loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

HAYA NDIO MAISHA: Tuwakuze watoto katika misingi ya kumjua Mungu

Hakuna ambaye anaweza kukana usemi huo, kwani ni kweli watoto wameumbwa katika hali ambayo ni rahisi wao kujifunza haraka mambo ama yawe mazuri au yawe mabaya, na hii inajidhihirisha kwa matendo wanayoyafanya tunapokuwa nao.

Mtoto anayejifunza mambo mazuri utaona anaiga na kufanya yaliyo mazuri, vilevile kwa mtoto aliyeona na kujifunza mabaya utaona akiiga hayo hayo mabaya aliyoyaona ama kutoka kwa wazazi, walezi au jamii inayomzunguka.

Kutokana na hali hiyo halisi ndio maana walezi, wazazi au watu wazima tunapaswa kuwajibika na kuwafundisha watoto habari za Mungu. Swali la kujiuliza Je, Mungu ni sehemu ya mazungumzo yako ya kila siku na watoto wako? Watoto wako wanamfahamu Mungu au neno la Mungu kwa kiasi gani? Au tumewekeza zaidi katika masuala ya dunia hii tu?

Wazazi au walezi wengi husisitiza watoto wao masuala ya elimu na maisha zaidi lakini wanasahau kumuweka Mungu mbele, kufundisha watoto umuhimu wa kumtegemea Mungu, kuwafundisha kuwa na hofu ya Mungu.

Weka mazingira ambayo yatawawezesha watoto waone ni jinsi gani unavyowekeza kwa Mungu katika kulisoma neno lake, kuomba, kuhudhuria ibada iwe kanisani au msikitini na kutumika katika kazi za Mungu.

Watoto wetu wanajifunza mambo mengi ambayo sio mazuri kwa maisha yao ya baadaye, lakini mtoto anayemjua Mungu sio rahisi kudanganyika au kutumbukia katika mambo mabaya, kwani tayari anakuwa umemjengea hofu ya kumuogopa Mungu.

Ukizungumza na mtoto wako kuhusu ukuu wa Mungu katika maisha ya kila siku utamjengea hazina kubwa ya imani kwa Mungu wake ambayo atakuwa nayo kila siku.

Pamoja na kuwahamasisha kupata maksi nzuri darasani, kujihusisha na michezo na kufanya kazi za nyumbani hakikisha unawafundisha kumtumikia Mungu katika umri wowote walionao. Neno la Mungu liwe sehemu ya maisha yako na watoto wako siku zote.

Sio siri katika dunia ya sasa kuna mambo mengi yanayoendelea katika jamii ambayo mengine sio mazuri kwa watoto wetu, kwa kumuelimisha hivi hivi tu anaweza asikuelewe lakini anapomtegemea Mungu ni rahisi kuyaepuka.

Sisi wengine tunashinda makazini, katika biashara au unakuwa safarini, watoto wanashinda na watu baki kama dada wa kazi au wasaidizi wengine na kadhalika, kuna baadhi yao wana tabia ambazo sio nzuri kwa hiyo mtoto anayemjua Mungu na anayejua mambo ya Mungu akiona jambo tofauti kutoka kwa watu hao atasema tu.

Ninao mfano wa mtoto mmoja ambaye mwenyewe ameshazoea kutazama katuni, kusikiliza nyimbo za injili na kutazama filamu za watoto au za masuala ya Mungu lakini siku dada wa kazi akiweka tu filamu zenye mambo tofauti na alivyozoea au akisikiliza muziki ambao sio wa dini utamsikia akiita, ‘mama mama huku dada anaangalia dunia” au wazazi wake wakirudi lazima aseme leo dada ameangalia filamu ya kutisha na mambo kama hayo.

Mtoto anayemjua Mungu huwezi kusikia akitoa neno chafu mdomoni, lakini wako watoto wana maneno machafu mpaka unashangaa, mtoto wa namna hii ni dhahiri hafahamu hata kama kuna Mungu.

Kimsingi wazazi, walezi msichoke kuwakuza watoto katika msingi wa kumfahamu na kumjua Mungu haijalishi ni wa dini gani. Watoto wakijengwa katika msingi huu watakuwa vijana na mabinti wazuri katika maisha yao ya baadaye.

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi