loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

FILAMU ZA KISWAHILI- Dangerous Desire: Wakati mwingine unatamani waliokufa wawepo aah!

Kwa mara nyingine sijui ya ngapi nimeangalia filamu ya utoto wa akina Kanumba na Ray, Dangerous Desire. Filamu hii ambayo pia wamo Blandina Chagula `Johari’ na Nuru Nassoro `Nora’ ni moja ya filamu iliyobana kisimulizi, ikatoa nafasi ya matumizi ya akili na kujaribu kugumu katika maisha japo ilipotoka kulishatoka filamu nyingine.

Dangerous Desire huwezi kulinganisha na sinema za sasa ambazo kwanza zina bajeti kubwa, lakini hazina ubunifu hata kidogo. Filamu hii ambayo nadhani ilishirikisha watu ambao katika muda huo walikuwa wanapitia vipindi mbalimbali, walionesha nia ya kuigiza sinema kwa kuicheza na si kuigiza kwa kufanya ulinganifu.

Ni rahisi sana kuzungumza jinsi waigizaji kama akina Ray (Vicent Kigosi) ambaye humu alicheza kama Japhet na mwenzake Kanumba (the Great) ambaye alicheza kama mdogo wa Ray jinsi walivyojitahidi kuonesha undugu wao wakiwa na matatizo tofauti. Kwenye Dangerous desire unanyimwa kueleza vitu fulani na twisti inapotokea inakuwa tamu zaidi.

Filamu ya zamani, lakini hizi za kisasa kama usipojua nini kinatakiwa kuendelea walahi utakuwa mjinga wa kutojua kwamba nyingi ya sinema zinazozalishwa sasa zinaweza kuwa za dakika tatu zaidi, bang!.. mwisho, halafu unasema ehee imekuwaje? Walikuwa wanaingia katika ulimwengu, walihitaji kishindo lakini walipojua wakaanza kulipua.

Zipo sinema za nyakati hizo ambazo akili ilitumika zaidi kuliko kupeleka hadithi hafifu kwa wenye kutaka kula, labda kwa kuwa walikuwa wanapambana na sinema za Kinaijeria wakawa wanajaribu kunawa na kula papo hapo. Kuna filamu za mwanzo zinazotoa maarifa zaidi ya kuigiza kuliko zinazofyatuliwa siku hizi ambapo unaanza kuona simulizi zimefilisika.

Pamoja na Dangerous Desire kujaribu kumuona Mungu na maagizo, watengenezaji walichukua maagizo fulani tu kwani maagizo mengine ukiyaweka yanakuwa yanaharibu sinema. Ndio kusema filamu hizi za zamani zilimkumbuka Mungu kwa maneno na muziki kisha zikadistoti ukweli kwa manufaa ya filamu, sio sasa.

Humu ndani kulikuwa na watu wa aina mbili ndugu wawili waliooa katika nyumba moja. Mmoja yeye mwenyewe hawezi kutengeneza watoto, mkewe anaweza na mwingine mke hawezi na mwenyewe anaweza. Simulizi hili lilipanda taratibu kutoka katika mapenzi, msuguano wa mapenzi kwa sababu ya watoto, maarifa duni ya kutambua kwamba watoto ni zawadi na kufanya iwe siri ambayo ikawa balaa la mauaji.

Naam watunzi wapo wachezaji wapo mbona siku hizi mauzauza? Au ndio usupa staa kukolea. Pengine niwalaumu watengeneza sinema wazalishaji ambao wamekuwa wakiangalia majina makubwa zaidi badala ya chipukizi ambao wakipewa mwelekeo wataweza kufanya vitu vinavyotakiwa.

Ahh nani wa kumlaumu, si ajabu watu wanaanza kufyatua sinema za zamani ili watu wajikumbushe manake siku hizi uongo kama kazi na mwisho unajulikana. Angalau kilikuwepo kipindi hapa huwezi kujua mwisho wa sinema sasa tunajua hata kipande cha pili.

Nawatakia Jumamosi njema Ninapatikana kwenye SMS 0713 176 669 au msimbebeda@gmail.com

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi