loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

ELIMU BAHARI: Nguchiro, mnyama mwenye wivu wa mapenzi

Kuna aina nyingi ya nguchiro na wanatofautiana kulingana na mazingira. Wanyama hawa wanapatikana Afrika, Asia na Ulaya ya Kusini na katika visiwa vya Hawaii nchini Marekani.

Kuna takribani jamii 33 za nguchiro wanaoishi sehemu mbalimbali duniani. Hata hivyo, katika nchi ya Madagascar kuna aina nne za nguchiro ambao baadaye walibainika kuwa wana tabia tofauti hivyo wamewekwa katika familia nyingine ya wanyama iitwayo Galidiinae.

Wanyama hawa ni warefu na wembamba na wana mkia mrefu wenye manyoya mengi. Nguchiro wanafanana na wanyama wengine maarufu kwa jina la chororo ingawa wao ni wakubwa zaidi. Wote wana sura ndefu na miili mirefu pia. Wana masikio madogo ya duara, miguu mifupi na mikia mirefu.

Wengi wana manyoya machache sana mwilini ingawa pia kuna jamii chache zenye manyoya mengi. Vidole vya nguchiro vina kucha ndefu na ngumu kwa ajili ya kazi ya kuchimba wakati wa kutafuta wadudu, nyoka na wanyama wadogo hususan panya. Pia mwili wao una mfumo maalumu unaozuia kudhurika na sumu.

Hata hivyo, nguchirio wanatofautiana kimo ila kwa wastani ukubwa wao ni kati ya futi moja na nne kwa urefu. Uzito wa nguchiro unatofautiana sana kulingana na jamii husika. Wapo nguchiro wadogo wenye uzito wa gramu 280 na wengine wana hadi kilo nne. Nguchiro wana rangi ya hudhurungi, kahawia, kijivu au nyeusi.

Wako kwenye kundi la wanyama wanaoishi kwa kula nyama na chakula chao kikuu ni wadudu, kaa, nyungunyungu, mijusi, nyoka, ndege na wanyama jamii ya panya. Pia hula aina nyingi ya mayai na mizoga inayotokana na wanyama mbalimbali. Nguchiro ni miongoni mwa adui mkubwa wa nyoka.

Wana uwezo wa kujikinga dhidi ya sumu ya nyoka wakati wa kupambana nao kabla ya kuwaua na kuwala. Nguchiro wanatofautiana tabia kulingana na mazingira. Baadhi wanaishi katika mfumo wa ujamaa na wengine wanaishi katika hali ya upweke kila mmoja akijitafutia chakula mwenyewe.

Nguchiro miraba na nguchiro wa jangwa wanawinda mchana na wakati mwingine usiku na hawana ushirikiano wala hawakai pamoja kwani kila mmoja kushika njia na kuishi peke yake. Dume na jike hutumia muda mfupi kukaa pamoja katika kipindi cha kujamiiana. Hata hivyo, kuna jamii zenye mfumo wa kijamaa hivyo kuishi katika kundi kubwa na kushirikiana kutafuta na kugawana chakula, kulea watoto pia kucheza pamoja.

Nguchiro wanapokuwa pamoja hupenda kucheza na kusimama kwa miguu miwili. Wengi wa jamii za nguchiro wana vifuko kwenye sehemu yao ya makalio vyenye kemikali inayotoa harufu ambayo huitumia kuweka mipaka na himaya ya maeneo yao. Pia, harufu hii hutumika kuashiria kuwa mnyama fulani yupo tayari kwa ajili ya kujamiiana.

Nguchiro wa Misri ndiye anayetambulika kama nguchiro anayependa kutembea peke yake. Hata hivyo, kuna wakati nguchiro hawa nao hutembea katika makundi. Tofauti na wanyama wanaofanana naye kama vile viverrids, nguchiro ni mnyama ambaye hufanya shughuli zake nyakati za mchana wakati wale wengine hujishughulisha zaidi usiku.

Nguchiro jamii ya Meerkat au kwa jina jingine Suricate (Surikata), ambao wana umbo dogo, wanaishi katika makundi ya hadi wanyama kati ya 20 na 30. Katika kila kundi kunakuwa na dume mkubwa mmoja na jike wake. Huwa wanaambatana na watoto wao na vijukuu na vitukuu.

Hawa hupatikana pia katika maeneo ya wazi huko kusini mwa Afrika katika nchi kama Angola, Namibia, Botswana na Afrika Kusini. Jamii nyingine ya nguchiro ijulikanayo kama meerkat; ni wadogo kwa umbo na chakula chao kikuu ni wadudu na wanyama wadogo wadogo na nyoka.

Udogo wa umbo na uzito mdogo ni mambo yanayowafanya wawe nguchiro hawa wawe hatarini sana kushambuliwa na wanyama wakubwa walao nyama na hata ndege wakubwa kama tai. Hata hivyo, nao huwakamata ndege wadogo wadogo na kuwala. Kama njia ya kujilinda katika kundi, nguchiro mmoja hufanywa mlinzi wakati wengine wakitafuta chakula.

Huyu hukaa sehemu iliyoinuka na kusimama kwa miguu miwili ya nyuma ili kumwezesha kuona mbali na pande zote. Anapoiona hatari, hutoa sauti kali ili kuwashitua wenzake kuwa kuna hatari inawanyemelea. Pamoja na sauti hiyo pia hutoa ishara hatari inatokea upande gani, kama ni angani au ardhini ili kuwawezesha wenzake kuchukua hatua zinazofaa kujilinda.

Nguchiro wa kijivu wa huko India wanafahamika kwa uwezo wao mkubwa wa kuwashambulia na kuwaua nyoka hata wale wenye sumu kali kama swila. Inaelezwa kuwa ngozi yao ngumu na uwezo wa kuhimili sumu ndio unaomuwezesha nguchiro kupambana na nyoka ambao ni tishio hata kwa binadamu.

Wataalamu wa viumbe wanasema kuwa kemikali iliyomo mwilini mwa nguchiro ndio inayowawezesha kujizuia na sumu ya nyoka kuingia kwenye damu na misuli. Ingawa nguchiro ana uwezo wa kuwinda nyoka, lakini mara nyingi hujiepusha sana kumwinda swila. Mbali na kuepuka kupambana na swila (cobra), wakati mwingine huacha kula nyama ya nyoka huyo kwa kuwa haiwavutii ikilinganishwa na nyama ya nyoka na viumbe wengine jamii ya panya.

Ingawa kuna nguchiro wanaopenda kukaa peke yao, kila mmoja akiweka mipaka katika himaya yake kwa lengo la kudhibiti mwingiliano wakati wa kujamiiana, nguchiro dume huweka mipaka yake kwa kutumia kemikali fulani mithili ya mkojo. Wakati wa kujamiiana dume na jike hukutana sehemu muafaka ndani ya mipaka ya dume husika.

Inaelezwa kuwa nguchiro dume ni miongoni mwa wanyama wenye wivu mkubwa wa kimapenzi. Kwa kawaida dume humiliki majike matatu na hutumia muda mwingi kulinda majike hayo ili yasipandwe na madume mengine. Msimu wa kujamiiana unapofika majike huwa katika hali ya joto kwa siku 10.

Dume hutumia siku tatu kulinda jike ili lisipandwe na dume jingine. Pamoja na jitihada za nguchiro dume kulinda mipaka yao, inaelezwa kuwa majike yana tabia ya kupenda kupandwa na madume tofauti na hivyo huchepuka na kufuata madume katika makundi mengine.

Majike hupata mwanya wa kuchepuka wakati dume anapokuwa karibu na jike mojawapo kwa kuwa dume hapanda majike hao kwa zamu. Baada ya kupandwa jike hubeba mimba kwa siku 60 hadi 70. Kwa kuwa huzaa kwa msimu, majike yote huweza kuzaa kwa siku moja ama kwa kupishana kati ya siku moja hadi mbili.

Nguchiro huzaa watoto wawili hadi sita ila kwa wastani kila jike huzaa watoto wanne. Watoto hao huzaliwa katika msitu mnene ama kwenye vichaka vyenye mimea mingi. Katika siku za mwanzo watoto wa nguchiro hutunzwa na yaya wawili hadi watatu wakati kundi nzima linapokuwa nje ya eneo kwa ajili ya kutafuta chakula.

Baada ya wiki nne watoto wa nguchiro huweza kutoka nje kwa ajili ya kutafuta chakula na husindikizwa na nguchiro wakubwa ili kuwasaidia na kuwalinda dhidi ya maadui. Nguchiro akifikisha umri wa miezi mitatu hadi minne huweza kujitegemea na kwenda kutafuta chakula bila usaidizi.

Nguchiro wanaoishi katika mfumo wa ujamaa hukaa katika makundi ya mchanganyiko wa madume na majike wapatao saba hadi 40. Hata hivyo, wastani wa kila kundi ni nguchiro 20. Wanalala pamoja nyakati za usiku na wanapenda kulala katika vichaka vinene au katika vichuguu vya zamani.

Hubadilisha makao yao kila baada ya siku tatu ili kujiepusha na maadui hasa mbwa mwitu. Wanapokuwa wamelala wengine huelekeza vichwa kusini na wengine kaskazini ili kujilinda dhidi ya maadui hasa mbwa mwitu. Nguchiro hawana mfumo wa utawala. Wakubwa na wadogo wana nafasi sawa na madume yanagombea chakula ambapo wa kwanza kufikia chakula ndio mwenye haki ya kula.

Nguchiro jike ni wataratibu na hawana tabia ya kugombea chakula. Hata hivyo, wanaheshimiana na kuonesha tofauti kidogo unapofika msimu wa kujamiiana ambapo jike huwa kwa kwanza kwenda kwa dume na hutafuta dume lenye umbo kubwa kuliko madume mengine.

Majike yenye umri wa wastani hawana fursa ya kufuata dume kabla ya wale wenye umri mkubwa hayajapandwa. Baada ya majike makubwa kupandwa wale wengine huweza kujitokeza na kufuata dume ambaye naye huchagua aanze yupi. Nguchiro pia anaweza kufugwa na kutumika kama mnyama wa kupambana na panya ndani ya nyumba kama vile anavyotumika paka.

Hata hivyo, pamoja na kuzuia panya, nguchiro anayefugwa anaweza kuwa mharibifu. Wakati nguchiro walipopelekwa huko Marekani kwa ajili ya kuua nyoka na panya, waliharibu pia mimea hasa ile midogo midogo ambayo nayo huitafuna kama sehemu ya mlo wao. Nguchiro pia walipelekwa katika Kisiwa cha Hawaii mnamo mwaka 1883 na tangu wakati huo wameonekana kuwa na madhara kwa wanyama wenyeji wa eneo hilo.

Kutokana na sababu hiyo, hivi sasa ni kinyume cha sheria kupeleka aina yoyote ya nguchiro huko Marekani na Australia. Nguchiro hupenda sana kuishi karibu na makazi ya watu. Hivyo mara nyingi huonekana wakikatiza barabara na nyakati za usiku wengi hugongwa na magari.

Baadhi ya watu wa Pakistan wanaopenda kucheza na na nyoka huwafuga nguchiro na kuwafundisha kupigana na nyoka na huwatumia kama sehemu ya michezo yao.

Miaka ya nyuma Wajapani walifuga nguchiro ili waweze kupambana na nyoka maarufu kwa jina la Habu lakini chama cha kutetea haki za wanyama walipinga kitendo hicho, jambo ambalo lilisababisha mpango huo kusitishwa. Makala haya yameandikwa na Kaanaeli Kaale kwa msaada wa mtandao wa kompyuta na vyanzo mbalimbali vya habari.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi