loader
Dstv Habarileo  Mobile
FILAMU : FEDHEHA-Filamu yenye mafundisho yasiyokanika

FILAMU : FEDHEHA-Filamu yenye mafundisho yasiyokanika

Ni filamu iliyochezwa na Rachel Haule (Recho) na kuzalishwa na mume wake Saguda George. Washiriki wengine wanaonogesha filamu hii ni Haji Salum (Mboto), Haji Adam (Baba Haji) na Fatma Makongoro (Bi Mwenda). Ni filamu yenye vituko inayotia hasira na huruma papo hapo hasa ukizingatia washiriki wake ambao wana uwezo wa kukutia huzuni na pia kukutia hasira na kicheko kwa mbali.

Fatma Makongoro al maarufu kama Bibi Mwenda ni mwanamke ambaye anamudu sana kucheza maeneo yanayoudhi ambayo yanasababisha mtafaruku mkubwa katika akili. Bibi huyu ambaye alikuwa na matatizo makubwa na mwanawe mwishoni mwa siku akiwa hoi kitandani mwake alikiri kumfanyia mambo kadha wa kadha mkamwana wake na hapo ndipo fedheha inapokuja.

Wakati anaomba msamaha na kukiri kumfanyia uchawi na hata kumpiga mkamwana wake kwa kushirikiana na mwanawe, mtazamaji fikira zinakuja pale ambapo Recho alikuwa akilia na mimba yake baada ya kuchakazwa kwa kipigo cha mama mkwe na mwanawe.

Nilipomuuliza Baba Haji kuhusu filamu hiyo alisema ni filamu yenye mafundisho sana, lakini akakiri kutokumbuka simulizi lake kwani amecheza takaribani mwaka mmoja uliopita: “Ni kipindi kirefu kaka Beda hebu ongea na projuza wake Saguda akupe storyline yake” alisema Baba Haji ambaye alicheza kama rafiki wa Mboto na kama mshenga. Naam ni picha ambayo imetengenezwa takribani mwaka mmoja sasa na ipo mitaani ikinadiwa na ipigiwa kite wakati mhusika mkuu Rachel ametangulia kwenye pumziko la milele.

Bi Mwenda kiukweli hakustahili kuwa vile kwani Recho alikuwa ni mtoto wake wa kufikia lakini kwa jinsi alivyokuwa na inda hakuwa na hata ile heri ya shari kwa mtoto wake huyo, yaani hata kujichanganya hakuweza na badala yake akamvuruga kwelikweli mtoto wake huyo wa kufikia. Ndani ya filamu hii Mboto ndiye mchumba wa Recho na Baba Haji ni rafiki mkubwa.

Kwenye filamu hii Baba Haji anazungumzia alichofanywa wakati anataka kuoa, alipobadilishiwa mke aliyemtaka. Ni huyu ambaye anakuwa na maelezo marefu ya hila za watu hali ambayo inamfanya Mboto kuwa na tabia za kiuangalifu zaidi. Kazi hii ya kampuni ya Rasa ina utamu wa aina yake hasa ukiangalia maisha ya Recho na jinsi malipo ya dhambi yanapofanyika hapa hapa duniani na wala si kwingineko.

Recho akiwa anaishi na mama wa kufikia Bi mwenda anakumbwa na madhila yote ambayo haya stahili kukutwa na mwanadamu katika hali ya kawaida. Vituko na madhila hayo hayaishii katika maisha lakini inapoletwa posa mama huyo anataka kuhakikisha kwamba mtoto huyo haolewi.Anafanya kila hilo ili mwanawe ndiye aolewe.

Akiona dalili ya kufeli anabadilisha maamuzi na anakwenda hadi kwa mganga wa kienyeji kuhakikisha kwamba Recho hazai. Lakini Mungu si wa kumfanyia masikhara kwa watu wake ambao hawana wa kuwapigania, anampigania Recho na Bi Mwenda anapata kiharusi kibaya. Ni ugonjwa huu ambao unampeleka vibaya na anayemsaidia ni Recho na mumewe.

Kama unaweza kuwa na nafasi ni vyema kuangalia jinsi watu wanavyopelekeshana katika maisha kwa sababu za husuda tu. Na ni sababu hizi hizi zinazofanya filamu hii kuwa wazi kwa watu, maana yake kuwa na maana katika jamii ambayo imejaa kuvurugana.

Ama hakika malipo ya uzandiki yapo katika maisha yetu ya kila siku na katika hili watu wanastahili kujifunza kuwa waangalifu kwa kuwa atakayekuzika humjui na nafuu yako si balaa kwa wengine. Kifupi washiriki wamefanikisha kuleta ujumbe mwingine yanajadilika katika ufundi, lakini simulizi ni zuri na waigizaji ni wale wanaojua nini wanachokifanya na kama unapenda Mboto walahi una sababu ya kusema kuhusu sinema hii.

“TUNALIMA, tunavuna sana kuliko kawaida, unaweza ukajikuta unauza ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi