loader
Dstv Habarileo  Mobile
Giza totoro katikati ya handaki la Tazara

Giza totoro katikati ya handaki la Tazara

Wakati huo usafiri huo ulikuwa bora, mzuri, wa uhakika na kufurahisha. Sasa hali imebadilika, usafiri huo ni tia maji tia maji, hauna ratiba maalumu. Nimeshuhudia nikiwa kwenye msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, pamoja na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na mbunge wa kuteuliwa ambaye ni Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro.

Safari ya asubuhi hadi usiku wa Desemba 8 na siku iliyofuata ya kuamkia kumbukumbu ya Uhuru wa Tanzania Bara, Desemba 9, mwaka 2013. Usafiri kwa njia ya reli ya Tazara, hauna uhakika. Ratiba ya usafiri huo ilivurugika, tangu tulipofika kwa magari hapo Makambako kutoka Njombe. Usafiri wa treni kutoka Kapiri Mposhi, Zambia utakuwa saa tatu.

Haukupita muda, ikaja habari kwamba utakuwa saa sita usiku, tukasikia saa tisa, ajabu na kweli tukaondoka saa 2.30 asubuhi. Mabadiliko ya ghafla ya ratiba kwa treni hiyo ni kawaida, kama msafiri yanaifanya siku iwe ndefu. Kwetu sisi usiku huo ulikuwa mrefu, kutokana na kulala usingizi wa mang’amung’amu, tukitarajia kusikia kwamba safari itaanza saa yoyote, lakini ikawa jioni, usiku, hadi asubuhi.

Usiku huo ulikuwa mrefu kutokana na baridi ya Makambako. Baridi yake inaambatana na upepo mkali, inapuliza hadi kurusha nguo, inagandisha na kusababisha kamasi kutoka bila simile. Bila sweta, koti au nguo nzito, au na migolole ya Kimasai kama tuliyokuwa nayo sisi bado haikufua dafu, tulitetemeka vile vile.

Reli ya Tazara imebadilika kila mtu analalamika, menejimenti inalalamika na wafanyakazi wanalalamika, vituo, majengo, mabehewa na nyumba za kupumzikia hali si yenyewe. Wakati baridi ikinipuliza, nilikumbuka kuchoka kwa reli kuliifanya menejimenti na wafanyakazi wa Tazara wawasilishe changamoto 36 kwa Katibu Mkuu wa CCM, Kinana alipozungumza nao Mbeya.

Walilalamika mengi, wakapendekeza kama Serikali imedhamiria kuinusuru Taraza hiyo iliyojengwa mwaka 1972, bora mjenzi wa reli hiyo, Mchina, arudi na kuiendesha, kwani ikiachwa vivyo hivyo itachungulia shimo. Lakini pia wakapendekeza ufumbuzi wa kweli lazima marais wawili, Jakaya Kikwete wa Tanzania na Michael Satawa wa Zambia, wakutane na kuufanyia marekebisho mkataba wa kujengwa kwa reli hiyo.

Viongozi wa wakati huo, Julius Nyerere wa Tanzania na Kenneth Kaunda wa Zambia, walikuwa na nia madhubuti ya kusaidia kusafirisha wapigania uhuru kusini mwa Afrika, jambo ambalo leo halipo, nchi hizo zimepata uhuru. Japo lengo la kusaidia nchi za Zambia, Zimbabwe na nyingine ambazo hazina bandari kusafirisha abiria na mizigo limebaki, nchi hizo zinashindwa kutumia reli hiyo kutokana na sababu nyingi.

Lengo la kusaidia kusafirisha abiria na mazao katika maeneo ya mikoa inamopita ya Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, bado limebaki. Suala la kufumua uongozi wa juu wa reli hiyo, ni muhimu kwani hakuna lazima mkurugenzi mkuu kutoka upande mmoja wa reli yaani Zambia, pamoja nzuri ya waasisi, hali imekuwa kinyume.

Kitendo cha kumnyima nguvu za kufanya lolote mkurugenzi msaidizi anayetoka Tanzania, kwani unasema anaweza kuombwa ushauri au asiombwe na mkurugenzi mkuu, jambo ambalo linampa ruhusa ya kuamua bila kuhitaji ushauri. Ushauri wao wa kwamba kila nchi isimamie kipande cha reli yake, badala ya kuendelea kusimamiwa kwa pamoja, kungesaidia katika kutafuta mizigo na abiria kadiri ya mahitaji ya nchi.

Wakati nikiwaza kuhusu malalamiko ya wafanyakazi na menejimenti kuhusu mkataba huo pamoja na hali ya shirika, zilikuwa zimepita saa mbili na nusu ndipo mabehewa yakawa yamepangwa tayari kuondoka. Safari ilianza, faraja ikaja kwamba tungetumia saa 18 kusafiri, lakini kwa bahati nzuri au mbaya tuliingia Dar es Salaam asubuhi kama muda tuliondokea Makambako siku ya pili yake.

Safari ni ndefu kutokana na treni kusimama saa moja kwenye vituo vikubwa vya Mlimba na Mang’ula na vituo vingine vidogo zaidi ya 20 kwa kusimama nusu saa. Tangu Makambako tukapita Mahongole, Kitandalila, Kihowela, Uchindile, Kitete, Mpanga, Kimbwe, Lumuma, Mlimba, ikawa jioni.

Usiku ukaingia Chita, Mgeta, Mbingu, Lwipa, Ifakara, Kaberege, Mang’ula, Msolwa, Pwaga, Lumungo, Kisaki, Matumbwe, Fugu, Kidunda, Gwate, Nyani, Mzenga, Vigama na Mwakanga tukaingia saa mbili asubuhi. Mwendo wa treni wa kacha kacha, honi nyingi ukaongeza saa nyingi kuwa njiani. Ubovu wa reli, uliongeza hofu, tukadhani mabehewa yanataka kuhama mataruma.

Kuruka ruka kwa mabehewa, kuliashiria tusingefika tuendako. Ndani ya treni japo tulikuwa daraja la pili, msongamano wa abiria wa daraja la tatu, hatukuukwepa. Kila kituo watu walipita na kurudi na mizigo, vurugu tupu. Japo kulikuwa na msongamano, usafiri wa treni una raha yake, kula na kunywa pamoja na kupiga picha za kumbukumbu kupitia madirisha makubwa na milango.

Pamoja na furaha hiyo, hofu ilitanda giza totoro ghafla. Si usiku kumbe ndio wakati tulikuwa tukipita kwenye mahandaki. Reli hiyo tangu Makambako hadi Dar es Salaam kuna mahandaki 19. Handaki likija, giza totoro linafunika mabehewa, usiku unakuja ghafla. Watu wanashika vifua na kuomba kwa miungu yao.Nyakati hizo hakuna kuonana wala kusikilizana.

Yapo mahandaki marefu, mengine yanafikia urefu kilometa moja hivi. Saa hizo watu wanakuwa ndani ya mabehewa na ndani ya giza. Hofu kubwa inatanda hasa treni inapokimbia kama vile inaruka ruka, unadhani kwamba imeacha mataruma. Giza totoro linafunika unadhani treni imeparamia mlima.

Kama ndio unasafiri kwa mara ya kwanza, ni wazi unaweza kudhani kwamba unapopita kwenye mahandaki hayo upo shimoni au kaburini. Wakati huo, ndani humo hakuna kutembea, kusimama wala kufanya lolote, ni giza totoro, hatuonani. Mkitoka kwenye handaki, mnatazama kama mpo salama. Utamsikia Seleman Jongo, Said Mwishehe, Sheila Simba, Mary Godfrey, Richard Mwaikenda, John Bukuku wakiulizana.

Wengine akina Bakari Kimwanga, Sylvanus Kigomba, Joseph Mpangala, MwanyiMkuu na Bashir Nkoroma, wanaangaliana usoni kama wapo salama, ndipo mazungumzo yanaanza. Kujenga reli hiyo, kulikuwa na maana kubwa ndio maana kuna wakati kulikuwa na treni inayotoa huduma kati ya Mlimba na Makambako, ikafa kifo cha kawaida.

Treni hiyo ilikuwa msaada mkubwa wa wananchi na wafanyabiashara wa maeneo ya Mang’ula na Mlimba ambao walisafirisha mazao na bidhaa za madukani na dawa kutoka Makambako na Mlimba. Wananchi wa eneo hilo ambalo ni maarufu hawakujali giza la mahandaki walisafirisha mpunga, viazi na matunda, kwao bila treni hakuwa na maisha ya watu.

Watu wa Uchindile hadi Chita, tangu hapo hawakuwa na usafiri mwingine, zaidi ya kutegemea wa treni, kwa kuchukua bidhaa Makambako na dawa Mlimba na kusafirisha wanafunzi na kutafuta huduma nyingine. Kupungua kwa safari za treni, kuzorota kwa huduma za reli na kuyumba kwa utendaji wa menejimenti yake, kumefanya maisha ya wakazi wa maeneo hayo kuwa na walakini.

Mohamed Mhala ni mkazi wa Uchindile anasema treni ya Tazara inawapa wakati mgumu kutokana na kufuta kwa treni iliyokuwa ikitoa huduma kwao na kupunguza kwa safari za treni. Anashauri kwamba, ingekuwa vema uongozi wa reli ungeongeza japo haupendi kurudisha treni ya Mlimba Makambako basi waongeze safari za treni ya kawaida na maalumu kutokana na umuhimu wake katika maeneo hayo.

Kwa sasa treni ya kawaida inapita mara mbili kwa wiki Jumatatu na Ijumaa na maalumu Jumatano tofauti na zamani ambapo ilifanya safari pia Jumanne. Lakini pia hivi sasa kuna mfumo mbovu wa kuwalazimisha abiria wanaoshuka njiani kulipa nauli ya vituo vikubwa. Ukipanda treni hata kama mtu anashuka njiani analazimika kukata tiketi ya kushuka popote lakini nauli ya kushuka vituo vikubwa tu.

Kwa sasa hakuna tiketi ya Dar es Salaam hadi Uchindile, hivyo mtu analazimika kulipia nauli ya Makambako, jambo linalowaumiza wananchi wanaoshuka vituo vidogo. Wananchi wa maeneo hayo wanategemea kilimo, bila usafiri wa reli hakuna maisha, wanashindwa kuendesha maisha yao, bila kujua hatima yao.

Maeneo hayo hayana barabara, yanategemea treni tu. Kwa wananchi hao bila treni safari za treni hakuna maisha. Reli ya Tazara kama inataka kusimama kweli ni lazima kufanyia marekebisho kuanzia uongozi wake, menejimenti na utendaji wa wafanyakazi na kuangalia mikataba iliyoifanya ijengwe ndipo itaondoka katikati ya giza la kwenye mahandaki.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi