki.

“MTU niliyefanya naye mahojiano alikuwa anafanya kazi kwenye ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi