loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ekari 18 za miwa zateketea kwa moto

Mshauri wa kiwanda hicho, Dk Hamza Hussein Sabri alithibitisha kuteketea kwa miwa hiyo, ambayo chanzo cha moto huo kinasadikiwa kuwa ni wakulima wa mashamba ya jirani waliokuwa wakisafisha mashamba yao na kutia moto.

Alisema ekari 18 za miwa, ambazo ni sawa na tani 500, zilikuwa zikitarajiwa kuzalisha sukari tani 50 kwa majaribio katika kiwanda hicho kwa mara ya kwanza.

“Ekari za miwa 18 zimeteketea kwa moto ambazo zimerudisha nyuma juhudi zetu na mikakati ya kuanza uzalishaji wa sukari mwezi ujao,” alisema Sabri.

Hata hivyo, alisema uchunguzi wa awali unaonesha kwamba moto huo umewashwa na baadhi ya wakulima wa mashamba ya jirani, waliokuwa wakisafisha mashamba yao, kwa ajili ya kazi za kupanda mazao mapya kwa ajili ya wakati wa mvua za vuli zinazoendelea kunyesha nchini kote.

Awali, Sheha wa Kijiji cha Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja Ali Haji Bakari, aliwataka wakulima na wafugaji kuheshimu mipaka ya kiwanda cha sukari pamoja na mashamba yake ili kuepuka matukio ya uharibifu.

Alisema tukio la kuteketea kwa moto kwa shamba la miwa ni sehemu ya vitendo vinavyorudisha nyuma wawekezaji katika mikakati yao ya kuzalisha sukari katika kiwanda hicho.

“Wakulima mnatakiwa kuwa makini wakati mnaposafisha mashamba yenu na kutia moto ili kuepuka uharibifu zaidi wa mashamba mengine kama ilivyotokea kwa mashamba ya miwa” alisema.

Meneja wa Kiwanda hicho, Mohamed Britchi aliwataka wananchi wa Kijiji cha Mahonda, kuhakikisha kwamba wanakilinda kiwanda hicho na matukio yoyote ya hujuma. Alisema kiwanda cha Sukari, tayari kimeajiri jumla ya wafanyakazi 470, ambao ni wakaazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

“Kiwanda cha Sukari cha Mohanda kipo kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Kaskazini ambao ndiyo wanaofaidika na ajira,”alisema meneja huyo.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja alisema kwamba wanafanya uchunguzi zaidi, kujua chanzo cha moto huo kama ni ajali au ni sehemu ya hujuma.

Uongozi wa Kiwanda cha Sukari umekuwa na mgogoro wa muda mrefu na wakulima wa mashamba jirani na eneo hilo, ambao wanatakiwa kuondoka katika maeneo hayo na kutoa nafasi kwa kiwanda kupanda miwa.

Kiwanda cha Sukari cha Mahonda kipo katika hatua za mwisho za matayarisho kwa ajili ya uzalishaji wa Sukari baada ya kukaa kwa muda wa miaka kumi bila ya kufanya kazi.

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi