loader
Dstv Habarileo  Mobile
FILAMU ZA KISWAHILI: Lulu apania kwenda kimataifa, abisha hodi dirisha dogo ZIFF

FILAMU ZA KISWAHILI: Lulu apania kwenda kimataifa, abisha hodi dirisha dogo ZIFF

Elizabeth al maarufu kama Lulu ni miongoni mwa mastaa wachache nchini ambao wamediriki kupeleka kazi yake ili kutoa wigo zaidi wa kutambulika kimataifa.

Kwa mujibu wa Meneja wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar, Daniel Nyalusi, Lulu ni miongoni mwa mastaa wachache na kampuni za filamu zilizodiriki kupeleka filamu zao katika tamasha dogo la filamu la ZIFF kwa lengo la kumpata mshindi ambaye kazi yake itapelekwa katika tamasha la filamu la Ujerumani.

Hii ni mara ya tatu kwa watu wa ZIFF kuandaa tamasha dogo likiwa ni sehemu ya dirisha dogo la kuelekea tamasha kubwa Julai, lakini likiwa na lengo la kuhamasisha utengenezaji bora wa filamu ili filamu za Kiswahili ziweze kwenda kimataifa bila hofu. Kwa mujibu wa Nyalusi, watu wengine ambao wamepeleka filamu zao ni pamoja na Adam Haji na Ray, huku makampuni yakiwa ni Steps na Pilipili Entertainment.

Alisema katika mazungumzo yaliyofanyika katikati ya wiki kutokana na haja ya kuzitathmini kwa makini, kwa sasa amefunga dirisha la kupokea filamu japokuwa hakuridhika na watu waliojitokeza, akisema ni wachache ukilinganisha na kazi kubwa aliyoifanya kutoa taarifa kwa wadau mbalimbali ili waweze kushiriki.

Alisema aliitisha maombi kwa njia za mtandao na kutumia mitandao kama blogu na mawasiliano mengine kuwapa taarifa wadau mbalimbali wengine akiwapigia simu na pia kutuma ujumbe wa simu, lakini amepata kazi 16 ambazo anasema zinafaa kuangaliwa.

“Mimi nadhani watu hawajiamini, watu wanadhani kwamba wakishamalizana na Wahindi wakachukua mkwanja wao basi, wanasahau kwamba majukwaa kama haya yanatanua wigo wa kujulikana na biashara,” alisema Nyalusi katika mazungumzo. Watanzania wamekuwa waoga sana kushiriki katika mashindano mbalimbali, hali ambayo inadumaza tasnia na pia inafanya watu kuogopa dunia nyingine wakati ukishiriki unaelewa mapema unatakiwa kufanya nini ili uweze kushinda.

Dirisha dogo safari hii litaenda sambamba na maadhimisho ya Mapinduzi Zanzibar na Januari 12 washindi watapewa tuzo. Kuwepo kwa mwitikio wa chini wakati upo mlango wa kutokea katika jamii ya kimataifa inadhihirisha si tu woga bali watu kutotambua kwamba kazi zao ni kazi zao suala ni kuona ni wapi utaweza kuiuza.

Pamoja na kutumia majaji kupata washindi, mfumo wa ZIFF ndogo safari hii unawashirikisha wananchi ambapo watawapigia kura waigizaji bora kwa kupitia njia ya simu baada ya kuona nominii na wao kuangalia fikira zao. Jumla ya filamu 16 zitaangaliwa na kufanyiwa kazi huku muigizaji bora akichaguliwa na wananchi.

“Kuna mfumo tutautangaza ambapo wananchi watashiriki kumpata muigizaji bora, wao ndio watashiriki kuona nani muigizaji bora wa kike na wa kiume,” alisema Daniel Nyalusi. Kuwepo kwa dirisha dogo la ZIFF kumeelezwa na waandaazi wenyewe kwamba wamekusudia kuleta ushindani katika soko la filamu na wakati huo huo kupata filamu bora za kuinadi Tanzania nchi za nje hasa katika masuala ya utamaduni.

Ingawa sinema zetu nyingi zimekuwa kama makapi au kopi za watu wengine bado (labda ndio maana watu wanaogopa kuzifikisha katika mashindano) bado wadau wengine wanaamini juhudi zinazofanywa na Tamasha la Filamu Zanzibar (ZIFF) hasa kwa kuwa na dirisha dogo kuelekea dirisha kubwa zina mantiki yake kama si faida katika kuendelea ushababi wa sinema hapa nchini.

Ofisa Mtendaji wa Tamasha la Kimataifa la filamu la Zanzibar (ZIFF), Profesa Martin Mhando, ambaye amerudi nchini juzi kuja kumzika mama yake kule Tanga akitokea Australia ambako anafundisha masuala ya filamu.

Akizungumza kwa njia ya barua pepe hivi karibuni, alisema kwamba safari hii wanataka ushindani wa mwaka huu uende pamoja na kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar huku somo la mwaka wa kesho la ZIFF likikomazwa na dirisha dogo wakati wa sherehe za mapinduzi ambazo zimerejesha heshima ya Mzanzibari.

“Japo moto wa mwakani yaani ZIFF 2014 ni Common Destiny yaani tukiwa na haja moja, kuishi kwa amani na kuleta mapinduzi ya kiuchumi, kifikira na maendeleo kwa amani, ZIFF kwa kuandaa dirisha dogo katika kipindi cha sherehe za mapinduzi kumelenga wageni ambao watakuja nchini kuweza kuchukua utamaduni huo na kuupeleka nje kwa furaha kubwa,” alisema.

Naam, Agosti mwaka huu wakati wa tamasha la ZIFF kulikuwa na jukwaa lililokuwa likizungumzia utengenezaji wa sinema bora zinazoweza kushindana kimataifa na huwezi kujua sinema bora bila kuwa na matamasha ya kutosha kufanya hivyo na ndio tamasha hili dogo.

Kwa kuwa na tamasha hili Profesa Mhando alisema wadau watakuwa na kasi ya kutaka kuelezea simulizi za kikanda kwa namna yetu sisi si kwa namna ya watu wa Ulaya. Mwezi uliopita wakati nazungumza na Dean Nyalusi, Meneja wa ZIFF alisema kwamba katika tamasha hilo dogo wanatarajia zaidi ya waigizaji kumi wa Bongo Movies kuwapo.

Tamasha hilo dogo la siku tatu linatarajiwa kufanyika kuanzia Januari 10 hadi 12, pamoja na kuburudisha Wazanzibari na wageni, tamasha hilo dogo la siku 3 ni kichochea cha ukuaji wa sanaa ya sinema nchini. Nyalusi alisema wakati huo waigizaji kama Lulu Michael, JB, Wema Sepetu, Irene Uwoya, Vincent Kigosi (Ray), Mzee Majuto, Cloud, Makombora, Mzee Mvita, Zawadi Joachim na Warda wataalikwa katika sherehe hizo.

Kuwapo kwa aina hiyo ya waigizaji kunaleta hisia mbalimbali katika uzalishaji wa sinema, lakini zaidi naweza kuthubutu kusema kwamba inatokana na pia ushindani wao wanaouleta katika tasnia ya filamu zao ambazo nyingi husambazwa na Steps. Ni watu hawa hawa ambao Steps Entertainment iliwapatia tuzo katika kile ambacho tunaweza kutafsiri kama kutambua mchango wao katika ujenzi wa kampuni ya Steps.

Ndani ya Mini ZIFF kutakuwa na Muigizaji Bora wa Kiume na Kike, Muongozaji Bora, Filamu Bora ya Mwaka, Muigizaji anayechipukia, Filamu bora katika Sauti, Filamu bora katika Hadithi, Balozi bora wa Filamu za Kitanzania, Kampuni au mtu aliyetoa mchango mkubwa katika Tasnia hii kwa mwaka huu na Tuzo ya Heshima.

Mini ZIFF 2013 ambayo inaletwa na ZUKU, Push Mobile, Azam Marine, Filamu Central Clouds TV kupitia kipindi cha Take One na Clouds FM kupitia kipindi cha Leo Tena, kimsingi imelenga kuamsha hisia za watanzania na pia waigizaji ili kupandisha chati katika jumuiya ya kimataifa. Mwaka jana tamasha hili lilifanyika katika ukumbi wa nyumbani kwa Tamasha la Majahazi pale Ngome Kongwe Zanzibar Januari 27 na 28 .

Tamasha hilo lilionesha filamu Tano (Dj Ben, Mr President, Big Daddy, Tifu la Mwaka na Pamoja) ambapo filamu hizo zilioneshwa bure na watu walijaa sana kuja kuangalia filamu hizo.

Tamasha hilo pia lilihudhuriwa na wasanii Jacob Stephen (JB), Steven Kanumba, (sasa marehemu) Issa Mussa (Cloud) na Irene Uwoya ambapo mashabiki walifurahi sana uwepo wa wasanii hao, wasanii hawa pia walipata fursa ya kukutana na wasanii wa filamu Zanzibar na kufanya mkutano wa pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Abdilah Jihad Hassan.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi