loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Fursa ya uwekezaji, usindikaji wa nyama Tanzania

Hatua hiyo inampatia pesa za mahitaji ambazo zinasaidia kuisukuma familia kwa miezi kadhaa kabla ya kufikiria kwenda kuuza ng’ombe mwingine. Hata hivyo, kule nchi jirani, mnunuzi huyo wa ng’ombe ana kiwanda cha kuchakata, kusindika na kuzalisha soseji na mazao mengine.

Anampeleka ng’ombe huyo kwenye machinjio ya kisasa, kisha anaongeza thamani ya nyama yake kwa kusindika, kuchakata na kutengeneza soseji na mazao mengine, tofauti na kama ng’ombe huyo angeuzwa kwenye soko la ndani.

Katika mchakato mzima wa kuzalisha soseji, ng’ombe yule ambaye mnunuzi wa nchi jirani amemnunua kwa mfugaji wa Kimasai kwa Sh 320,000 za Tanzania, anamwingizia karibu Sh milioni moja za Tanzania licha ya ukweli kwamba soko kubwa la soseji hizo ni katika maduka na supermarkets za Tanzania! Mbali na mwekezaji yule wa nchi jirani kupata faida maradufu na kulipa kodi katika nchi yake, anatengeneza ajira kadhaa nchini mwake.

Machinjioni, wasafirishaji, waendesha mashine, watengeneza mifuko na wengineo kadhaa wanapata ujira wao katika biashara hiyo lakini kwa upande wa pili wa shilingi, aliyefaidika kidogo na ujira mdogo wa ng’ombe anayemchunga kwa takribani miaka mitano ni mfugaji mmoja wa Kimasai na kijana wake.

Hali kama hii inasemekana ndio hiyo hiyo kila unapokwenda katika nchi zinazopakana na nchi yetu hata kama zingine hazina viwanda vya kuongezea thamani inasemekana idadi kubwa ya ng’ombe wanaolisha nchi hizo ni kutoka Tanzania. Hata hivyo, idadi kubwa ya mifugo hiyo imepitia njia za panya (zisizo rasmi) hivyo hazilipiwi tozo ya aina yoyote.

Ni kutokana na ukweli huu unaomfanya Jeremiah Temu aseme kwamba Tanzania haina sababu ya kuagiza nyama na mazao yake nje ya nchi endapo juhudi zitafanyika katika kuhakikisha kwamba uchakataji na usindikaji wa nyama na mazao yake unafanyika hapa nchini kwa kiwango cha kimataifa.

Temu, Ofisa Mifugo Mkuu wa Bodi ya Nyama Tanzania anatoa wito huo wakati akizungumza na gazeti hili kwenye maonesho ya Wakulima, maarufu kama Nanenane, yaliyomalizika mkoani Lindi hivi karibuni.

Katika kufikia hatua ya Tanzania kutohitaji kuagiza nyama na mazao yake nje ya nchi, Temu anashauri kwamba wadau wa tasnia ya nyama wanatakiwa kujizatiti kwa kuwekeza katika eneo hilo, wakati Bodi ya Nyama Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) ikiendelea kuhamasisha wawekezaji kuwekeza kwenye eneo hilo.

Uhamasishaji unashauriwa ufanyike kwa kushirikisha balozi zetu nje ya nchi ili kupata wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika eneo hilo la kusindika nyama hapa nchini.

“Kiasi kidogo cha usindikaji kinachofanyika nchini hivi sasa ni kukata nyama tu (meat cuts) hivyo tunahitaji kupanua zaidi usindikaji wa nyama na mazao yake na kufungasha kwenye vifugashio kama vile makopo na kutengeneza soseji na mazao mengine ya nyama hapa hapa nchini. “Haiwezekani tukaendelea kuwa na mifugo mingi na kuishia hapo tu, tukaacha uongezaji wa thamani wa nyama ufanyike nchi jirani. Kinachotakiwa ni uwekezaji mkubwa kwenye usindikaji,” anasema Temu.

Ni kwa msingi huo, Temu anawashauri wadau wa tasnia ya nyama na vyama vyao kujizatiti zaidi na kuhakikisha kwamba sasa wanafanya kazi kibiashara, kwa kuangalia pia, mahitaji ya soko maalumu la ndani na la nje ya nchi. Hata hivyo, anasema hayo yote yatawezekana kama wafugaji wataanza kufuga kisasa wakilenga biashara zaidi na si ufahari wa kuwa na mifugo mingi au kufuga kimazoea.

“Kwa mfano, wengi wanapeleka sokoni ng’ombe anapokuwa na shida ya pesa na siyo kwamba sasa anafaa kuvunwa kwa ajili ya kuzalisha nyama bora,” anasema na kufafanua kwamba ng’ombe wengi wanaopelekwa sokoni huwa wameshazeeka, wakiwa na umri mkubwa miaka mitano au zaidi.

Anaendelea kueleza kwamba ng’ombe anayefaa kuzalisha nyama bora anatakiwa awe na umri wa miaka miwili hadi mitatu na nusu. Hivyo, anawaasa wakulima kufuga kisasa ili ng’ombe wanaopelekwa sokoni wawe na madaraja ambayo yatatoa nyama bora. Temu anawashauri wafugaji kuvuna mifugo yao inapofikia ubora unaohitajika na soko kama wakulima wa mazao wanavyofanya, mazao yao yanapofikia wakati wa kuvuna hawasubiri siku ya kutaka kupika/kuuza ndipo waende kuvuna.

“Wakati mwingine mfugaji anamchelewesha ng’ombe kumpeleka sokoni hadi nyama yake inakuwa haifai kuliwa kwa uzee kutokana na kusubiri aongezeke uzito,” anasema. Hata hivyo, anasema mifugo ya aina hii (iliyozeeka) inaweza kutumika kuzalisha mazao mengine ya nyama endapo uchakataji na usindikaji ungekuwa unafanyika hapa nchini.

Kingine anachoshauri Temu ni machinjio za kisasa chache zilizopo zifanye kazi kwa uwezo wake kuliko hali ya sasa ambapo machinjio nyingi zinakabiliwa na changamoto ya vifaa na utaalamu wa uchinjaji. “Tunazo machinjio kadhaa za kisasa yaani “abattoir” ambazo zinafanya kazi chini ya uwezo wake kutokana na kutokuwepo kwa usindikaji.

Machinjio za kisasa zilizopo hapa nchini ni pamoja na SAAFI, Dodoma, Arusha Meat, Orpul - Simanjiro, iliyokuwa Pride Meat -Mvomero na Iringa. Kadhalika, mtaalamu huyo wa nyama na mifugo anaonesha masikitiko yake kwa Jiji la Dar es Salaam kutokuwa na machinjio ya kisasa licha ya kuwa na idadi kubwa ya walaji wa nyama.

Hata hivyo, Temu ana matumaini kwamba machinjio ya kisasa inayojengwa Ruvu mkoani Pwani inayomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) inaweza kuwa mkombozi wa jiji hilo. Anafafanua kwamba machinjio hiyo itakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 800 na mbuzi ama kondoo 400 kwa siku.

Aidha, kwa sasa anasema kama walaji wa nyama wangekuwa wanakubali kula nyama iliyopoozwa ingewezekana Jiji kupata nyama kutoka machinjio za kisasa zilizopo mikoani.

Anatoa wito kwa serikali za mitaa kwa maana ya halmashauri za miji, wilaya na majiji kuhakikisha zinakuwa na machinjio za kisasa, ikiwezekana Halmashauri zilizoko jirani zishirikiane kujenga machinjio ya kisasa moja ili kupata huduma bora na wakati huo huo zikipunguza gharama za uwekezaji na uendeshaji.

Anasema, kwa mujibu wa sheria zinazosimamia ubora na usalama wa nyama na bidhaa zake, machinjio zote zisizokidhi viwango zitafungwa sambamba na kuwawajibisha wote wanaochinja wanyama nyumbani au mahali pengine popote ambapo si machinjio inayotambulika.

Aidha, anasema walaji wote wanayo haki ya kula nyama bora na salama, hivyo ni vema kuzingatia kanuni za uchinjaji ambapo mnyama hupumzishwa kwa siku mbili hadi nne kama amesafirishwa toka mbali. Aidha, wakati wa kumchinja anatakiwa kupotezwa fahamu kwa kutumia mbinu ifaayo kabla ya kuchinjwa.

Kadhalika anasema baada ya kukata shingo mnyama aning’inizwe ili damu nyingi iwezekanavyo itoke kwa ajili ya kuongeza ubora wa nyama na uhifadhi. Kadhalika anasema ni muhimu mifugo ichunwe ngozi ikiwa imeninginia hivyo hivyo kuhakikisha usafi wa nyama na ubora wa ngozi.

Anafafanua kwamba nyama ikishachinjwa, inatakiwa ikae kwenye ubaridi (chiller) kwa siku kuanzia mbili hadi 21 ili misuli ijitengeneze kuwa nyama, na kwa hatua hiyo nyama inaongezeka thamani kwa maana ya ulaini, utamu na kupungua vimelea vya magonjwa. “Nchi nyingine zinazozingatia ubora na usalama wa nyama, lazima nyama iwekwe kwenye baridi kwa siku 21 ndipo iuzwe ,” anasema.

Nyama inatakiwa kuchunwa ikiwa imening’inizwa ili damu itoke kadri ninavyowezekana. Nyama iliyopoozwa kwa siku zaidi ya mbili huwa laini, tamu na yenye ladha. Tanzania haina sababu ya kuagiza soseji kama uwekezaji katika uchakataji na usindikaji wa nyama utafanyika nchini kwa kiwango cha kimataifa.

Kuna aina nyingi za mazao ya nyama zinazoweza kuzalishwa hapa nchini badala ya nyama ya kukata buchani. Tanzania, kwa kuwa na mifugo mingi haina pia sababu ya kuagiza nyama za kopo toka nje ya nchi.

Ofisa Mifugo Mkuu wa Bodi ya Nyama, Jeremiah Temu (kulia anayeangalia kamera) akitoa maelezo kwa watu waliofika katika banda la Bodi hiyo wakati wa sherehe za Nanenane mwaka huu. Pamoja na mambo mengine, alieleza namna Tanzania inavyoweza kuboresha mazao ya nyama kupitia uwekezaji na kuongeza ajira nchini.

“WANAOFANYA shughuli za maendeleo katika vyanzo vinavyotiririsha maji ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi