loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

HAYA NDIYO MAISHA: Picha hizi za ajabu ajabu kwenye mitandao zina faida gani kwa jamii?

Ukatili umekuwa ukifanyika katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya familia hadi mazingira ya kijamii, watu wamekuwa wakifanyiana unyama wa kutisha, tena kwa sababu zisizokuwa na msingi wala maana yoyote.

Wakati haya yakiendelea kuna baadhi ya watu wamegeuza matukio haya kama sijui njia ya kujifurahisha au ndio mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia maana mimi binafsi naona kama kinachoendelea hivi sasa sio kitu kizuri na ni udhalilishaji.

Kwa nini nasema hivi, siku hizi yanapotokea matukio ya ukatili iwe watu kushambuliwa au kuuawa kwa ukatili kuna watu wamekuwa mstari wa mbele kupigapicha na kuzisambaza katika mitandao ya kijamii, jambo ambalo binafsi naona sio jambo zuri au jema kwa sababu hata kama mtu amekufa bado huko ni kumdhalilisha, hasa ukizingatia namna alivyopoteza maisha katika mazingira ya kikatili.

Hivi karibuni kulikuwa na habari ya mama aliyefanyiwa kitendo kibaya na mumewe ambaye alimchoma sehemu za siri kwa kile kinachodaiwa kumkuta na Shilingi 2000 ambazo mwanamume huyo alidai eti kahongwa, kwa kweli ni tukio la kusikitisha na kuhuzunisha kuona mtu mwingine anamfanyia ukatili mtu mwingine kwa kiasi hicho.

Lakini kibaya zaidi ni namna picha za mwanamke huyo zilivyokuwa zikisambazwa kwenye mitandao ya jamii, zikizonesha majeraha katika sehemu zake za siri, jamani ni picha za kumdhalilisha, hata wewe uliyetumiwa hazikusaidii kwa jambo lolote labda kama una roho mbaya ndio utazifurahia.

Tukio lingine ni la mwanamume ambaye inadaiwa alifumaniwa na kisha kupigwa shoka katika paji la uso, nazo picha zilikuwa zikisambazwa kwenye mitandao, au za tukio la kijana wa kazi aliyemshambulia mtoto wa bosi wake na kisha kula ubongo wake na yeye kujikata sehemu za siri.

Swali ninalojiuliza au kuwauliza Watanzania wenzangu hivi hizi ni picha za kufurahisha kweli watu kushabikia kusambaziana katika mitandao?

Kuna picha zingine kabisa ambazo zinatakiwa kuwa mikononi mwa hospitali ama polisi kutokana na unyeti wake, lakini cha ajabu zinafika katika mitandao ya kijamii, ndipo hapo maswali yanakuja je, ndani ya mamlaka hizi kuna baadhi ya watu wanakiuka maadili na kufanya kazi za kupigapicha kuzisambaza?

Kimsingi kwa kweli jamii inapaswa kuheshimiana na kuacha kujifurahisha kwa kutazama au kutumiana picha za ajabu ajabu ambazo hazina faida yoyote zaidi ya kujaza mambo ya kutisha ndani ya akili na moyo, na mwisho wake ndio hayo watu wanajifunza masuala ya ukatili.

Changamoto kwa mamlaka husika zinazohusiana na masuala ya mawasiliano, hivi hakuna utaratibu au njia ya kudhibiti vitendo hivi maana kwa kweli sio vizuri na mara nyingine ni kudhalilisha familia au watu waliokutana na majanga ya kufanyiwa vitendo hivi vibaya vya kikatili.

Naamini ni suala la ustaarabu na utu tu watu kuheshimiana na kuthaminiana na kuacha kufurahia kuangalia picha za matukio haya, kumbuka huyo aliyefanyiwa ni mwanadamu mwenzio na wala hakuomba au hakutarajiwa kufikwa na jambo kama hilo, sasa inapotokea tena anageuzwa sinema kiasi hiki haipendezi hata kidogo.

Vile vile wewe mtu mzima unayefanya mambo haya unamfundisha nini mtoto kuwa teknolojia ndio faida yake hiyo?au teknolojia ni kwa ajili ya mambo yenye manufaa kwa maisha yake.

Wewe mwenye tabia hii ya kupenda kusambaza picha za matukio hayo ya watu wanaofanyiwa ukatili, unapofikiria kufanya hivyo jiulize je ungekuwa wewe au ndugu yako wa karibu, ungejisikiaje? Jaribu tu kutafakari kama mtu mwenye utu na hekima na ukishajipima utapata jibu kama unachokifanya ni sawa au la.

Hivyo hivyo kwa wewe unayefurahia kupokea au kutumiwa picha za namna hivyo, na ukashabikia kuzitazama na kuzijadili, jiulize ungekuwa wewe watu wanakuangalia mitandaoni na kujadiliana ungejisikiaje? Usifanye kitu ambacho wewe binafsi usingependa kufanyiwa, ni somo dogo la kujitafakari na kujipima kiubinadamu.

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi