loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

ELIMU BAHARI: Farasi, mnyama anayetafakari

Farasi ni mnyama mkubwa kuliko punda na pundamilia. Wana macho makubwa kuliko wanyama wote wa nchi kavu, na wanasifika katika kazi ya usafirishaji wa watu na mizigo. Pia wanatumika kwa kazi za mashambani, kuvuta magari na mashine mbalimbali. Kuna aina tatu za farasi na aina mojawapo ni farasi wenye asili ya Ulaya na Tarpani ambao hivi sasa inadaiwa wametoweka.

Aina ya pili ni farasi wanaofugwa na aina ya tatu ni farasi mwitu ambao ni wachache ikilinganishwa na wale wanaofugwa. Asili ya farasi wote si kufugwa bali walikuwa wanyama mwitu. Tafiti mbalimbali kuhusu ufugaji wa farasi zinaeleza kuwa ufugaji wa farasi ulianza katika bara la Asia miaka 3,000 iliyopita kabla ya Kristo.

Hata hivyo, tafiti za hivi karibuni zinasema ufugaji huo wa farasi ulifanyika sehemu mbalimbali duniani na sio Asia pekee ingawa bara la Asia na Ulaya waliwafuga kwa wingi zaidi wanayama hao. Pia baadhi ya watu hufuga farasi kwa ajili ya maziwa na nyama mithili ya ng’ombe.

Pia wapo wanaofugwa kwa ajili kushiriki katika michezo, kwa mfano mashindano ya mbio au kuruka juu ya vizuizi na wengine hufugwa kwa ajili ya kushiriki katika vita. Farasi wako kwenye kundi la wanyama wanaokula majani. Wana uwezo wa kula nyasi kilo saba hadi 11 za majani kila siku na kunywa maji lita 38 hadi 45 kwa siku.

Farasi wadogo huwa na meno 38 na wanapokomaa huota meno manne ya ziada na kuwafanya kuwa na jumla ya meno 42. farasi ana uwezo wa kuonja chakula chake kama ni kitamu au la. Hivyo akipewa majani matamu hula kwa wingi ila akibeua majani machungu au yanayoweza kumdhuru hukataa kula.

Mfumo wa tumbo la farasi haumuwezeshi kutapika hivyo huwa makini anapokula chakula kwa kuwa hawezi kutapika chakula kinachomdhuru. Pia hana uwezo wa kupumua kwa mdomo. Farasi wana uwezo wa kulala usingizi wakiwa wamesimama na miguu yao huwawezesha kulala pasipo kuanguka. Hata hivyo hulala uzingizi mnono wanapokuwa wamajilaza chini.

Mfumo wao wa kulala huwawezesha kuwekeana zamu ya kulinda kundi hivyo baadhi ya farasi kulala usingizi wa mang’amu ng’amu wakiwa wamesimama huku wengine wakiwa wamejilaza chini na kupata usingizi mzito. Kwa kawaida hulala wastani wa saa tatu hadi nne kwa siku. Farasi wanaona vizuri ingawa hawawezi kutambua vyema rangi nyekundu na nyingine zinazoshabihiana na nyekundu.

Wana uwezo wa kuzungusha masikio yao kwa nyuzi 180o hivyo husikia vizuri bila kugeuza shingo na wanasikia kuliko binadamu. Uwezo wao wa kuhisi ni mkubwa jambo linalowezesha kuwaepusha binadamu na hatari katika vita au katika safari za kawaida. Farasi wana rangi za kahawia, nyeusi na nyeupe.

Pia kuna farasi wenye rangi mchanganyiko na hutofautiana kimo kulingana na mazingira wanayoishi. Farasi wakubwa zaidi wana uzito wa kilogramu 1,000 na hutumiwa kwa kazi nzito za mashambani au msituni kama vile kufuta magogo. Hata hivyo, kazi zilizokuwa zinafanywa na farasi hivi sasa zinafanywa kwa kutumia vifaa vya kisasa.

Farasi wana uwezo wa kutambua au kuhesabu vitu visivyozidi vitatu, wana uwezo wa kufikiri na kutafakari hasa wanapokutana na kitu kisicho cha kawaida huweza kusita kwenda na kusimama kwa muda kama mtu anayetafakari na kama akiridhika anaweza kwenda au kubadili njia hata bila kuongozwa na mtu anayemuendesha.

Inaelezwa kuwa farasi jike wana mapenzi makubwa na sio wasumbufu wakati wanapofuatwa na dume wakati wakiwa kwenye kipindi cha joto. Farasi jike huingia kwenye kipindi cha joto kwa siku 17 hadi 20. Hata hivyo, madume wana maringo kwa kuwa huwa makini wakati wa kuchagua jike.

Wanapenda kuchagua majike yenye nguvu ili waweze kupata watoto wazuri na wenye maumbo wakubwa. Farasi hubeba mimba kwa kipindi cha miezi 11 ila kuna wanaochukua muda mrefu zaidi hadi mwaka mmoja na juma moja. Kwa kawaida wanazaa mtoto mmoja ingawa hutokewa wakazaa mapacha.

Mtoto wa farasi anaweza kusimama na kukimbakimbia muda mfupi baada ya kuzaliwa Watoto wa farasi huzaliwa wakati wa masika na hunyonyeshwa kati ya miezi minne hadi sita... Farasi huanza kufundishwa kazi akiwa na umri wa miaka miwili hadi minne. Farasi hasa dume hukomaa na kuanza kupanda jike akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu ila mifupa yake huendelea kukua na kukomaa hadi anapofika umri wa miaka sita.

Hata hivyo, umri wa kuzaana hutofautiana kati ya farasi mwitu na farasi wa kufugwa ambao uhuru wao wa kujamiiana ni mdogo ikilinganishwa na farasi mwitu. Uwezo wa farasi kujamiiana unatofautiana kwa umri kutokana na aina ya farasi, ubora wa matunzo, na mazingira.

Farasi wanaopewa matunzo mazuri na wenye eneo kubwa la kuishi huanza kujamiiana mapema ikilinganishwa na farasi wasiokuwa na matunzo mazuri au wanaoishi sehemu ndogo. Pia farasi huanza mafunzo ya kazi wakiwa na umri tofauti kulingana na kazi husika. Farasi wa kazi za nyumbani kama vile kubeba mizigo na watu, huanza kufundishwa wakiwa na miaka miwili hadi mitatu.

Farasi kwa ajili ya michezo na mashindano ya kukimbia huanza kufundishwa wakiwa na umri wa miaka minne hadi mitano kwa kuwa mbio zinahitaji farasi mwenye misuli mikubwa na mifupa iliyokomaa. Farasi hukimbia mwendo tofauti kulingana na mazingira na madhumuni ya mwendo.

Kwa kawaida huenda mwendo wa kilomita sita kwa saa moja ila akiwa mwenye mashindano huenda hadi kilomita 48 kwa saa moja. Farasi ni maarufu kwa usafiri hivyo wafugaji wa husema, “bila miguu hakuna farasi.” Farasi wanatabia ya kupenda kupigana na huweza kujibu mashambulizi katika vita.

Tabia hiyo ya farasi ndio iliwawezesha askari kuanza kutumia farasi katika vita hasa katika vita kuu ya pili ya dunia. Farasi kwa shughuli za kijeshi huanza kufundishwa akiwa na umri wa miaka sita. Farasi humudu mafunzo kulingana na uwezo wa mwili wake. Tafiti zinaonesha kwamba anayepatiwa mafunzo akiwa amekomaa vya kutosha humudu kazi ikilinganishwa na farasi waliyopatiwa mafunzo hayo kabla hawajakomaa.

Farasi huishi umri kati ya miaka 25 hadi 30. Hata hivyo, baadhi ya farasi wanaishi maisha marefu zaidi ambapo karne ya 19 farasi maarufu kwa jina la Old Bill aliishi miaka 62. Ripoti ya hivi karibuni inasema farasi anaejulikana kwa jina la Sugar Puff aliingizwa katika kitabu cha kumbukumbu za dunia kwa kuwa farasi aliishi miaka mingi zaidi. Farasi huyo alikufa mwaka 2007 akiwa na umri wa miaka 56.

Farasi wanaishi katika makundi kulingana na kaliba yao. Wanaweza kukusanyika kwenye makundi kulingana na aina ya farasi pia huweza kuishi na wanyama wengine pia binadamu. Makala haya yameandaliwa kutokana na vyanzo mbalimbali vya elimu ya viumbe na mazingira.

TANGU mwishoni mwaka jana 2020, ...

foto
Mwandishi: Kaanaeli Kaale

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi