loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

HAYA NDIYO MAISHA: Ishi vyema na watu wote

Wengi wetu tumewahi kuishi nyumbani kwa ndugu na jamaa na wengine bado tunaoshi kwao maana kwa jamii yetu jambo hili halikwepeki.

Kuna changamoto katika kuishi na ndugu ama jamaa, na hizi changamoto ziko pande zote yaani kwa ndugu au jamaa unapoishi na yule anayekwenda kuishi hapo, hii ni kwa sababu kama wanadamu kila mmoja ameumbwa kwa tabia na hulka yake.

Unapokwenda kuishi na mtu ni vyema kwanza uisome familia hiyo na hasa mama mwenye nyumba nini hapendi, kinamkasirisha, kumkera au ni nini anapenda.

Kamwe huwezi kuishi kwa amani kwa mtu kama utaenda kinyume na mama wa hapo nyumbani au mazingira ya hapo nyumbani, kwa sababu kila familia ina mipango au taratibu zake. Jambo la msingi ni kuhakikisha unaishi kwa amani naye na kikubwa ni kumheshimu kama mzazi wako au wazazi wako.

Hakikisha pale unapoishi na ndugu au mtu waishi na wewe kwa kukutazama kama mmoja wa wanafamilia wakiangalia unakula, unalala upo salama inatosha, usitake makuu kama vile upo kwako au kwenu na kuanza kiburi sababu ya hili na lile.

Mshukuru Mungu kwa hilo na kama unapata ya ziada tambua ni kwa neema tu, kwa nini nasema ushukuru wako wengine wanatafuta sehemu ya kukaa wanakosa hata ndugu wa kumpa maji, wewe umepata basi kaa kwa heshima na adabu usilete kiburi na kujifanya mjuaji.

Wako watu wanakwenda katika nyumba za watu kuishi wanamdharau mama mwenye nyumba kama ndugu yao wa damu ni baba mwenye hiyo nyumba au wanamdharau baba mwenye nyumba kama ndugu yao ni mama mwenye nyumba, hii sio tabia nzuri hata kidogo.

Kumbuka heshima ni kitu cha bure, na tunaambiwa mkubwa amheshimu mdogo na mdogo amheshimu mkubwa, kwa hiyo haijalishi huyo ndugu au jamaa unayeishi naye yuko vipi, lakini kama umenyanyua mguuu kutoka huko ulikokuwa unaishi na kuamua kwenda kuishi nyumbani kwa watu lazima ujenge heshima.

Lazima ufahamu unavyowatendea wengine nawe utakuja kutendewa, onyesha moyo wa shukrani, uwe na bidii ya kazi na msikivu, hakuna mtu atakayeona shida kukaa na mtu msikivu, mchapakazi na mtii.

Mara nyingine mtu unakwenda na hisia zako tu kwa sababu tu yuko mwingine alishaishi hapo akatoka na maneno kibao kuhusu ndugu au jamaa, basi na wewe ukiingia umebeba taarifa hizo, unaingia kwa mbwembwe nyingi hata kabla hujaona ukifanyiwa ubaya wowote, hii sio tabia nzuri hata kidogo.

Wengi wanalalamika fulani ananitesa, fulani hanipendi lakini ukichunguza utaona wao ndio chanzo cha tatizo kwa sababu kasikia tu taarifa fulani haujui kuishi na watu, fulani anatesa ndugu n.k basi unakwenda umebebeshwa taarifa hizo na kuanza kiburi na kutosikiliza, unadhani ndugu au jamaa anayekaa nawe atafanyaje sasa?

Lazima naye atakugeukia na ndipo utakapoona unaonewa wakati uliingia na mambo yako kichwani. Kama ambavyo unamheshimu baba, mama na ndugu zako wa karibu, basi ukaheshimu hata wale ndugu, jamaa au rafiki unayekwenda kuishi naye, kwa sababu kamwe huwezi kujenga kiburi kwa mzazi au ndugu yako wa karibu.

Iwapo unakwenda kuishi kwa ndugu ambao ni familia, waheshimu kama unavyowaheshimu wazazi na ndugu zako na utaona ukibarikiwa kwa namna ya ajabu.

Wako watu wanaamini mtu au watu wa kuwaheshimu ni baba, mama na ndugu wa karibu, lakini lazima ufahamu hata mtu baki kama ni mtu mzima mheshimu kama baba au mama yako unavyomheshimu nyumbani, vile vile kama unavyowaheshimu na kuwajali ndugu zako wa damu iwe hivyo pia hata kwa watu baki.

Hakikisha wakati wote unaishi na kukaa na watu vizuri, ukitanguliza upendo, heshima na usikivu mbele, hakika utaishi sehemu yoyote bila tatizo, hata ukikabiliana na vikwazo au changamoto fulani hutaona tofauti kwa sababu utakuwa umejaa amani na furaha tele.

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi