loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

HAPPY BALICE: Ajitoa kundi la Mtanashati

Hiyo ni kutokana na kuona migongano ya makundi, jambo ambalo limemfanya kuamua kuwa msanii atakayefanya kazi zake mwenyewe. Kwa mara ya kwanza alikuwa katika kundi hilo, akiwa na wasanii wengine kama Abdulaziz Chande ‘Dogo Janja,’ Musa Kitale ‘Kitale’, Pancras Ndaki ‘PNC’ na Suma Mnazareti.

Katika kipindi hicho, alifanya kazi nyingi, lakini zilizopata umaarufu ni mbili; ya kwanza ikiwa Bora Sioni aliyoimba yeye mwenyewe na Watasubiri ambayo ilikuwa ya kundi. Akizungumza na gazeti hili, Balice alisema yapo mengi yaliyomfanya kuamua kuwa msanii wa kujitegemea bila ya kuwa na kundi lolote.

Anasema kwa mara ya kwanza alijiunga na Kundi la Mtanashati mwaka 2011, baada ya rafiki yake aliyekuwa akiimba naye kumshauri kujiunga nalo baada ya kazi yake ya kwanza. Anasema sanaa alianza kwa kuimba kwaya kanisani, kwa lengo la kujiunga na shindano la kusaka vipaji la Bongo Star Search 2011 (BSS 2011).

“Rafiki yangu aliponiona naimba alinikubali sana, na kuniambia anaweza kunisaidia kwenda studio kwa ajili ya kukutana na mtu atakayemsaidia kurekodi bure,” anasema msanii huyo. Anasema baada ya kupewa imani kwamba anaweza kwenda kurekodi, aliamua kuachana na mawazo ya kwenda kujiunga na shindano hilo.

Ndipo wakaenda kwenye studio ya Burn Record chini ya Shedy Clever, akarekodi wimbo wake wa kwanza ulikuwa ukiitwa Sina Upendo. Anasema wimbo huo alimshirikisha msanii mwenzake, Kervin aliyekutana naye hapo studio. “Nilikuwa natumia mtindo wa Rhumba nikichanganya na Zouk, ambapo kila mtu aliyeisikia akaipenda,” anaeleza Balice.

Baada ya wimbo huo, anasema ndipo akajitokeza mtu mwingine na kumwambia, anaweza kwenda kufanya majaribio kwa Ustadhi Juma na Musoma. Jambo ambalo alikubaliana nalo na kuamua kuchukua wimbo huo na kwenda kumsikilizisha, ili kuweza kupima uwezo wake.

“Wakati naenda na wimbo huo, waliusikiliza na wakaupenda, nikaambiwa nikatengeneze na mwanamuziki wa kundi hili, PNC, nikakubaliana nao,” anafafanua msanii huyo.

Baada ya kujiunga na kundi hilo, anadai kuwa PNC ambaye tayari alikuwa na jina kubwa, alikataa kuimba tena wimbo huo kwa kuhofia kuonekana kuiga wimbo huo. “Ilibidi aige mashairi ambayo aliimba Kervin, akasema haiwezekani kwa kuwa yeye ni msanii mkubwa sana,” alidai Balice.

Ikabidi wakubaliane kutengeneza wimbo mwingine ili aweke mashairi yake baada ya kuonekana ule akibadili mashairi na yeye kuimba yale yale hautakuwa mzuri. Anasema baada ya hapo wakatengeneza wimbo mpya, Naumia, ambao ukaingia katika mzunguko na wakasubiri zamu yake ifike usambazwe.

Lakini anasema wimbo huo haukutoka sababu PNC na Dogo Janja walikuwa wakitoa kazi zao nyingi na yeye alihitajika kufanya kazi yake. “Nilitunga kazi yangu mwenyewe nikaingia studio na kuifanya, itafanya vizuri katika video,” anabainisha msanii huyo. Anasema wimbo huo ulikuwa unaitwa Bora Sioni, ambao ulifanya vizuri na kwa kiasi kikubwa aliitwa kwenye mahojiano ya redio na luninga na hata kupata matamasha machache.

Lakini baada ya kukamilika kazi hiyo, alianza kuugua kwa muda mrefu, akawa ameamua kuachana na muziki ili kujiuguza. Mwaka 2012, aligundulika kuwa na uvimbe ndani ya tumbo, akaanza kuingia kwenye mikakati ya kufanyiwa upasuaji. “Nilifanyiwa operesheni, lakini kabidi nikae kwa muda mrefu bila kujishughulisha na kazi ngumu, nikawa nimepumzika zaidi,” anasema.

Lakini wakati yupo katika hali ya kujiangalia afya yake, ndipo kundi likaingia kwenye matatizo makubwa na migongano iliyowafanya wasanii kusambaratika. Anasema sababu hiyo ilimfanya asitamani tena kujiunga na kundi lolote na kuona ni bora awe msanii huru atakayekuwa na meneja wake.

“Meneja wangu atakuwa kwa ajili ya kazi yangu peke yangu, na sikutaka kuhangaika na kundi la wasanii wengi kutokana na sababu nyingi nilizoziona nikiwa na kundi,” anaeleza. Alisema miongoni mwa sababu zilizomfanya kutotamani tena kuingia kwenye kundi ni kuepukana na mzunguko mkubwa kwa wasanii katika kufanya kazi, na kuchukua muda mrefu.

Balice anasema unaweza ukawa na kazi nzuri, lakini ikawa ndani ya mzunguko mrefu mpaka ifike zamu yako ya kuisambaza. Pia unaweza kufika muda wako wa kuisambaza, bosi akawa katika hali mbaya ya kifedha, jambo linalosababisha kazi hiyo isiwe ndani ya promosheni ya kutosha.

Anasema kingine ni meneja kuwa na watu wake ambao amekuwa akiwathamini kuliko wengine, jambo lililokuwa likimuumiza wasanii wengine. “Mnaweza mkawa mnafanya kazi nzuri, lakini baadaye ukashangaa kazi yake isifike mbali, kutokana na kukosa promo kutokana na wingi wa watu,” alisema.

Anasema wingi wa watu unawafanya baadhi yao kukosa nafasi, ingawa wanakuwa na kazi nzuri. Sababu nyingine inayomfanya kutotamani kuwa bila ya kundi kunatokana na kuyumba kwa kundi hasa kipindi kigumu. Anasema mara nyingi kundi huwa linapitia kwenye wakati mgumu, hali ambayo imekuwa ni ngumu kumsimamisha msanii mmoja mmoja.

“Kuna muda wasanii wenyewe mnakuwa na migogoro, hata kuwekeana fitina za hapa na pale hali inayopelekea kukosa nguvu ya kuweza kufanya kazi kwa moyo,” anaeleza. Pia anasema kwa kuwa msanii wa kike, wakati mwingine baadhi ya viongozi au wasanii wenzake humhitaji kimapenzi ili kumwinua kimuziki.

“Hilo halizuiliki kwa mtu yeyote hata kama sio msanii. Mtu anaweza kukuhitaji kukusaidia na baadaye kukupenda. Lakini pia mtu anaweza kukupenda kiukweli, na mwingine ikawa kwa ajili ya kukutumia,” anasema. Anasema mara nyingi amekuwa akiwaambia ukweli kuwa kama akiamua kumkubali kila anayemtaka, atakuwa na wanaume wengi kwani kila siku hufanya kazi na huhitaji msaada zaidi.

Kwa sasa, ameshakamilisha wimbo mpya, Liar (Mwongo) akiwa chini ya meneja wake, Hans ‘Hansi Q’ ambaye pia ni mtayarishaji wa kazi hiyo kupitia Kampuni ya Rocfame Music Group. Malengo yake ni kuwa msanii mkubwa atakayefanya kazi kimataifa zaidi. Happy Balice ni mwenyeji wa Dodoma, aliyemalizia elimu ya msingi katika Shule ya Msigani, Dar es Salaam na kusoma Shule ya Sekondari ya Morogoro.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Mohammed Mussa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi