loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

HAYA NDIYO MAISHA: Walimu hawa wanafundisha maadili gani wanafunzi wao?

Nayasema haya kutokana na tukio ambalo nimelisikia kupitia chombo kimoja cha habari, nikajiuliza sasa tunajenga jamii ya namna gani iwapo hata wale tunaoamini wanachangia kiasi kikubwa kuwajenga watoto katika msingi mzuri na tabia njema ndio hao wanaoharibu watoto kwa kuwashirikisha kufanya mambo yasiyozingatia maadili na ya utovu wa nidhamu.

Yaani kilichonifanya kuyasema haya ni baada ya kusikia tukio redioni ambapo mzazi mmoja alikwenda kuulizia masuala ya mtoto wake katika shule ya moja msingi iliyopo Tabata, jijini Dar es Salaam lakini matokeo yake akajikuta akiambulia kuzomewa na kupigwa na mawe na wanafunzi baada ya kupata maelekezo kutoka kwa walimu wao.

Kwa maelezo ya mzazi huyo ambaye ni mama, kosa lake kubwa la kujikuta akiambulia hayo ni baada ya kuhoji risiti ambazo zilitokana na malipo waliyokuwa wakitoa kwa ajili ya ulinzi shuleni hapo, kosa lingine ni mtoto wake kumtaja mwalimu ambaye alimkataza mtoto huyo kutohudhuria masomo ya ziada (twisheni) wakati utaratibu wa shule mtoto anapaswa kulipia na kuhudhuria masomo hayo.

Katika kujadiliana huko mzazi na walimu akiwemo mwalimu mkuu walipishana lugha kidogo, hadi kufikia hatua ya mwalimu mmoja kumtishia mama huyo kuwa atampiga.

Hata hivyo, jambo baya zaidi wakati mzazi alipoamua kuondoka, ndipo Mwalimu Mkuu alipoamuru wanafunzi kumkimbiza mama huyo kwa mawe na kumzomea, ikumbukwe pia mama huyo mtoto wake anasoma katika shule hiyo hiyo.

Halafu vuta hisia wanafunzi wanapokuwa kundi kubwa walivyo na kelele na vurugu na amri inatoka kwa mwalimu, tena mwalimu mkuu.

Kama wewe ni mzazi au mama ungesikia wakati mama huyo akizungumza hakika ungetokwa na machozi, yaani watoto wadogo wanamkimbiza mama mtu mzima, kwa mawe na kumzomea, halafu walimu wanacheka wakifurahia kitendo hicho, hakika ni mazingira ya kudhalilisha sana.

Mama huyo alijaribu kukimbia na kupita vichochoro nakufanikiwa kuwakwepa wanafunzi, bado haikutosha watoto hao walifika nyumbani kwa mzazi huyo, wanapajua kwa sababu ya mwanafunzi mwenzao na kuanza kurusha mawe tena nyumbani, mpaka mzazi aliyekuwa amebaki nyumbani (baba sasa) kutoka nakushangaa naye ni vipi, ndipo wanafunzi hao wakatimka.

Kilichonisikitisha zaidi ni kumsikia mtoto wa mzazi huyo alipokuwa akihojiwa na kulia kwa uchungu kuwa alipoona mama yake anakimbizwa, yeye na rafiki yake walilazimika kubadilisha njia, lakini bado alikutana na wanafunzi wengine ambao walijitapa kwa kusema, ‘tumemkimbiza mama yako, tumemzomea na kumpiga jiwe la kichwa.”

Mtoto huyo wakati akiyasema haya alikuwa akilia kwa uchungu mkubwa. Kwa kweli kitendo walichofanya walimu hawa tena wakiongozwa na Mwalimu Mkuu kwangu ni kitendo cha kudhalilisha, fedheha na aibu kufanywa na walimu ambao walipaswa kuwa ndio wakufunzi wa wanafunzi juu ya kuheshimu wakubwa bila kujali ni mzazi wake au la.

Sio hivyo tu pia kisaikolojia walimu wamemuathiri mtoto ambaye mzazi wake alizomewa, hakika hatakuwa na hamu tena ya kurudi katika shule hiyo, lakini pia hatakuwa ana amani ya kukaa tena na wafunzi wenzake, kimsingi ni jambo baya ambalo halipaswi kufumbiwa macho.

Naamini wakati wote walimu na wazazi au walezi wanapaswa kuwa marafiki kwa sababu jukumu lao wote ni kuhakikisha watoto wanasoma na kupata elimu, lakini pia wanalelewa katika maadili mazuri ikiwa ni pamoja na kuheshimu wakubwa, lakini kwa haya yaliyotokea sijui walimu hawa wanawajengea wanafunzi taswira gani?

Kufuatia tukio hilo Msemaji wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu alipohojiwa alisema wanasikitika na kutoa pole kwa mzazi aliyefanyiwa kitendo hiki kibaya cha kudhalilishwa na kufedheheshwa na wanafunzi, lakini pia aliahidi kuwa kama halmashauri watafuatilia kujua kwa undani.

Msemaji huyo alisema yako maadili na taratibu zinazowaongoza walimu namna ya kuwasiliana na kuzungumza na wazazi yanapokuja masuala mbalimbali ya wanafunzi, hivyo basi kwa hili lililotokea naamini hatua stahili zitachukuliwa dhidi ya walimu wote waliohusika hata kama ni Mwalimu Mkuu, kwa sababu hata wanafunzi wakihojiwa walikuwa wanasema wametumwa na Mwalimu Mkuu.

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi