loader
Picha

Heko RITA kuwezesha usajili watoto

Ndiyo maana tunapoona Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) akitoa taarifa ya mafanikio katika kipindi kifupi tunaona vyema kuwapongeza.

Katika gazeti letu la leo tumeandika kwamba tathmini ya ujumla ya RITA inaonesha Mpango wa Usajili wa Watoto umefanikiwa sana kwani zaidi ya watoto 2,324,349 wamesajiliwa kupitia mpango huu na inategemewa watoto takribani 400,000 zaidi kusajiliwa katika mikoa ya Mara na Simiyu ambapo kampeni ya kuondoa bakaa imezinduliwa wiki hii.

Hiyo inatokana na kampeni kubwa kupitia Mkakati wa Kusajili Matukio Muhimu kwa Binadamu na Takwimu (CRVS) unaofanyiwa kazi sanjari na Mpango wa Kusajili na kutoa vyeti vya Kuzaliwa kwa watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano (U5BRP).

Mpango wa Usajili wa Watoto ulianzishwa na RITA na wadau wengine wa usajili kwa lengo la kuhakikisha katika kila eneo utekelezaji wake umeanza moja umewezesha kila mtoto anayezaliwa katika eneo hilo kusajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa ndani ya muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Tunapaswa kutambua kwamba Cheti cha Kuzaliwa ni nyaraka ya msingi ambayo kila mwananchi aliyezaliwa nchini anatakiwa kuwa nayo kwani imebeba taarifa nyingi za msingi ambazo humtambulisha aliye nacho.

Mathalani Cheti cha Kuzaliwa ingawa huonekana kama karatasi ya kawaida, lakini ni zaidi ya karatasi, kwani umuhimu wake hujidhihirisha pale mwananchi anapotakiwa kuthibitisha baadhi ya taarifa zake binafsi.

Kutokana na umuhimu wa cheti na kasi ya upatikanaji wa sasa, iliyowezeshwa na Mpango huu wa RITA uliowezesha kupeleka maboresho makubwa katika mfumo wa usajili kwa watoto na huduma za usajili wa watoto kusogezwa karibu na maeneo ya wananchi inastahili kuendelea kuungwa mkono kwa ushiriki wa wananchi.

Tunasema hivyo kwa kuwa hapo awali umbali kutoka maeneo ya makazi ya wananchi kwenda katika ofisi za wakuu wa wilaya imekuwa moja ya changamoto kubwa iliyosababisha wananchi wengi kutosajiliwa kutokana na gharama zinazoambatana na kufuatilia cheti.

Ingawa mpaka sasa Mpango huu umeanza na unaendelea kutekelezwa katika mikoa 11 ambayo ni Mwanza, Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe, Mtwara, Lindi, Geita, Shinyanga, Mara na Simiyu tunaamini kwamba utapelekwa mikoa yote ili kukamilisha kazi hii kwa mapema zaidi.

Tunaamini uwapo wa hatua za makusudi za kurahisisha usajili utaleta matunda zaidi kama alivyosema Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Emmy Hudson kwa kuwa kwenye mpango wa usajili wa Watoto vituo vinavyosajili kwa sasa ni vya kudumu hata baada ya kumaliza bakaa la watoto wasio na vyeti vya kuzaliwa.

Tunatoa wito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika mpango huu ili kuufanikisha na hivyo kuisaidia serikali katika mipango yake na pia wananchi kuwa na taarifa muhimu binafsi zinazowahusu wao katika nyaraka zinaoztambuliwa kisheria.

HAKUNA ubishi kwamba ili kuimarisha biashara yoyote ile duniani, zikiwemo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi