loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Flaviana na kiu ya kusaidia elimu

Flaviana ni mwanadada mrefu, mwembamba, mcheshi na mzuri kwa ujumla wake anaonekana kuwa ni mwenye malengo katika fani yake ya uanamitindo hasa anapounganisha mitindo na kusaidia elimu. Anaamini kuwa uanamitindo sio lazima tu kuonekana jukwaani au katika vyombo vya habari na katika matangazo ya biashara peke yake.

Akizungumza na gazeti hili, Flaviana anasema kuwa kwake uanamitindo ni kuchukua mwonekano mzuri anapokuwa akionekana kwenye majukwaa ya mitindo na kisha kuweka katika hali halisi.

Akifafanua hoja hiyo, anasema akiwa mwanamitindo anayewakilisha vema nchi nje ya mipaka, anaona inatakiwa kujichukulia kama kioo katika jamii na kuanza jitihada za kuhamasisha mabadiliko kwenye jami.

Akiwa anaamini kuwa elimu ni chanzo cha mabadiliko katika jamii anaichukulia umuhimu mkubwa elimu hiyo kwa kuanza kusaidia wanafunzi wenye uhitaji maalumu.

Anaongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa sekta ya elimu kwa wanafunzi ameamua kuanzisha mradi wa utoaji wa vifaa vya elimu kwa wanafunzi hasa wale waliopo katika mazingira magumu. Anasema mazingira hayo magumu kwa wanafunzi yanatofautiana kwa kuwa wapo ambao wanakosa faraja ya moyo huku wengine wakiwa wanakosa hata vifaa vya kujisomea wakiwa darasani. Anaongeza kuwa chini ya mradi huo wanafunzi wanapatiwa madaftari, kalamu, mkebe, mabegi na misaada mingineo muhimu ya kimasomo. “Mimi nimechagua elimu kama ndio njia mojawapo ya kuleta chachu ya mabadiliko katika jamii, na kwa kutambua hilo ninawasaidia wanafunzi walio katika elimu ya msingi na hadi sasa ni mengi nimeshayaanza kuyafanya,” alisema Flaviana.

Katika kuonesha dhamira yake ya dhati katika kusaidia watoto wenye uhitaji huo maalumu wa misaada ya shule, mwanamitindo Flaviana anasema kuwa tayari kwa msimu huu wa Januari ambapo wanafunzi wanarejea darasani, amewasaidia wanafunzi 1,000 vifaa hivyo vya shule.

Anasema kuwa misaada hiyo imetolewa kwenye Shule ya Msingi Chanzige iliyopo Kisarawe ambapo wamesaidiwa wanafunzi 280, na pia wanafunzi 420 wa Shule ya Msingi Kimanzichana iliyopo Mkuranga.

Anaongeza kuwa wanafunzi wengine ni wa Shule ya Msingi Msinune iliyopo Bagamoyo ambapo wanafunzi 300 wamesaidiwa.

“Sasa unaweza kuona ni kwa jinsi gani ambavyo kuna wanafunzi wamesaidiwa kupitia mradi huu ambapo wanapewa vifaa hivyo kwa bure kabisa kila mmoja na tunazidi kujipanga kuhakikisha kuwa mwezi Julai tunasaidia wengine wengi zaidi,” anasema Flaviana.

Pia mwanadada huyu anasomesha wasichana 15 wanaopata elimu ya sekondari katika shule mbalimbali za Serikali nchini. Katika kufanikisha azma hiyo, Flaviana amekuwa akisaidiwa na watu mbalimbali; mfano ni Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) pamoja na mdau wa mitindo kutoka Marekani, Russell Simons.

Flaviana anaonekana kuwa na moyo wa kushirikiana na wadau wengine katika kufanya kazi hiyo ya kusaidia watoto wenye uhitaji maalumu.

Akishirikiana na Simons, amepewa madaftari ya mazoezi na kalamu za wino kwa wanafunzi 500 walio chini ya mradi wa Tanzania Mitindo House, The Olevolos Project ya Arusha na Shule ya Msingi Mwasele, Shinyanga.

Kwa msaada huo wa Russell Simons, katika kila mwanafunzi kwenye wanafunzi hao 500, kila mmoja atapatiwa madaftari 10 na kalamu ya wino moja. Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa PSPF, Hawa Kikeke anasema kuwa mfuko huo unatambua jitihada zinazofanywa na wasanii katika kuleta mabadiliko kwenye jamii.

Anasema kuwa kazi ya uanamitindo aifanyao Flaviana ni moja kati ya walengwa wa mfuko huo ambao uanatambua pia wafanyakazi wasiokuwa kwenye mfumo rasmi wa ajira.

Anaongeza kuwa kwa kutambua jitihada zake za kuleta mabadiliko katika jamii, PSPF imeamua kumuunga mkono katika kufanikisha msaada wake wa wanafunzi wa awamu ya kwanza ya Januari wa kutoa misaada kwa wanafunzi 1,000.

“PSPF inatambua nafasi za wafanyakazi kama hawa katika suala zima la kusukuma mabadiliko kwenye jamii na ndio maana na sisi tumeona kuwa ni wakati pia wa kuungana naye,” anasema Kikeke.

“Wasanii, wanamitindo na hata wajasiriamali wadogo hawa wanahitajika katika Mfuko huu wa PSPF sasa ni kwa nini na sisi tusimuunge mkono mwanadada kama huyu ambaye ni mwanamitindo na anasaidia jamii,” anaongeza Kikeke.

Flaviana anawataka watu mbalimbali kujitokeza na kumuunga mkono katika harakati hizo ambazo amesema kuwa ni kwa faida ya Watanzania kwa ujumla.

MWANAHARAKATI mmoja anayejiita Mimi ...

foto
Mwandishi: Evance Ng'ingo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi