loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Gesi yakonga nyoyo wakazi wa kisiwa cha Songosongo

Hata wanafunzi wenye safari za kwenda Dar es Salaam, Lindi na Mtwara husafirishwa kwa ndege tena bure na wawekezaji mbalimbali wanaotafuta mafuta katika kisiwa hicho au wanaojenga bomba la gesi litokalo katika kisiwa hicho hadi Dar es Salaam. Mbali na masuala hayo ya maendeleo ya kijamii yanayopatikana katika kisiwa hicho, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kwa mtu mmoja mmoja jambo ambalo wanahitaji kujikomboa.

Unawaona watoto wa shule, wapitao barabarani na hata maeneo ya wakazi utaona wakitembea bila viatu huku wengine wakiwa wamevaa nguo za shule zilizochakaa pamoja na kukosa lishe mahsusi. Tatizo kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo kwa sasa ni usafiri wa kutoka na kuingia katika kisiwa hicho, jambo linalofanya ni wageni wachache wanaofika ambao wana uwezo wa kutumia usafiri wa ndege.

Mkazi wa kisiwa hicho, Halima Msesi anasema changamoto hiyo inawafanya wananchi kuishi kwa hofu kwani iwapo itatokea mgonjwa anayehitaji kupelekwa kwenye hospitali kubwa nje ya kisiwa inakuwa mtihani. “Tunayo zahanati hapa lakini kama unavyojua baadhi ya magonjwa makubwa inatulazimu kupeleka wagonjwa ng’ambo, lakini uvukaji wake kwa kweli ni mgumu ni vema serikali ikaangalia suala hili la kivuko cha uhakika,” anasema.

Kampuni ya maendeleo ya mafuta ya China (CNPC) inayosimamia ujenzi wa bomba la gesi kutoka katika kisiwa hicho hadi jijini Dar es Salaam waliamua kutoa sehemu ya mapato yao kwa wananchi hao. Walitoa boti ya kubebea wagonjwa kwa wananchi viatu pea 240, jezi za mpira 30 pamoja na mipira 10 kwa ajili ya mpira wa miguu kwa shule ya msingi Songosongo, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 105.

Hafla ya kupokea msaada wa vifaa hivyo iliyofanyika katika shule ya msingi Songosongo, uliohudhuriwa na viongozi wa kijiji, kata na wananchi wa kisiwa hicho. Naibu Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya CNPC, Mao Qiping, anasema misaada hiyo ni shukrani kwa wakazi wa kisiwa hicho kwa ukarimu waliouonesha tangu walipoanza kazi ya ujenzi wa bomba hilo mpaka sasa inapotarajia kukamilika.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Abdallah Yahya anasema msaada huo utasaidia kuwa na usafiri wa uhakika kwa wagonjwa badala ya kutumia mashua ambazo ni hatari kwa maisha. Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya Msingi Songosongo, Haji Njechele anasema boti hilo litasaidia kupunguza vifo ambavyo vilikuwa vikitokea kutokana na kukosekana usafiri.

“Pia itasaidia akinamama wajawazito kuwa na uhakika wa usafiri, kwani walilazimika kuondoka katika makazi yao miezi mitatu kabla ya kujifungua,” anasema Njechele. Anashukuru kwa vifaa vya michezo vilivyotolewa kwani vitasaidia kukuza michezo shuleni hapo pamoja na wanafunzi kuwa na viatu, kwani wengi walikuwa wakivaa viatu vya wazi (yeboyebo).

Mtendaji wa kata hiyo ya SongoSongo, Shamte Bungara anasema kata hiyo imenufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli za wawekezaji wa gesi na mafuta, kwani kumekuwa na maendeleo tofauti na awali. Anasema mafanikio hayo ni pamoja na kutumia umeme wa bure, lakini sasa wanakabiliwa na tatizo la wananchi kujiunganishia umeme ovyo bila kufuata taratibu.

Pia anasema katika shule yao ya msingi na sekondari wawekezaji wamewawezesha kutokuwa na tatizo la vitabu wala madawati kwani sasa kila mwanafunzi ana kitabu chake cha masomo yote. Huku kukiwa hakuna mzazi anayelipia chochote kwa wanafunzi wanaosoma sekondari, jambo linalofanywa na kampuni mojawapo ya uwekezaji huku wakijengewa hosteli kwa yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 50.

Anasema hosteli haijaanza kutumika kutokana na kukosa uzio pamoja na maji kutokana na kuwepo kwa vyoo vya kisasa wanasubiri maji yafike ili kuweza kutumika. Anasema licha ya mafanikio katika elimu bado wanakabiliwa na changamoto ya walimu kutokana na ukweli kuwa ukosefu wa kivuko cha uhakika unawafanya kukosa walimu wanaopangiwa kufanya kazi kisiwani hapo.

“Katika sekondari yetu changamoto ya walimu ni kubwa kidogo kwani hatuna walimu wa masomo ya sayansi wengi waliopo ni masomo ya sanaa huku shule ya msingi yenye wanafunzi 40 ina walimu wanane tu ambapo kila mwalimu ana masomo sita ya kufundisha,” anasema.

Akizungumzia suala la huduma za afya, mtendaji huyo anasema hakuna madaktari katika zahanati iliyojengwa na wawekezaji hao, lakini wamekuwa wakiwasaidia kwa kumtoa daktari katika kambi zao mara mbili kwa wiki. Anasema daktari huyo hufika katika zahanati hiyo Ijumaa na Jumatatu huku wakiwa na mikakati ya kutoa dawa na vifaa tiba kwa lengo la kuokoa maisha ya wananchi wa kisiwa hicho.

“Ukweli wawekezaji hawa wanatusaidia sana katika huduma za kijamii na tunaona fahari kuwepo rasilimali katika eneo letu, jambo la msingi ni kuboresha mazingira hasa kuwa na kivuko cha uhakika,” anasema.

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi