loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hakuna watoto wanaojileta wenyewe

Nimejikuta nikipata huzuni na maumivu ya moyo baada ya kusoma habari ya mtoto aliyeteswa na mama mlezi kwa kuwekwa kwenye boksi tangu akiwa na miezi tisa mpaka anatimiza miaka minne ndio linagundulika tukio hilo.

Naamini mzazi au mlezi yeyote mwenye uchungu habari hii lazima itakuwa imemgusa kama sio kuumiza moyo baada ya kusoma ama kuona kwenye vyombo vya habari, kwani ni kitendo cha kinyama na cha kusikitisha kwa kiumbe huyu asiyekuwa na hatia yoyote.

Tukio hili la kusikitisha limetokea Morogoro ambapo mama mkubwa wa mtoto huyo aliamua kumfungia kwenye boksi zaidi ya miaka mitatu kama mnyama ili asiambukizwe virusi vinavyosababisha Ukimwi.

Jambo la kushangaza na kuumiza zaidi kuona anayefanya kitendo hiki ni mwanamke ambaye siku zote katika jamii inaelezwa kuwa mwanamke ni mtu mwenye upendo na uchungu mkubwa kwa mtoto au watoto, lakini siku hizi hali imekuwa tofauti.

Yapo matukio mengi ya kikatili ambayo siku hizi baadhi ya wanawake wamekuwa wakihusika moja kwa moja kufanyia watoto wao au watoto wa kuwalea kwa maana ya watoto wa ndugu zao au watoto wa kambo.

Hapo ndipo najiuliza huyu mama mlezi wa mtoto wa Morogoro ana mkataba gani na Mungu, hadi aone kumficha mtoto kwenye boksi ndio kumuepusha na maambukizi ya Ukimwi!

Najiuliza nashindwa kupata jibu kama huyu mwanamke kweli anafikiria sawasawa au ana tatizo la kufikiri. Yaani kama isingekuwa wasamaria, huyu mtoto angeendelea kuteseka na huenda mwisho akapoteza maisha kwa sababu ya mwanamke ambaye haoni thamani ya mtoto huyo kuishi maisha ya ubinadamu kama walivyoishi watoto wengine.

Kama mama huyo aliona ni mzigo kuishi na mtoto huyo, kwa nini hakumrudisha kwa baba yake, hata kama baba yake anadai alikuwa anamuogopa mke wake, lakini ni jukumu lake na ni mtoto wake analivyomleta duniani alikuwa akifikiria nini?

Nabakia kujiuliza na huyu baba jamani, hivi kweli unakwenda kumsalimia mtoto wewe kila siku unaambiwa kalala, kaenda kucheza na wenzake unaridhika tu, kwa nini usilazimishe hata kuingia ndani kumuona kama kalala kweli au kuamuru aitwe umuone.

Napata mashaka hata na huyu baba mtoto kama kweli alikuwa anampenda mtoto wake au alishaona ametua mzigo aendelee na maisha yake.

Sitaki kuzungumza mengi kwa sababu suala hili linaendelea kufanyiwa uchunguzi na vyombo vya dola na naamini ukweli utawekwa bayana.

Hoja yangu lakini ni kuwakumbusha pia wazazi na walezi kuhusu wajibu wa kuwalinda na kuwatetea watoto. Wakiwa katika hali ya udogo watoto ni tegemezi kwa watu wazima, lakini kama watu wazima wenyewe ndio hawa wenyewe roho za namna hii watakimbilia wapi.

Hakuna mtoto au watoto wanaojileta wenyewe duniani, wazazi ndio chanzo cha wao kukanyaga katika dunia hii, kwa hiyo kila mzazi kwa nafasi yake anapaswa kuwajibika na kuhakikisha watoto wanaishi katika mazingira salama na upendo.

Mwito wangu kwa mamlaka husika kuhakikisha zinawachukulia hatua wazazi na walezi wale walioshindwa kuwalinda watoto na kugeuka kuwa ndio wakatili kwa watoto ili iwe fundisho kwa yeyote mwingine atakayetaka kujaribu kufanya matendo ya kikatili kama haya.

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi