loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Furaha, changamoto kivumbi tenisi A. Mashariki

Uandaaji wa mashindano hayo ulikuwa ni utaratibu wa kawaida wa kila nchi mwanachama wa Shirikisho la Tenisi Duniani (ITF) na Afrika (CAT) ambapo kila nchi inatakiwa kuandaa mara mbili na huu ulikuwa ni mwaka wa pili kwa Tanzania.

Ushindani uliokuwepo katika mashindano hayo ulikuwa ni mkubwa tofauti na matarajio na washiriki wengi ukilinganisha na mwaka jana ambapo nchi chache zilishiriki kwani kila timu ilijiandaa kikamilifu ili kupanda kiwango cha ubora wa tenisi.

Kwa upande wa Tanzania, kikosi ambacho kilikuwa kikisimamiwa na uongozi wa TTA ukiongozwa na Mwenyekiti Methusela Mbajo, Makamu wake Fina Mango na Kocha Mkuu, Kyango Kipingu, kilifanya vizuri kwenye mashindano hayo kwa asilimia 95. Kocha Kipingu anasema aliandaa timu yake kwa muda mrefu na alikuwa na malengo ya kufanya vizuri ili kubaki katika nafasi nzuri.

Anasema lengo lake limetimia kwani kutokana na juhudi za wachezaji wake wamewezesha Tanzania kushika nafasi ya pili kati ya nchi nane zilizoshiriki huku Burundi ikiwa katika nafasi ya kwanza na Comoro ikishika mkia.

“Nashukuru Mungu kwamba juhudi zimetuwezesha kufanya vizuri, mazoezi yangu yameonekana kwa baadhi ya wachezaji, kwa kweli tumefarijika sana,” anasema Kipingu.

Wachezaji wa Tanzania waliofanya vizuri kwenye mashindano hayo ni Omary Sulle, Tumaini Meshuko, Georgina Kaindoh, Jakline Kayuga na Mallya Nicodemo. Kipingu anasema hao ndio waliofuzu kushiriki kwenye mashindano ya tenisi ya Afrika yatakayofanyika nchini Kenya, Machi mwaka huu.

Akizungumzia ushindi wake, Sulle anasema ushindani ulikuwa ni mgumu, lakini alikuwa akifanya mazoezi mara kwa mara ili kufikia lengo alilojiwekea la kushinda.

“Nashukuru Mungu kwamba lengo langu limetimia kama ambavyo nilikuwa naomba, nafasi ya kushiriki mashindano ya Afrika nimeifurahia, kwa sasa itabidi nijipange kwa sababu najua kuna kibarua kizito mbele,” anaeleza mchezaji huyo.

Mchezaji huyo aliyezaliwa mkoani Arusha, alianza kucheza tenisi toka akiwa mdogo na amekuwa akishiriki kwenye mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Mwaka 2010, akiwa katika mashindano ya Afrika Mashariki nchini Kenya, alionesha juhudi na kufanya vizuri na hivyo kupata udhamini wa masomo kwenda kupata mafunzo ya mchezo huo katika kituo cha kukuza vipaji cha Burundi kinachofahamika kama East Africa Training Centre.

Kwa sasa anaishi nchini humo huku akidhaminiwa masomo yake ya sekondari katika Shule ya Kimataifa ya Kings. Anasema moja ya vitu vilivyomfanya kuchukuliwa ni nidhamu, juhudi na kujituma uwanjani. Hilo kwake bado analiendeleza.

Mchezaji mwingine wa Tanzania aliyepata nafasi hiyo ni Mallya Nicodemo ambaye naye anaishi Burundi akipewa mafunzo ya tenisi na kuendelezwa kimasomo.

Mafunzo waliyopata katika kituo hicho yamezaa matunda katika timu ya Tanzania kwa vile walionesha juhudi kubwa na kuwa tegemeo kwa timu hivyo kupata nafasi ya kufuzu. Kocha wao, Msimamizi wa kituo hicho, Francis Rogoi anasema ili mchezaji apate nafasi hiyo ni lazima aoneshe kwamba anaweza, nidhamu na ndipo achukuliwe.

Anasema ikiwa wachezaji hao wataendelea kuonesha juhudi siku zijazo hadi wanamaliza masomo huenda wakatafutiwa vyuo vya mchezo huo nchini Marekani. Mchezaji mwingine aliyefanya vizuri ni Tumaini Meshuko aliyecheza kwa vijana chini ya umri wa miaka 16.

Meshuko anatoka Arusha na ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Lemara. Anasema alijiandaa kushinda na ndoto imeweza kutimia. Ushindi huo sio wa kwanza kwake, anasema mwaka jana pia alifanya vizuri na ndoto yake kubwa ni kuja kuwa mchezaji wa kulipwa wa kimataifa.

Anasema kufuzu kwake katika mashindano ya Afrika kunampa faraja kubwa na anajipanga kwa kufanya mazoezi ili kurudi tena na ubingwa. Kwa upande wa wachezaji wa kike, Georgina na Jakline ndio waliofanya vizuri kati ya wasichana wachache waliokuwemo.

Kipingu anasema wachezaji waliopo ni wachache hivyo baada ya kumaliza mashindano ya Afrika, anajipanga kuhakikisha anaongeza idadi ya wachezaji wa kike ili wakati ujao wawakilishe Tanzania vizuri zaidi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti Fina Mango anasema amefarijika kwa kiasi kikubwa kuwa walimaza mashindano salama lakini pia wachezaji wameonyesha uwezo mkubwa.

Pia, anaeleza mpango wa TTA wakati ujao katika kutengeneza timu kuwa kutakuwa na mashindano yatakayofanyika kila baada ya miezi mitatu ili kuandaa wachezaji chipukizi wa baadaye.

“Tutakuwa na mashindano yatakayokuwa yakifanyika kila baada ya miezi mitatu lengo ni kuhakikisha tunatengeneza timu, tukiwa na umri kuanzia miaka 12 hadi 16 wasichana kwa wavulana, tunatawaka wakati ujao tufanye mambo makubwa kuliko haya,” anasema Mango.

Alizungumzia mpango wa kutafuta wachezaji katika mikoa mingine ya Tanzania na kusema kuwa wataanzisha kliniki kwa ajili ya kutoa mafunzo ya mchezo huo mikoani ili kuwapata wachezaji wengi watakaokuwa wakifundishwa mchezo huo katika shule. Mango anasema kwa kuanza wataenda mkoani Morogoro kisha mikoa mingine yenye viwanja.

Pamoja na hayo, kuanzia Machi kutakuwa na program ya kubadilishana wachezaji na nchi za Ulaya. Anasema kwa kuanza, amefanya mazungumzo na Chama cha Tenisi Norway ambapo wataleta baadhi ya wachezaji kuja kujifunza Tanzania na wakati ujao, Watanzania wataenda nchini humo ilimradi waoneshe juhudi kwenye mashindano mbalimbali.

Licha ya TTA kuonesha juhudi katika mashindano ya mwaka huu, changamoto kubwa mbele yao ni fedha, kinahitaji kuungwa mkono katika kutimiza mipango yao hasa ikizingatia kwamba wanahitaji kupeleka wachezaji kwenye mashindano ya Afrika.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais Kanda ya Nne wa Tenisi Afrika (CAT) na Afrika Mashariki, Patrick Gichira, wachezaji waliofuzu ikiwa hawatapelekwa kwenye mashindano hayo kuna adhabu itatolewa.

MWANAHARAKATI mmoja anayejiita Mimi ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi