loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Edward Kumalija: Wasanii wa mikoani huumizwa na soko

Wengi wa waigizaji wamekuwa wakifanya filamu, lakini kazi imekuwa wanapofika Dar es Salaam kutafuta soko, hapo ndipo wanapokutana na changamoto nyingine zinazotokana na wanunuzi wa kazi hizo. Miongoni mwa matatizo makubwa yanayotokana na wanunuzi wa filamu hizo ni kutaka wasanii fulani ambao wanawajua wao kuigiza katika filamu yako.

Wanachohitaji waigizaji wao kuigiza katika nafasi ambazo wao wanazihitaji katika filamu yako na kama ukishindwa kufanya hivyo, basi inakuwa imekula kwako. Mwigizaji mchanga wa filamu kutoka mkoani Mwanza, Edward Kumalija anaelezea jinsi alivyoweza kuteseka na baadhi ya kazi zake kutokana na masharti ya wanunuzi wa kazi hizo.

Kumalija anasema kwa mara ya kwanza alipotengeneza filamu yake iliyokwenda kwa jina la Nyanda ilipokamilika, aliamua kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta soko. Lakini anasema baada ya kufika alihangaika kwa muda wa mwaka mmoja, bila ya kupata nafasi ya kuchukuliwa kazi yake, ingawa kila kampuni aliipatia demo ya filamu hiyo.

“Nilitafuta soko kwa mwaka mzima,hadi nilipopata nafasi ya kuuiza katika moja ya kampuni ya usambazaji,” anasema Kumalija. Anasema kila kampuni aliyokuwa akipeleka kazi hiyo, walimtaka kuwa na msanii fulani ndiyo aigize, na wala hawakutaka wasanii ambao yeye aliwaweka.

Kumalija anasema kutokana na hali hiyo, ilimkatisha tamaa baada na kutamani hata kurudi nayo Mwanza, ndipo ikachukuliwa na kampuni ya usambazaji wa filamu Tanzania ya Pilipili Entertainment. “Kila kampuni ambayo utapeleka kazi yako, wanasema wanataka kuiona skripti kwanza, kabla ya kuiona filamu yenyewe,” anasema msanii huyo.

Anasema wanachotaka uwapelekee skripti ya filamu unayotaka kuitengeneza, wanaiangalia na kuikagua ndipo wanapokupangia wasanii gani wanaotakiwa kuwaingiza kwenye filamu hiyo. Wakishapanga wasanii hao, basi wewe kazi yako ni kwenda kuongea nao ili waigize katika filamu hiyo.

Lakini kama ukishindwa kufanya hivyo, filamu yako hawaipokei au watainunua kwa bei ya hasara, ambayo kamwe hutokubali. “Kila msanii mkubwa huwa ana gharama yake kulingana na nafasi anayocheza au kutokea, kwenye kava la filamu yako kwaajili ya mauzo,” anafafanua Kumalija.

Anasema lakini tatizo kubwa linakuja kwa msanii ambaye unataka aigize kwenye filamu yako, unaweza kupanga bajeti nzima na kutumia zaidi ya Sh milioni nane hadi tisa, kutokana na wasanii wakubwa kulipwa kuanzia Sh milioni mbili hadi nne kwa kila msanii. Wakati ukifika sokoni anasema wanaweza kukwambia filamu yako, watainunua kwa gharama ya shilingi milioni tisa hadi kumi na tano, wakati wewe filamu umetumia shilingi milioni hadi nane kuitengeneza.

“Kuna wasanii wanalipwa hadi milioni nne, hivyo ukiwaweka wasanii wenye majina watatu tayari bajeti imejaa,” anasema msanii huyo. Anasema yeye hajapata tabu sana ya kuzungumza na wasanii wenye majina kwa ajili ya kazi zake, kwa kuwa tayari alikuwa na ukaribu na wasanii hao kutokana na mazoea nayo kama ilivyokuwa kwa marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’.

Lakini anasema kwa msanii mchanga ambaye hana uhusiano wa karibu na waigizaji wakubwa na kibaya zaidi, awe anatoka mkoani huwa anapata tabu hata kuingia hasara. Anasema hivi sasa amekamilisha filamu yake mpya ya Who is the Father, filamu ambayo amewashirikisha wasanii wakubwa kama Athuman Amri ‘King Majuto, Chuchu Hans, Stanley Msungu na yeye mwenyewe ambaye ameigiza kama staa wa filamu hiyo.

Anasema gharama kubwa aliyotumia kumnunua msanii katika uigizaji wake ni King Majuto ambaye alitumia Sh milioni nne kwa ajili ya kumlipa. Kumalija anasema tumaini lake kwa sasa lipo kwenye filamu yake mpya hiyo mpya ya Who is the Father ambayo kwake anahisi kama tumaini la kumfanya atambulike zaidi.

“Wasanii wengine kuwalipa gharama kubwa ni kawaida, kutokana na mavazi wanayotumia, na vitu vingine vidogo vidogo vinagharimu zaidi ya shilingi laki nane,” anaelezea. Katika filamu yake hiyo mpya ambayo inatoka mwezi huu, anasema iliandikwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Fred na yeye kuwa kama mmiliki.

Anasema ni filamu ambayo inaelezea juu ya maisha ya familia ambayo alikuwa akiishi na baba yake, Mzee Majuto. Anasema kutokana na matatizo aliyokuwa nayo ambayo yalikuwa ni siri ya baba yake, analazimishwa kuoa. Bila ya kutegemea anajikuta baba yake akilazimisha kaka mtu, kutembea na mke wake na baada ya hapo inatungwa mimba.

Lakini kikubwa anakuja kujiuliza, kama nina matatizo haya, je na hawa watoto zake wengine, baba yao ni nani? Anasema zaidi ya kuwa ni filamu ya matukio ya kuchekesha, kupitia mwigizaji mahiri King Majuto, lakini pia kuna umakini mkubwa uliyoigizwa na wasanii kama Chuchu Hans na Msungu.

Edward Kumalija aliyezaliwa katika kijiji cha Ikoma, Nyakato jijini Mwanza, hajaoa na anajipanga kuwa mwigizaji mkubwa wa tasnia ya filamu. Anasema malengo yake ni kufanya filamu za kimataifa zenye kiwango cha juu na kushika soko la filamu Tanzania.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Mohamed Mussa

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi